Kwa ufupi
- Na katika wiki hii moja iliyopita, Makengeza, naona hii misimamo mitatu imesimama zaidi na zaidi. Ni dhahiri kwamba sipendi kabisa kuona uharibifu wa aina yoyote ile.
Jamani nchi yetu! Si salama na watu wakienda
huko usalama unahama kabisa. Ndiyo maana sishangai kupata barua lukuki
kutoka huko. Nimechagua moja tu.
Makengeza,
Nimeona mengi katika maisha yangu ndiyo maana siamini mengi. Lakini kuna mawili ambayo yanajidhihirisha kila wakati.
1. Mtu akipotosha ukweli makusudi, ujue maslahi yake yamo humu.
2. Mtu akihemka kupita kiasi ujue maslahi yake yameguswa pia.
Huko ninakokaa kijijini, kuna jirani mmoja ambaye
ni mhamiaji. Anawadharau wenyeji hakuna mfano. Anawatukana eti ni
wavivu, wajinga, hawana mawazo ya maendeleo, angekuwa na uwezo
angewafutilia mbali. Kumbe shida yake ni kwamba anataka kuweka bomba
yake mwenyewe kwenye chemchemu ya kijiji ili avute maji anavyopenda na
wanamzuia wakisema kwamba chemchemu kile ni kwa faida ya wenyeji wote
pale.
Huyu jirani anaona kwamba kwa kuwa ana pesa
zisizohesabika, ana haki ya kufanya apendavyo bila kuwajali wenyeji wa
eneo hili. Na anapoenda kwa wanene wenzie daima kazi yake ni kuwakashifu
viongozi wa kijiji eti wanaharibu vyanzo vya maji, wana ubaguzi dhidi
ya wahamiaji na kadhalika. Kumbe yeye ndiye mwenye ubaguzi na yeye ndiye
anayetaka kuharibu vyanzo.
Naam na hapo nakumbuka imani yangu ya tatu ya maisha.
3.Ukiona mtu anamshutumu mwenzie kwamba ana tabia fulani mbaya, bila shaka mshutumu yumo humohumo.
Kweli kabisa. Kwa nini atuhumu mwenzie anatembea nje bila ushahidi wowote kama na yeye hana tabia ileile?
Na katika wiki hii moja iliyopita, Makengeza,
naona hii misimamo mitatu imesimama zaidi na zaidi. Ni dhahiri kwamba
sipendi kabisa kuona uharibifu wa aina yoyote ile. Sipendi kuwaona watu
ambao huenda hawana hatia wanatiwa hasara katika maisha yao, iwe ni
kwamba wamepokonywa ardhi au mali yao na wanene wasio na huruma, iwe ni
kwamba wameharibu mali ya wenzao katika kumaliza hasira ya kupokonywa au
kudanganywa.
Inabidi niseme hivyo maana wanene wanapenda majibu
mepesimepesi kwenye masuala mazito. Kama yule aliyekuwa mdola wa Dar es
Salaam, ambaye alijaribu kumnyamazisha mtu yeyote anayejaribu kueleza
hali halisi ya wauza ngono eti ni wateja wao. Hii tabia ya kutoa kashfa
badala ya hoja inakera sana. Na hata katika hali hii ya sasa ukijaribu
kufunua pazia ili watu waone sawasawa, waambiwa na wewe mchochezi.
Tena hili neno mchochezi limetiwa mbolea hadi limesambaa kama
magugumaji. Hapa kijijini kwangu, ukiulizia mapato na matumizi huko
kijijini, unaitwa mchochezi, ukitaka kujua kwa nini mwenyekiti wa kijiji
ameporomosha bonge la hekalu huku shule ya ukata inazidi kukatika licha
ya michango ya wananchi, ni mpinzani, ni mchochezi. Ukihoji kwa nini
mwekezaji hawekezi bali anapora laivu, mchochezi. Na sasa ukisema
wananchi wa mahali fulani wana hoja, mchochezi pia. Funika hoja kwa
kuwakashifu wenye hoja.
Lakini hebu tuache kutafakari kifukara. Hata kama
wako wachache wanaopiga kelele eti gesi haitoki Mtwara ngo! Hili si dai
la wanaMtwara walio wengi. Wanajua hawawezi kula gesi au kulimia gesi au
kunywea gesi. Wana akili zao licha ya kashfa zote. Wao wanataka kufaidi
rasilimali iliyopo kwenye eneo lao. Sasa hapo kuna mambo mawili. Si
kweli kwamba wengine hawadai hivyo. Wanaoishi kandokando ya mbuga za
wanyama wanapaswa kulipwa kiasi fulani (hata kama haitoshi).
Wanaoishi karibu na migodi mikubwa wanadai
kuboreshewa miundombinu na huduma za jamii (hata kama haitoshi).
Wanaolima mazao mbalimbali wanataka mazao yao, kama pamba kwa mfano au
kahawa, yashughulikiwe palepale. Kwani kiwanda cha kahawa kiko Dodoma?
Vinu vya pamba viko Mtwara? Kwa hiyo dai lao ni sawasawa na madai ya
watu kila mahali Tanzania. Wafaidi wao kwanza siyo badala ya wananchi.
Pili, wana ugonjwa unaoitwa katika ung’eng’e
ahadiosis … yaani uahadizi. Wamesikia ahadi nyingi kiasi kwamba ahadi
zinawadhuru maana wamekata tamaa na hizi ahadi. Ni ugonjwa mbaya maana
huleta homa ya ubongo, huchemsha bongo hadi washtuka wameingia mitaani
katika kujaribu kutuliza jinsi ubongo unavyochemka.
Ndiyo maana wakiona mipango inaendelea kama awali
huku ahadi zinamwagwa wanaona kwamba wanadanganywa. Na siyo wao tu.
Wafugaji sehemu nyingine ni vivyohivyo na wachimbaji wadogo sehemu
mbalimbali vilevile. Wanaona mifano lukuki kila siku. Kwani haya
mashangingi yote yanatokana na nini?
Tatu, wanene wanapodai kwamba maliasili ni mali ya
Wabongo wote, wanasema kweli? Kwelikweli. Ni mali ya mwanakijiji wa
Tanganyika huko au ni mali ya wanene wenyewe tu? Hii siyo sababu kwa
nini wamehemka hadi wanatoa povu? Wanaona kwamba wana asili ya mali,
ndiyo maana rasilimali ya wote kiasili ni wao. Ndipo hapo niliposema
ukiona mtu anamshtumu mwenzie tabia fulani, ujue anayo yeye.
Nne, Waswahili wamesema siku nyingi. Afichaye
ugonjwa, mauti humfichua. Wale waliopewa jukumu la kulinda amani ndani
ya nchi wamefichiwa magonjwa yao miaka nenda rudi. Hebu angalia tafiti.
Nani ana imani nao. Nani anaamini kwamba akienda kutoa taarifa kwao
hatatolewa upepo bila hata kushughulikiwa? Nani haongelei suala la
rushwa miongoni mwao? Hii ni hatari sana. Maana kwa imani yangu huwezi
kulinda usafi wa eneo kama wewe mwenyewe ni mchafu. Na iwapo
umeshadharaulika kutokana na uchafu wako, hautasikilizwa, wala
kuheshimiwa. Lakini wameachiwa kuendelea kujichafua hadi basi. Kwa hiyo,
badala ya kutumia jeshi letu kulinda nchi dhidi ya maadui wa nje
tunawatumia dhidi ya raia wenzetu. Hatari kwelikweli.
Lakini zaidi ya yote, watu wakilipuka kwa wingi,
huwezi kudhibiti hali kwa mkong’oto. Ni hesabu rahisi sana. Ukimkung’uta
mmoja, umeshachokoza wenzake wanne ambao hawapendi kuona uonevu huo.
Kwa hiyo wanaamka na wao inabidi kuwakong’ota wote hao wanne. Na wao pia
wana wanne wao watakaokasirika pia yaani watu kumi na sita.
Wakikong’otwa na wao, ni watu sitini na nne … baada ya hapo mia mbili
hamsini na sita, kisha 1024, kisha 4096 …. na kadhalika. Huwezi
kuyafunika maji yakianza kububujika. Hivi, Msumbiji Kaskazini wana gesi
kuliko sisi? Mbona hatusikii fujo za namna hiyo?
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni