Jumanne, 2 Julai 2013

Marekani, jasusi mkubwa duniani


Inaonekana kwamba kati ya majanga ya kidiplomasia yaliyoikumba Marekani katika miongo ya hivi karibuni, hayajalizidi janga la hivi sasa ambalo limeikumba nchi hiyo baada ya kijana mmoja wa miaka 30 anayejulikana kwa jina la Edward Snowden kufichua ujasusi mkubwa unaofanywa na Marekani kupitia programu ya kijasusi ya PRISM. Karibu wiki tatu zilizopita, ajenti huyo wa zamani wa Shirika la Kijasusi la Marekani CIA alifichua jinsi Marekani inavyofanya ujasusi mkubwa sana katika kona zote za dunia kwa kutumia programu ya PRISM. Tab'an ujasusi wa Marekani kwa mataifa mengine duniani una historia ndefu sana na kwa karne nyingi nchi hiyo imekuwa ikililalamikiwa na mataifa mengine ulimwenguni kwa kufanya ujasusi dhidi ya mataifa hayo na kutoheshimu haki yao ya kujitawala.  Pamoja na hayo lakini, ujasusi uliofichuliwa hivi sasa na kijana huyo wa Kimarekani umeushitua kupindukia ulimwengu na unaonekana kama vile ni filamu za hadithi za kubuni na za ki-James Bond. Swali la kujiuliza hapa ni kuwa, kwa nini ufichuaji huu uliofanywa na Edward Snowden umeushitua vibaya ulimwengu? Kwanza kabisa ni kwamba PRISM ni programu pana sana ya kijasusi ambayo inakusanya na kusambaza taarifa nyingi za kijasusi kwa mkupuo mmoja. Kwa maneno mengine ni kuwa, programu hiyo inakusanya taarifa za mazungumzo ya simu ya watu wote kwenye kona zote za dunia na kupeleka moja kwa moja taarifa hizo kwa Shirika la Usalama wa Taifa la Marekani, NSA. Tab'an kitendo cha shirika la NSA cha kusikiliza mazungumzo ya simu za watu duniani ni jambo ambalo limekuwa likifanyika kwa miaka mingi, lakini kuwafanyia ujasusi watu wanaotumia Intaneti ni jambo jipya lililofichuliwa na Edward Snowden. Kwa mujibu wa nyaraka hizo, taarifa zote za watumiaji wa Intaneti zikiwemo barua-pepe, chat, mafaili ya sauti, picha na mengineyo yanayopakuliwa kutoka katika Intaneti yanakusanywa na programu hiyo na kutumwa kwa Shirika la Usalama wa Taifa la Marekani NSA. Jambo hilo lina maana ya kwamba, Marekani imedhibiti miamala yote ya wanadamu duniani kwa ghafla moja. Nukta nyingine katika nyaraka zilizofichuliwa na mfanyakazi huyo wa zamani wa shirika la NSA zinaonyesha kuwa, ujasusi huo wa Marekani haufanywi dhidi ya watuhumiwa wa ujasusi na wakazi wa nchi zenye ugomvi na Marekani tu, bali hata marafiki na waitifaki wa karibu kabisa wa Marekani hawakusalimika na programu hiyo ya kijasusi ya PRISM. Hii ina maana ya kuwa, Marekani inawaangalia watu wote kwa jicho la uadui na shaka. Yaani wananchi wote wa Uingereza, Ujerumani na Ufaransa ni hatari sana kwa Wamarekani kwa kiwango kile kile cha hatari ya wananchi wa Afghanistan, Pakistan na Yemen kwa nchi hiyo. Sifa nyingine ya programu hiyo ya kijasusi ya PRISM haikuishia tu kwa wananchi wa kawaida bali inawafanyia ujasusi pia viongozi wa ngazi za juu wa nchi za duniani zikiwemo ofisi za Umoja wa Ulaya huko Washington na New York, bali hata katika makao makuu ya umoja huo mjini Brussels, Ubelgiji. Kukusanya taarifa za siri za viongozi wa nchi na jumuiya za kimataifa kunaipa uwezo serikali ya Washington kuwalazimisha viongozi hao kutii amri za Marekani wakati wowote wanapotaka, vinginevyo viongozi hao wakubali kufedheheshwa na Marekani kupitia kufichuliwa siri zao. Lililo muhimu hapa ni kuwa, Wamarekani hawakukanusha mambo yaliyofichuliwa na Edward Snowden, bali wamekiri kuwepo programu hiyo na wametoa amri ya kutafutwa kimataifa aliyefichua siri hizo. Hii ina maana kwamba Wamarekani hawana nia ya kuachana na ujasusi huo licha ya kufichuliwa kashfa hiyo. Hatari zaidi ni kuwa, Edward Snowden ana nyaraka nyingine za siri ambazo kama zitatangazwa, basi serikali ya Marekani itakumbwa na kashfa nyingine kubwa ya kijasusi.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni