Kwa ufupi
- Walitamani angekuwa kwenye gari la wazi ili waweze kumwona, lakini walishindwa kufanya hivyo kutokana na magari yaliyokuwa yamembeba kupita kwa kasi zaidi
Dar es Salaam. Maelfu ya wakazi wa D Dar es
Salaam, walijitokeza kwa wingi jana kumlaki Rais wa Marekani, Barack
Obama aliyewasili nchini kwa ziara ya siku mbili inayohitimishwa leo
huku wakilalamikia kutomwona.
Kwenye Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius
Nyerere, msafara wake ulipitia Barabara za Nyerere, Nkrumah, Samora,
Magogoni hadi Ikulu.
Ukonga Majumba Sita
Wakazi wa maeneo ya Gongo la Mboto, Ukonga,
Kitunda, na Tabata walifurika eneo la Majumba Sita kwa ajili ya kumwona,
lakini hali ilikuwa tofauti.
Magari yalizuiwa kuanzia Njia panda ya Segerea na
hayakuruhusiwa kusogea karibu na barabara inayotoka uwanja wa ndege.
“Mimi nimefika hapa kwa ajili ya kumwona, sikumwona jamani yaani
nimepigwa na jua bure,” alilalamika dada mmoja akiwa na wenzake huku
ameshikilia kandambili mkononi.
Naye Mkazi wa Tabata Mawezi, aliyejitambulisha kwa
jina la Jana Kamanzi alilalamikia mwendo kasi wa magari hayo na
kushindwa kumuona kiongozi huyo.
Kipawa/Jeti Lumo
Maeneo hayo walijitokeza watu wengi huku wengine wakiwa na mikeka ya kukalia tayari kumlaki kiongozi huyo.
Gazeti hili lilishuhudia umati huo kwa wakazi kutoka maeneo ya Jeti, Kipawa, Karakata waliofika kumlaki Rais huyo wa Marekani.
Baadhi ya mama lishe walitumia nafasi hiyo kuuza
chakula kwenye ndoo za plastiki kwa kificho, huku wafanyabiashara ya
maji na wao wakitumia nafasi hiyo kupandisha bei ya maji huku wakiuza
kwa kificho.
Vingunguti
Katika maeneo ya Vingunguti, umati ulifurika pande
zote mbili za barabara kwa wakazi wa Vingunguti na Kijiwe Samli
wakiwamo wafanyakazi ambao ofisi zao ziko karibu na Barabara ya Nyerere.
Maafisa Usalama waliokuwa wamejichanganya na wananchi,
walimkamata mama mmoja aliyekuwa akijaribu kuvuka barabara kabla ya
msafara wa Rais Jakaya Kikwete kupita wakati akienda kumpokea mwenyeji
wake, Rais Obama.
Kwa kuwa kila mmoja alikuwa akimwangalia, wakati
anajiandaa kukatisha barabara na msafara unakuja, walimkimbilia na
kumdaka na kisha kuondoka naye. Hata hivyo haikuweza kufahamika mama
huyo alikuwa na lengo gani.
Magari yalizuiwa kutoka Vingunguti na hata yale yanayotokea Kijiwe Samli, barabara zake zinaingia
Barabara ya Nyerere.
Barabara ya Nyerere.
Baadhi ya wakazi hao walisikika wakilalamika kutomwona Rais Obama kwani walitarajia angekuwa kwenye gari la wazi waweze kumuona.
Wakazi wengine walilalamikia hali hiyo, mbali na
kutotarajia umati na kushindwa kumwona, walijua kuwa atakuwa kwenye gari
la wazi ambalo wangeweza kumuona.
Makutano ya Mandela na Nyerere (Tazara)
Wananchi walivamia msafara wa Rais Obama katika eneo la Tazara na kusababisha msafara huo kupunguza mwendo.
Kitendo hicho kilitokea wakati Rais huyo na
msafara wake uliokuwa na zaidi ya magari 15 ukitoka Uwanja wa Ndege wa
Kimataifa wa Julius Nyerere ukienda Ikulu.
Msafara wa Rais Obama haukuwa katika mwendo wa
kasi na ulipokaribia makutano ya barabara hizo maeneo ya Tazara,
wananchi walivuka kutoka upande wa pili kushuhudia msafara huo kwa
ukaribu zaidi.
Kitendo hicho cha wananchi kuvamia msafara huo kwa
ghafla kiliwachanganya askari polisi waliokuwa wachache, hivyo
kusababisha msafara huo kupunguza mwendo.
Awali askari Polisi waliimarisha ulinzi na
kuwazuia watu kuvuka barabara kutokana na magari kupita kwa kasi eneo
hilo na wananchi walitiii amari hiyo.
Njia Panda ya Veta
Katika maeneo yanayounganisha Barabara ya Nyerere na Chang’ombe,
polisi walifanya kazi ya ziada kuzuia mamia ya watu waliofika kumlaki .
Mamia ya watu hao kutoka Temeke, Chang’ombe,
Tandika, Ilala walifurika katika eneo hilo kutaka kumuona kiongozi huyo,
lakini hata hivyo wengi walisikika pia wakilalamikia kutomwona.
Kamata
Wakazi wa maeneo ya Kariakoo, Gerezani, Ilala walifurika kuanzia njia panda ya Shauri Moyo huku wakiwa katika hali ya utulivu.
Polisi walikuwa na kazi ya kuzuia wakazi hao waliokuwa wanavuka barabara kabla na baada ya misafara kupita.
Mtaa wa Nkrumah
Hali ilikuwa tete katika Mtaa wa Nkrumah ambako
ulipita msafara wa Obama wakati akitokea Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa
Julius Nyerere.Msafara wa Rais Obama ulipita katika Mtaa wa Nkrumah kwa
ajili ya kuingia Mtaa wa Samora kuelekea Ikulu.
Maduka na ofisi kadhaa zilizoko maeneo ya Nkrumah,
Kidongo Chekundu na Mnazi Mmoja yalifungwa kutokana na watu kuwa na
hamu ya kuuona msafara wa Obama. Watu walikuwa wengi pande zote za
barabara na msafara wa Obama ulipofika kwenye eneo hilo, watu
walimshangilia kwa nguvu.
Hata hivyo, watu wengi walisikitishwa na kitendo
cha kutomwona Obama kwani wengi walitegemea kuwa watapanda gari lenye
vioo ambavyo wangeweza kumwona kwa urahisi wakati akipita katika eneo
hilo la Nkrumah.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni