Alhamisi, 15 Agosti 2013

Jeshi la Misri limeua watu 2,200


  Miili ya baadhi ya watu waliouawa Cairo, Agosti 14 2013
 
Harakati ya Ikhwanul Muslimin nchini Misri imesema jeshi la nchi hiyo leo Jumatano  limewaua watu 2,200 baada ya kutumia nguvu kuvunja mkusanyiko wa wafuasi wa rais aliyepinduliwa, Mohammad Mursi katika eneo la Rabaa al-Adawiya katika mji mkuu wa nchi hiyo, Cairo.  Aidha Ikhwanul Muslimin kupitia tovuti yake ya ikhwanonline imesema zaidi ya watu 10,000 wamejeruhiwa katika vurugu hizo za leo. Baadhi ya duru za  Ikwanul Muslimin zimesema idadi ya waliouawa ni zaidi ya 2,600. Wizara ya Afya Misri imedai kuwa ni watu 149 waliouawa katika machafuko ya leo. Huku hayo yakijiri makamu wa Rais wa Misri Mohammad el Baradei amejiuzulu kulalamikia mauaji hayo ya umati yaliyotekelezwa na jeshi. Katika upande mwingine rais Adli Mansour wa serikali ya mpito Misri ametangaza hali ya hatari nchini humo kwa muda wa mwezi moja ujao.
Katika kulalamikia jinai za jeshi, wananchi waliokuwa na hasira wanaendeleza maandamano katika mikoa na miji mbalimbali ya nchi hiyo kama vile Asyut ,Ismailia na Alexandria. Baadhi ya ripoti zinasema watu 15 wameuawa katika machafuko mabaya yaliyoibuka  Ismailia na wengine 10 wamepoteza maisha huko Alexandria. Waandamanaji waliokuwa na hasira wamelaani hatua ya vikosi vya usalama kuwafyatulia risasi waandamanaji mjini Cairo.
Hii ni katika hali ambayo Sheikh Mkuu wa Chuo Kikuu cha Al-Azhar nchini humo, Ahmad al-Tayyib amewataka Wamisri wote kwa ujumla kudhibiti nafsi zao sambamba na kutumia akili katika kuamiliana na hali ya mambo.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni