Ijumaa, 23 Agosti 2013

Kambi ya upinzani Guinea yatishia kususia uchaguzi

Viongozi wa vyama vya upinzani nchini Guinea Conakry wametishia kuwa watasusia uchaguzi wa bunge uliopangwa kufanyika tarehe 24 Septemba mwaka huu. Viongozi wa vyama hivyo wanamtuhumu Rais Alpha Conde wa Guinea kuwa amepanga kufanya udanyanyifu katika uchaguzi huo na kuwapa ushindi wagombea wa chama chake.

Kwa mujibu wa katiba ya Guinea Conakry, uchaguzi wa bunge unapaswa kufanyika siku sitini baada ya kuanza kipindi cha rais wa nchi. Hata hivyo uchaguzi wa bunge la nchi hiyo umekuwa ukiakhirishwa tangu mwaka 2011 hadi sasa kwa kisingizio cha kutokuwapo mazingira yanayofaa.
Guinea Conakry imekuwa ikikumbwa na mapinduzi ya mara kwa mara ya kijeshi tangu ilipopata uhuru hadi mwaka 2010. Novemba mwaka 2010 kulifanyika uchaguzi wa kidemokrasia ambao ulimfikisha madarakani Rais Alpha Conde. Wachambuzi wa mambo waliutaja uchaguzi huo kuwa ndio zoezi la kwanza la kukabidhiana madaraka kwa njia ya amani nchini Guinea baada ya rais kuchaguliwa moja kwa moja na wananchi.
Viongozi wa vyama vya upinzani nchini Guinea wanamlaumu Rais Conde kwa kuainisha tarehe ya uchaguzi wa bunge bila ya kushauriana na kambi ya upinzani na wanamtuhumu kwamba ametayarisha mpango wa kuchakachua kura. Vilevile serikali ya Conde inalaumiwa kwa kushambulia na kukandamiza vyombo vya habari vya kambi ya upinzani. Kambi hiyo inasema vyama vya upinzani vimenyimwa uhuru wa kusema na kujieleza ambao ni miongoni mwa nguzo kuu za demokrasia.
Baadhi ya wakosoaji nchini Guinea Conakry wanasema kuwa, hali ya kutoaminiana iliyopo sasa baina ya wananchi na utawala ni matokeo ya ukandamizaji mkubwa unaofanywa na vyombo vya usalama vya dola dhidi ya waandamanaji wa kambi ya upinanzi.
Moja ya masuala yanayozusha mivutano kati ya vyama vya upinzani na serikali ya Guinea ni marekebisho katika vikosi vya usalama na jeshi la nchi hiyo. Satua na ushawishi mkubwa wa jeshi la Guinea katika masuala ya siasa za nchi hiyo umekuwa ukisababisha mapinduzi ya mara kwa mara. Mfano wa wazi wa ukweli huo ni jaribio lililoshindwa la wanajeshi la kutaka kumwondoa madarakani Rais Alpha Conde mwenyewe.
Kampeni za uchaguzi wa bunge nchini Guinea zilianza tarehe 24 Agosti kote nchini humo. Hata hivyo chama tawala kimejiimarisha zaidi kutokana na kuhodhi vyombo vya mawasiliano ya umma na rasilimali zote za taifa. Suala hili pamoja na vizingiti na sheria zinazobana kampeni za uchaguzi za vyama vya upinzani, vimeilazimisha kambi ya upinzani kutishia kwamba yumkini vikasusia uchaguzi huo.
Weledi wa mambo wanasema uamuzi wa Umoja wa Afrika wa kutuma wasimamizi katika uchaguzi ujao wa bunge nchini Guinea Conakry huwenda ukatuliza wasiwasi wa kambi ya upinzani na kudhamini uwazi na uhuru katika zoezi hilo.
 

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni