Maafisa nchini Sudan wamesema wanajeshi saba wa kulinda amani wa Umoja wa Mataifa wameuwawa huku wengine 17 wakiachwa na majeraha baada ya kuvamiwa hapo jana kusini mwa jimbo la Darfur.
Jeshi la pamoja la Umoja wa Mataifa na Umoja wa Afrika (UNAMID) lilishambuliwa na kundi kubwa la watu wasiojulikana karibu kilomita 25 Magharibi mwa eneo la Khor Abeche, ilipo kambi ya jeshi hilo.
Umoja wa Mataifa umesema waliofariki ni wanajeshi wa kulinda amani kutoka Tanzania na waliojeruhiwa ni wanajeshi na polisi wakiwemo wanawake wawili ambao ni washauri wa kipolisi.
Mwakilishi maalum wa jeshi la pamoja la UNAMID Mohamed Ibn Chambas amelaani vikali shambulizi hilo na kusema kwamba waliolifanya watasakwa na kushtakiwa kwa uhalifu huo ambao unavunja sheria za kimataifa zinazolinda haki za kibinaadamu.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni