Aliyekuwa makamu wa Rais wa Sudan Kusini Riek Machar amesema
atagombea urais katika uchaguzi mkuu mwaka 2015 dhidi ya Rais
Salva Kiir aliyemfuta kazi mapema wiki hii. Akizungumza katika
mkutano wa hadhara jana kwa mara ya kwanza tangu kufutwa kazi,
Machar alisema atawania kupitia chama tawala na kumpinga Kiir.
Machar ameongeza kuwa ili taifa hilo liungane haliwezi kuvumilia
utawala wa kiimla.Rais Kiir alivunjilia mbali baraza la mawaziri na
kumfuta kazi makamu wake siku ya Jumanne kufuatia ripoti kuwa
kuna mzozo wa uongozi ndani ya chama tawala hasa kati ya Kiir na
Machar.Kiir amepunguza idadi ya mawaziri kutoka 29 hadi 18. Pia
alimsimamisha kazi katibu mkuu wa chama cha SPLM Pagan Amum
akisubiri kukamilika kwa uchunguzi wa madai ya kudharau mamlaka
na kuleta mgawanyiko ndani ya chama tawala. Machar amesema Kiir
ana haki kikatiba kumfuta kazi makamu wa rais na kulivunja baraza la
mawaziri lakini amemshutumu kwa kile alichokiita pengo la uongozi
lilioachwa baada ya hatua hiyo kwa kushindwa kujaza nafasi zao
mara moja.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni