Msanii wa filamu Elizabeth Michael maarufu kama Lulu akiweka shada la
maua kwenye kaburi la aliyekuwa msanii mwenzake Steven Kanumba wakati wa
kumbukumbu ya mwaka mmoja tangu kifo chake.
In Summary
- Msanii huyo anakiri alitamani kuhudhuria mazishi ya mpenzi wake huyo, lakini haikuwa rahisi kwani alikuwa rumande.
MWIGIZAJI wa filamu Bongo,
Elizabeth Michael ‘Lulu’, amezungumzia historia ya maisha yake na
matukio aliyopitia katika umri wake ambao katika hali ya kawaida ni
mdogo kwa mhusika kuwa gumzo kwenye jamii.
Lulu alijikuta akiwa mahabusu ya Segerea baada ya
mpenzi wake Steven Kanumba kufariki akiwa naye. Wengi walishangaa na
kutoamini kuwa wasanii hao walikuwa wapenzi kwani jambo hilo halikuwahi
kujulikana.
Uhusiano na Kanumba
Lulu anasema yeye na marehemu walikuwa na uhusiano
wa kimapenzi kwa muda mrefu, lakini moja ya makubaliano yao ilikuwa ni
kuishi katika maisha ya siri hiyo. Katika hilo hataki kuzungumzia undani
wa siri iliyokuwapo baina yao.
“Mapenzi yangu na Kanumba ilikuwa ni makubaliano
yetu kufanya iwe siri, nadhani haikuwa na maana kwetu, mapenzi yalikuwa
ya muda mrefu, lakini sitaki kuzungumzia uhusiano wetu kutokana mambo
mengi yamepita,” anasema.
Msanii huyo anakiri alitamani kuhudhuria mazishi ya mpenzi wake huyo, lakini haikuwa rahisi kwani alikuwa rumande.
Anasema maisha ya mahabusu yamemjenga na kumfanya
kuwa mtu tofauti. Anasema sasa anaona kuwa anao wajibu wa kutumia muda
wake kupitia filamu, kuwaelimisha vijana na watu wazima kuhusiana na
maisha.
Katika hilo anasema anaandaa filamu mbili ikiwamo ya ‘Mapenzi Ya Mungu’.
Anasema ‘Mapenzi Ya Mungu’ ameigiza kwa kushirikiana na Mama mzazi wa marehemu Kanumba (Flora Mtegoa).
Anasema filamu hiyo inaeleza kuhusu maisha yake
alipokuwa rumande, kikubwa hapo anasema maisha ya huko yamemfanya amjue
Mungu zaidi.
Lulu anasema kuwa filamu yake ambayo ipo tayari
inasubiri kuzinduliwa wakati wowote ni ya ‘Foolish Age’ inayoelezea
maisha yake na majanga aliyopitia.
Anaamini kuwa wakati mtu anapokuwa katika umri
mdogo, anaweza kufanya mambo ya hatari ambayo si rahisi kabisa
kuyabaini kwa muda huo na hata kama akionywa hawezi kuelewa.
“Filamu ya Foolish Age inazungumzia jambo ambalo nina uzoefu
nalo. Unajua katika umri wa namna hiyo mhusika anakuwa mbishi, hasikii
hata akiambiwa,” anasema.
“Kupitia filamu hiyo ninaweza kuwafundisha watu
mambo muhimu, nitafurahia kama nitawaokoa hata watu kumi kupitia kile
nilichopitia mimi.”
Uhusiano na Mama Kanumba
Maisha ya Mama Kanumba na Lulu yamekuwa ya
maelewano hata kuweza kuwafanya Mama Kanumba na Mama Lulu kuwa pamoja
kwa nyakati tofauti.
Lulu anasema kuwa sasa wanaishi kama familia moja
kila mtu anaelewa kilichotokea, ndio maana katika kuonyesha hilo
wameigiza filamu pamoja.
Unapozungumza na Lulu kwa sasa, utabaini
mabadiliko makubwa kwake kwani anaonyesha jinsi anavyoweza kuwafundisha
wengine kupitia katika maisha yake.
Anasema awali alipoingia rumande alikuwa na mawazo mengi, lakini baadaye aliukubali ukweli na kujikuta akinenepa.
Marafiki
Kwake anahisi hajawahi kuwa na marafiki kwani ni
vigumu sana kumjua rafiki wa kweli. Anasema katika mazingira yake huwa
anakutana na watu kwa ajili ya kazi.
“Ninashindwa kufahamu kama ni kweli nina marafiki
au la, hata wale walioshindwa kuungana nami katika shida siwezi
kuwalaumu,” anasema.
Mipango yake
Ni kumiliki kampuni ya utengenezaji filamu na
kutayarisha filamu zake. Kwake jambo kubwa ni kuwa msanii mahiri
atakayeitangaza nchi yake ya Tanzania na kuvuma ulimwenguni kote
“Ninataka kuwa mfano kwa nchi yangu, kama ilivyo kwa Genevieve
Nnaji au Noah Ramsey wa Nigeria, wameitangaza sana nchi yao wale,
nafikiri nami wakati wangu umefika,” anasema.
Lulu anasema kuwa pamoja na wasanii hao kuwa mbali, lakini wanajulikana kila kona kutokana na ubora wa kazi zao.
source---mwanasport gazeti
source---mwanasport gazeti
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni