Umoja wa Afrika, zamani ukiitwa Umoja wa Nchi Huru za Afrika
(OAU), unaadhimisha miaka 50 tangu kuundwa kwake, ukiwa na hadithi ya
mafanikio na mapungufu, lakini ukisalia na dhamira ya kusonga mbele.
Tarehe 25 Mei 1963: Mataifa 30 huru ya Afrika yakutana
katika mji mkuu wa Ethiopia, Addis Ababa, kuanzisha Umoja wa Nchi Huru
za Afrika (OAU). Lengo: umoja wa bara hilo na pia uhuru na mamlaka ya
wanachama wake. Mwaka huo huo, OAU inaunda Kamati ya Ukombozi yenye
makao makuu yake nchini Tanzania, ambayo inaunga mkono mapambano dhidi
ya utawala wa wachache Namibia na Afrika ya Kusini.
1976: Mtawala wa kijeshi wa Uganda, Idi Amin, atangazwa
kuwa rais wa maisha. Ukatili wake dhidi ya kiasi cha wahanga 400,000
wapelekea kuvunjwa kwa sera ya OAU ya kutokuingilia mambo ya ndani ya
nchi.
1980: OAU yazindua kile kilichoitwa
“Lagos Plan of Action” yaani Mpango Kazi wa Lagos” nchini Nigeria.
Mpango huo wadhamiria kuongeza ushirikiano wa kikanda na kutandika
msingi wa Jumuiya ya Uchumi ya Afrika. Mafanikio yake hayakuweza
kuonekana mara moja.
1985: Morocco yajitoa rasmi kwenye OAU ikilalamikia
kuruhusiwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kiarabu ya Sahrawi (Sahara ya
Magharibi) kujiunga na Umoja huo mwaka 1982. Kundi la waasi wa Polisario
lilikuwa limejitangazia uhuru wake kutoka Morocco na kuunda jamhuri na
kuanzisha serikali wakiwa uhamishoni.
1989: Kamisheni ya Haki za Binaadamu na Watu ya OAU yaundwa rasmi.
1991: Mataifa wanachama wa OAU
yaanzisha “Jumuiya ya Uchumi ya Afrika” kwa lengo la kuwa na uchumi
mmoja wa Afrika kufikia mwaka 2025 kwa kuigiza mfano wa Jumuiya ya
Kiuchumi ya Ulaya ambayo ilikuwa muasisi wa Umoja wa Ulaya.
1994: Baada ya kumalizika kwa utawala wa kibaguzi, Afrika ya Kusini yajiunga na Umoja.
1999: Katika mkutano maalum wa kilele mjini Sirte
(Libya, OAU inajadili uundwaji wa Umoja wa Afrika wenye malengo mamoja
ya kisiasa kama vile Umoja wa Ulaya. Wazo hilo lilitokana na Muammar
Gaddafi aliyekuwa kiongozi wa Libya kwa wakati huo.
2000: Kuelekea enzi mpya: Katika
mkutano mjini Lome, Togo, viongozi wakuu wa mataifa ya OAU wanasaini
makubaliano ya kuasisi Umoja wa Afrika (AU). Kwa mujibu wa Kifungo Namba
30 cha mkataba huo, serikali zilizoingia madarakani kwa njia isiyo ya
kidemokrasia zitengwe na Umoja huo.
2001: Sasa OAU inaitwa rasmi Umoja wa Afrika na ina
wanachama 53. Morocco haijiungi na AU kwa sababu ya mgogoro unaoendelea
kwenye Sahara ya Magharibi. OAU na AU zinaendelea kuwapo kwa pamoja
katika kipindi cha mpito cha miaka miwili. Vyombo vikuu vya Umoja wa
Afrika ni mkutano mkuu wa kilele wa viongozi wa mataifa wanachama na
uwenyekiti unaozunguka kila mwaka. “Jumuiya ya Uchumi ya Afrika” inakuwa
sehemu ya AU.
2002: Baraza lililoasisi AU linakutana Durban (Afrika ya Kusini). Makao makuu ya umoja huo yabakia Addis Ababa (Ethiopia).
2003: AU yaanzisha Baraza la Usalama
kama lile la Umoja wa Mataifa. Linaundwa na wawakilishi 15 wa
kuchaguliwa kutoka mataifa wanachama na linaweza kufanya operesheni za
kuingilia kati kijeshi na za kulinda amani barani Afrika dhidi ya
matakwa ya taifa mwanachama.
2004: AU yafungua “Bunge la Afrika” mjini Midrand
(Afrika ya Kusini). Sasa lina wajumbe 265 waliochaguliwa kutoka mataifa
wanachama. Lengo la bunge hilo ni kutekeleza siasa na malengo ya AU na
kukuza demokrasia na maendeleo ya uchumi. Bunge hilo ni chombo cha
ushauri tu na halina nguvu ya kutunga sheria. Mwaka huo huo, Umoja wa
Afrika watuma wanajeshi katika mkoa wenye migogoro wa Darfur kupitia
kikosi chake cha AMIS (Kikosi cha Umoja wa Afrika nchini Sudan) na
UNAMID (Kikosi cha Umoja wa Mataifa jimboni Darfur).
2005: Somaliland ambayo ni sehemu ya kaskazini mwa
Somalia, yawasilisha ombi la uwanachama kwa AU. Mkoa huo hautambuliwi
kimataifa kama dola na hakuna dalili kwamba kwa siku za karibuni
Somaliland itaweza kujiunga na AU.
Taifa la Kaskazini Magharibi ya Afrika, Mali, linavuliwa uwanachama wake
kwa muda kutokana na mapinduzi ya kijeshi. Baada ya uchaguzi wa mwaka
2007 larudishwa tena lakini laondolewa tena kwa muda baada ya mapinduzi
mengine ya kijeshi ya mwaka 2008.
2006: Kutokana na Azimio 1725,
Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa linaruhusu kupelekwa kwa Kikosi
cha Kulinda Amani cha Umoja wa Afrika nchini Somalia (AMISOM). Kufikia
mwishoni mwaka 2012, idadi ya wanajesji wanaoilinda serikali ya Somalia
yaongezeka hadi 17,000.
2009: Kutokana na kanuni yake ya uwenyekiti
unaozunguka, kiongozi wa Libya, Muammar Gaddafi anakuwa rais wa AU.
Wakati wa uwenyekiti wake, anapigania kwa nguvu dira yake ya “United
States of Africa”. Afrika ya Kusini ni miongoni mwa mataifa
yanayopingana vikali na wazo hilo.
2012: Waziri wa Mambo ya Ndani wa Afrika ya Kusini,
Nkosazana Dlamini-Zuma, awa mwanamke wa kwanza kwenye historia ya umoja
huo kuchaguliwa kuwa mkuu wa Kamisheni ya AU. Ni nafasi ya juu kabisa
kwenye umoja huo.
2013: AU ina wanachama 54, yaani nchi zote za Kiafrika
isipokuwa Morocco. Sahara ya Magharibi ni mwanachama kamili wa AU lakini
si mwanachama wa Umoja wa Mataifa wala haitambuliwi rasmi kuwa dola.
Hata mengi ya mataifa ya AU hayaitambui Sahara ya Magharibi kama dola.
Uwanachama wa Jamhuri ya Afrika ya Kati umesitishwa tangu kufanyika kwa
mapinduzi ya kijeshi mwezi Machi 2013. Guinea Bissau na Madagascar pia
zimesitishwa uwanachama.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni