Jumanne, 16 Julai 2013

Vyombo vya habari vyafuatilia habari kuhusu kupungua kwa ukuaji wa uchumi wa China






Takwimu zilizotolewa jana na Idara ya Takwimu ya China zinaonesha kuwa katika nusu ya kwanza ya mwaka huu, pato la taifa GDP lilikuwa ni Yuan trilioni 24.8009, ambalo liliongezeka kwa asilimia 7.6 kuliko mwaka jana wakati kama huu. Takwimu hizo zimefuatiliwa na vyombo vya habari vya nchi mbalimbali. Fadhili Mpunji ana maelezo zaidi.
Shirika la Utangazaji la Uingereza BBC limesema katika robo ya pili ya mwaka huu, ukuaji wa uchumi wa China ulipungua kuliko ule wa robo ya kwanza, lakini serikali ya China ilitimiza lengo la kasi ya ongezeko la ukuaji, na inatarajia ongezeko la uchumi kutegemea matumizi katika soko la ndani badala ya kuuza bidhaa kwa nje.
Gazeti la Financial Times la Uingereza linaona kuwa viongozi wa China wa awamu mpya wanazingatia zaidi mageuzi ya kina na wala si hatua za kuchochea ongezeko la uchumi katika muda mfupi. Kutokana na kupungua kwa kasi ya ukuaji wa uchumi, labda China haitaweza kutimiza lengo la asilimia 7.5 ya ongezeko la uchumi kwa mwaka huu. Kama hali hii ikitokea, itakuwa ni mara ya kwanza kwa ukuaji wa uchumi wa China kutotimiza lengo lililowekwa baada ya bara la Asia kukumbwa na msukosuko wa fedha mwaka 1998. Hata hivyo, kuna dalili zinazoonesha kuwa hali ya kudidimia kwa uchumi wa China imedhibitiwa, shughuli za huduma na viwanda zimeongezeka kwa kasi, hali ambayo inaweza kuziba hasara zinazotokana na kupungua kwa uuzaji wa bidhaa kwa nje.
Gazeti la The WallStreet Journal la Marekani limesema mwaka huu, China itachangia asilimia 13 ya shughuli za kiuchumi duniani, kupungua kwa ukuaji wa uchumi wa China kutakuwa na athari kubwa kwa uchumi wa dunia. Gazeti hilo limesema kutokana na kupungua kwa ukuaji wa uchumi, makampuni ya China yanayozalisha bidhaa muhimu yabane matumizi na kupunguza kuagiza rasilimali kutoka nje, na hali hii itaziathiri nchi za Indonesia na Australia zinazouza nje rasilimali kwa wingi zaidi, na kufanya bei za nishati na rasilimali katika sehemu nyingine duniani kushuka na kupunguza kiwango cha mfumuko wa bei, kwa hiyo nchi mbalimbali zitaweza kuchukua hatua za kuchochea ukuaji wa uchumi wao dhaifu.
Wanahabari na wasomi wengi nchini Marekani wanaona kuwa kupungua kwa ongezeko la uchumi wa China ni changamoto inayoyakabili mageuzi ya kimuundo yaliyopendekezwa na viongozi wa China. Wachambuzi wanaona kuwa uchumi wa China uko katika kipindi cha mwanzo cha mabadiliko ya njia za kujiendeleza, ambapo ukuaji wa uchumi unategemea zaidi uwekezaji, na itachukua muda wa miaka kadhaa kutimiza lengo la kuwa uchumi unategemea zaidi matumizi ya soko la ndani.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni