Madaktari wakimfanyia mtu upasuaji wa kurekebisha ukubwa wa titi
Na Vicky Kimaro, Mwananchi
Inawezekana hufurahii umbo ulilozaliwa nalo. Kama ndivyo sasa teknolojia hiyo tayari imeingia nchini.
Miaka ya hivi karibuni, kumeibuka wimbi kubwa la
wanawake kwa wanaume ambao wanafanyia matengenezo maumbile yao ‘Plastic
Surgery’ kama sura, kupunguza vitambi, kuongeza makalio, kuongeza au
kupunguza matiti.
Awali wimbi hili lilibuka zaidi kwenye nchi za
magharibi, lakini kutokana na utandawazi, dunia kuwa kijiji, kwa hivi
sasa watu wengi wamekuwa na mwamko wa kutengeneza shepu katika sehemu
mbalimbali za maumbile yao.
Kwa hapa Tanzania, watu wengi hukimbilia nchini
India kwenda kufanya upasuaji wa aina hii ambao wengi wao wanafanya
aidha kwa kujua au kwa kutokujua madhara yake, lakini lengo kuu ni
kujipendezesha na kuonekana mwenye mvuto machoni mwa watu.
Dk Zaituni Sanya bingwa wa upasuaji Hospitali ya
Taifa Muhimbili alifanya mahojiano maalum na Mwandishi wa habari hizi na
kusema: “Kwa hapa Tanzania upasuaji unaofanyika ni ule wa kurekebisha
sura na ule wa matiti ndiyo sana.”alisema
Akifafanua zaidi alisema: “Kwa upande wa sura
upasuaji tunaofanya ni kwa wale ambao utakuta wameota vinyama au wana
uvimbe uvimbe kwenye sura, ndiyo tunawafanyia na tena upasuaji wake
unatumia nyuzi nyembamba sana maalumu ambazo hazionekani, lakini ule wa
kuchonga sura kama ule uliokuwa ukifanywa na kina Michael Jackson
hatufanyi.
“Upasuaji wa matiti ndiyo tunafanya sana hapa
nchini, mimi binafsi ninafanya na kwa hapa Muhimbili gharama zake ni
zilezile kama za upasuaji mwingine wowote, lakini kwenye hospitali za
binafsi upasuaji huu ni gharama sana.
“Wengi wanaokuja hapa unakuta niwasichana kuanzia
umri wa miaka 20 hadi 35 na hawa wanakuja siyo kwamba wanaumwa la hasha,
wanafanya upasuaji huu kwa ajili ya urembo tu, unakuta matiti yao ni
makubwa hivyo wanakuja kwa lengo la kuyapunguza.
“Matiti makubwa yanasababishwa na chembe chembe
ambazo zinatengeneza mafuta na kuyafanya kuwa makubwa kupita kiasi,
tunapofanya upasuaji tunaondoa mafuta yaliyozidi na kuliweka titi kwenye
umbo zuri ambalo mhusika atataka na kwa saizi ambayo atapendelea, na
pia wakati wa kushona inabidi uangalifu sana ili isisababishe madhara.
Mbali na kupunguza wanaongeza?
“Kwa hapa Tanzania hapana, toka nimeingia kwenye
udaktari wa upasuaji mwaka 2004 sijapata mgonjwa ambaye anahitaji
kuongeza ukubwa wa matiti zaidi ni kuyapunguza, na hii si tu kwa hapa
Muhimbili bali pia kwenye hospitali kubwa zote za watu binafsi hakuna
wagonjwa wa aina hii zaidi ya wale wanaohitaji kupunguza.
Hata hivyo Dk Sanya alisema kuwa hana takwimu
sahihi za idadi ya watu ambao wanaenda kwa ajili ya tatizo hilo zaidi ya
umri ambao wengi wao ni wasichana kati ya miaka 20 hadi 35.
“Upasuaji wa kupunguza matiti hauna madhara yoyote
kwa vile tunapunguza chembe chembe zilizozidi pamoja na mafuta na
hatutumii kemikali zozote. Ila kama upasuaji wake utakosewa basi madhara
ambayo muhusika atapata ni kuwa hatoweza kumnyonyesha mtoto na kama
mnavyojua matiti yakijaa misuli inapanuka na hivyo ni lazima mhusika
atapata maumivu makali ambayo yatatibiwa na dawa za kutuliza maumivu.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni