Mazungumzo ya kuunda baraza la mawaziri Misri yaendelea

Waziri Mkuu mpya wa Misri  Hazem al-Beblawi amepanga kuwa na mazungumzo zaidi hii leo ya kuunda baraza jipya la mawaziri huku waendesha mashtaka nchini humo wakichunguza malalamiko ya uhalifu dhidi ya kiongozi aliyeondolewa Mohammed Mursi pamoja na wanachama wa chama chake cha Udugu wa Kiislamu.
Hapo jana Al-Beblawi akiwa pamoja na makamu wa rais Mohammed El Baradei alifanya mazungumzo na wateule wa nafasi za uaziri. Huenda baraza hilo jipya la mawaziri linalotarajiwa kuwa na wizara 30 likaundwa siku ya Jumanne ama Jumatano wiki ijayo.
Tayari Mwanasiasa wa mrengo wa kushoto Godah Abdel Khalek amekataa nafasi aliyopewa ya kuwa waziri wa ugavi katika serikali ya mpio. 
Wakati huo huo waendesha mashtaka nchini humo wamesema malalamiko dhidi ya Mursi yanahusisha kuchochea ghasia, kufanya upelelezi na hata kuharibu uchumi wa Misri. Ofisi ya Mwendesha mashtaka hata hivyo haikusema ni nani aliyewasilisha mashtaka hayo.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni