Timu ya wataalamu wa Umoja wa
Mataifa wa silaha za kemikali imewasili mjini Damascus Syria leo ili
kuchunguza kama silaha hizo hatari zimetumika katika vita vya ndani
nchini humo au la. Serikali ya Rais Bashr al- Assad imesema makundi ya
kigaidi yanayoungwa mkono na madola ya kigeni yametumia silaha hizo
dhidi ya raia huku Marekani ikiielekezea serikali ya Damascus kidole cha
tuhuma kuwa ndiyo iliyotumia silaha hizo. Kama ulivyo mgogoro wenyewe
wa Syria kadhia ya utumiaji silaha za kemikali nayo pia imeyagawa madola
makuu ya dunia. Wakati Russia inasisitiza kwamba waasi walitumia gesi
aina ya sarin katika mji wa Aleppo mnamo mwezi Machi mwaka huu, Marekani
inadai kwamba vikosi vya serikali ya Syria vilitumia japokuwa ni kwa
kiwango kidogo silaha za kemikali dhidi ya waasi.
Timu hiyo ya wataalamu 20 wa Umoja wa
Mataifa inayojumuisha wataalamu kutoka Shirika Linalopiga Marufuku
Silaha za Kemikali (OPCW) inaongozwa na mwanasayansi kutoka Sweden Ake
Sellstrom. Kwa mujibu wa timu hiyo, watakachofanya ni kujaribu kubaini
kama silaha za kemikali ikiwemo sarin na gesi nyengine za sumu
zimetumika katika vita vya Syria na si kutaka kujua ni nani aliyetumia
silaha hizo. Wataalamu hao wa silaha za kemikali watafanya uchunguzi
katika eneo la Khan al- Assal na sehemu nyengine mbili ambazo bado
hawajaziainisha…
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni