Jumatatu, 15 Julai 2013

29 wauawa Syria

Mashambulio ya ndege za kivita na makombora kutoka jeshi ya serikali ya Syria  dhidi ya vijiji kadhaa katika wilaya ya  kaskazini magharibi ya Idlib yamewauwa watu 29.
Ripoti za  Shirika linalokagua haki za binaadamu Syria lenye makao yake makuu mjini London-Uingereza, zimesema jeshi lilifanya hujuma tano tofauti, ikiwa ni pamoja na shambulio la roketi katika kijiji cha Maghara ,lililowauwa watu 13. Shirika hilo hutegemea  taarifa kutoka kwa wanaharakati, wanasheria na madaktari walioko sehemu mbali mbali ndani ya Syria.
Wakati huo huo, mjumbe maalum wa Katibu mkuu wa Umoja wa mataifa anayehusika na watoto  na mizozo ya silaha, Leila Zerrougui amewasili Syria leo kwa mazungumzo ya siku tatu  kuhusu vita vinavyoendelea nchini humo.
Mjumbe huyo atakutana na  maafisa wa serikali, wawakilishi wa Umoja wa mataifa na mashirika yasiyokuwa ya kiserikali. Ziara ya bibi Zerrougui ni sehemu ya ziara yake katika nchi kadhaa za eneo hilo  ambazo ni Jordan, Iraq, Uturuki na Lebanon, kwa lengo la kutathmini janga la watoto wa Syria na  familia zilizoathirika kutokana na vita hivyo.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni