Jumatatu, 10 Juni 2013

Siyo wakati wa Taifa Stars kukata tamaa


Kwa ufupi


•Hivi sasa Taifa Stars imebakisha mechi mbili katika hatua hii ya makundi ambazo ni dhidi ya Ivory Coast itakayofanyika jijini Dar es Salaam na dhidi ya Gambia itakayofanyika huko Banjul.



Juzi timu yetu ya taifa ya Soka ‘Taifa Stars’ ilifungwa na Morocco mabao 2-1 katika mechi muhimu ya kuwania tiketi ya kufuzu kushiriki Fainali za Kombe la Dunia 2014 zitakazofanyika huko Brazil.



Katika mechi hiyo iliyochezwa kwenye Uwanja wa Marrackech huko Morroco, vijana wa Taifa Stars walijitahidi kupambana katika mechi kutafuta ushindi, lakini bahati haikuwa yao. Kwa matokeo hayo, Taifa Stars imeendelea kushika nafasi ya pili katika Kundi C ikiwa nyuma ya Ivory Coast yenye pointi 10 huku Morroco ikishika nafasi ya tatu ikiwa na pointi tano na Gambia ipo nafasi ya mwisho ikiwa na pointi moja. Hivi sasa Taifa Stars imebakisha mechi mbili katika hatua hii ya makundi ambazo ni dhidi ya Ivory Coast itakayofanyika jijini Dar es Salaam na dhidi ya Gambia itakayofanyika huko Banjul.



Mechi kati ya Taifa Stars dhidi ya Ivory Coast itachezwa Juni 16 ambayo ni Jumapili hii kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam, ambapo kama Taifa Stars ikishinda mechi hii itakuwa imefikisha pointi tisa na kuikaribia Ivory Coast ambayo mechi yake ya mwisho itacheza na Morooco huko Abidjan.



Sisi tunaamini huu wa siyo wakati sahihi kwa vijana wa Taifa Stars na mashabiki wa soka nchini kukata tamaa kwani matumaini ya kufanya vizuri katika hatua hii ya makundi na kutinga raundi ya tatu ambayo ni hatua ya mtoano bado yapo.



Kama watu wanakumbuka vizuri, watakumbuka kuwa Stars ilianza kushiriki mashindano haya tangu raundi ya kwanza, ambapo mechi ya kwanza Stars ilicheza ugenini 2011 dhidi ya Chad na kuibuka na ushindi wa mabao 2-1, lakini timu hizo ziliporudiana jijini Dar es Salaam, Stars ilichapwa 1-0 hata hivyo ilisonga mbele na kuingia hatua ya makundi ambayo ni raundi ya pili.



Katika raundi ya pili tayari Taifa Stars imecheza mechi nne, ambapo mechi ya kwanza ilichapwa 2-0 na Ivory Coast ugenini, mechi ya pili Taifa Stars iliichapa Gambia 2-1 nyumbani, mechi ya tatu Taifa Stars iliichapa Morocco 3-1 nyumbani na mechi ya nne Taifa Stars imefungwa 2-1 na Morocco ugenini.



Ni wazi Taifa Stars baada ya juzi kukubali kufungwa na Morocco imejiweka katika wakati mgumu wa kuingia 10 bora au raundi ya tatu, kwani yapo makundi kumi na kila kundi linatakiwa kutoa mshindi wa kwanza kuingia hatua hiyo ya raundi ya tatu ambayo ni hatua ya mtoano, ambapo katika kundi la Taifa Stars timu ya Ivory Coast hivi sasa ina nafasi kubwa kwani ina pointi 10 na imebakisha mechi dhidi ya Taifa Stars na mechi dhidi ya Morocco, ambapo itakuwa nyumbani.



Lakini, hata hivyo siku zote mpira unadunda, na ndiyo maana tunasema huu siyo wakati wa wachezaji na mashabiki wa soka Tanzania kukata tamaa kwani lolote linaweza kutokea.



Sisi tunaamini kuwa katika mechi ya Jumapili dhidi ya Ivory Coast, wanachotakiwa kufanya wachezaji wa Stars ni kujiamini, kujituma kwa kucheza bila hofu wakitambua kuwa wanakumbana na timu yenye wachezaji wengi wanaocheza soka ya kulipwa Ulaya, lakini inafungika na ndiyo maana hadi sasa haijajihakikishia kuingia raundi ya tatu.



Tunaamini wachezaji wa Taifa Stars watakuwa na uzalendo, umoja na lengo moja, kwa sababu siku zote lengo moja huleta ushindi, na ushindi utaiweka Taifa Stars katika nafasi nzuri katika kundi lake.



Tunatarajia wachezaji wa Taifa Stars wataendelea kutekeleza wajibu wao wa kuliwakilisha taifa na kuwafurahisha Watanzania hasa katika mechi ya Jumapili dhidi ya Ivory Coast, pia tunatarajia mashabiki wengi wa soka watajitokeza Jumapili kuishangilia Taifa Stars.





Hakuna maoni:

Chapisha Maoni