
Jaji Joseph Warioba
Kwa ufupi
- Hivyo, siyo kweli kwamba vyombo vya habari havikuwaeleza wananchi kinagaubaga kwamba mchakato wa kupata Katiba Mpya bado unaendelea.
Tangu Rasimu ya Katiba Mpya ilipozinduliwa wiki moja iliyopita, vyombo vya habari vimekuwa vikichapisha na kutangaza vifungu nyeti mbalimbali vilivyomo katika Rasimu hiyo. Lengo limekuwa siyo tu kuwafahamisha wananchi kuhusu vipengele mbalimbali vilivyomo katika Rasimu hiyo, bali pia kuanzisha mjadala wa kitaifa ili hatimaye ipatikane Katiba bora inayotokana na wananchi wenyewe.
Bahati mbaya baadhi ya watu wameutafsiri mwenendo huo wa vyombo vya habari kama hatua ya kuwapotosha wananchi ili waione Rasimu hiyo kama Katiba Mpya. Kwamba vyombo hivyo vinajenga dhana kwamba Rasimu hiyo ni kilele cha mchakato wa kupata Katiba Mpya, hivyo wananchi wanaweza kupumbazika kwamba zoezi hilo sasa limefikia tamati.
Inawezekana kabisa kwamba dhana hiyo imejengeka kutokana na wananchi wengi kuijadili Rasimu hiyo kwa hamasa kubwa, huku baadhi ya wanasiasa na viongozi katika ngazi mbalimbali nchini wakikumbwa na kiwewe na mfadhaiko mkubwa kwa hofu kwamba Rasimu hiyo ni kiama chao cha kupoteza nafasi za uongozi.
Hivyo, siyo kweli kwamba vyombo vya habari havikuwaeleza wananchi kinagaubaga kwamba mchakato wa kupata Katiba Mpya bado unaendelea. Tangu Rasimu hiyo izinduliwe na Makamu wa Rais, Dk Mohamed Gharib Bilal wiki iliyopita, vyombo hivyo vimekuwa vikiwasisitizia wananchi pasipo kuacha shaka kwamba mchakato huo ndio kwanza unaanza na kwamba bado kuna mijadala ya Mabaraza ya Katiba, Kura ya Maoni na hatimaye Bunge la Katiba.
Hata hivyo, jambo kubwa linalojitokeza hapa ni kwamba wananchi, baadhi ya wanasiasa na viongozi katika ngazi mbalimbali wanauona mjadala wa Rasimu hiyo kuwa muhimu zaidi pengine kuliko hatua nyingine za mchakato huo zilizobaki. Hapana shaka kwamba Rasimu hiyo ndiyo dira inayoonyesha njia, mbali na ukweli kwamba wajumbe wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba waliotayarisha dira hiyo ni watu waadilifu, wengi wao wakiwa na rekodi ya utumishi uliotukuka, mbali na majina yao kuonekana katika jamii kama taasisi.
Hatujawahi kutilia shaka uadilifu na uzalendo wa Jaji Joseph Warioba, Jaji Augustino Ramadhan, Salim Ahmed Salim na wajumbe wengine wa Tume hiyo waliotayarisha Rasimu hiyo. Hata hivyo, yafaa ieleweke kwamba tunaposema hivyo hatuna maana kwamba Rasimu hiyo isikosolewe na kwamba ni sahihi na kamili kwa asilimia mia moja. Lazima kuna mapungufu ya hapa na pale na tayari baadhi ya mapungufu hayo yameanza kuainishwa na kujadiliwa na wananchi.
Katika mijadala ya Rasimu hiyo inayoendelea nchini kote, jambo kubwa linalojitokeza ni hofu kubwa inayotokana na baadhi ya wanasiasa kutojua mustakabali wao baada ya Katiba Mpya kuzinduliwa, hivyo wameelekeza nguvu zao katika kupinga vifungu katika Rasimu ya Katiba Mpya vinavyogusa masilahi yao, vikiwamo kuanzishwa kwa serikali tatu, mgombea binafsi hadi ngazi ya urais, kushinda uchaguzi kwa zaidi ya asilimia 50, kufutwa kwa Viti Maalumu na kadhalika.
Wanasiasa wengi katika kundi hilo linalopinga Rasimu hiyo hata kabla ya kuisoma kwa undani ni wale walioasisi Katiba iliyopo na nyingine zilizopita. Hawataki mabadiliko yatakayogusa nafsi zao au kukubali ukweli kwamba Katiba Mpya lazima iweke mfumo mpya utakaoleta mabadiliko ambayo pia utekelezaji wake utasimamiwa na taasisi mpya. Iwapo tutapiga vita hofu na ubinafsi Watanzania tutapata Katiba itakayotuongoza kwa miaka mingi ijayo.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni