Waziri wa Habari wa Syria Omran al- Zoubi amesema kuvamiwa kijeshi nchi yake na Marekani kutachochea machafuko zaidi katika Mashariki ya Kati. Al- Zoubi ameonya kuwa athari mbaya ya kwanza ya kuvamiwa kijeshi Syria itakuwa ni kuwaka moto ambao hautoiunguza nchi hiyo pekee bali utaenea katika eneo lote la Mashariki ya Kati na kuongeza kwamba kuishambulia kijeshi Syria haitokuwa kazi nyepesi. Waziri wa Habari wa Syria ametoa tahadhari hiyo katika hali ambayo katika kipindi cha mwaka mmoja sasa machafuko ya Syria tayari yameshaenea katika baadhi ya maeneo ya Mashariki ya Kati. Onyo hilo limetolewa kufuatia matamshi ya Waziri wa Ulinzi wa Marekani Chuck Hagel kwamba Pentagon imejitayarisha kuchukua chaguo lolote la dharura dhidi ya Syria na ipo tayari kutumia nguvu iwapo Rais Barack Obama ataidhinisha suala hilo. Tangu mwaka 2011 Syria imekumbwa na machafuko makubwa ya umwagaji damu yaliyotokana na vita vilivyoanzishwa na makundi ya kigaidi yanayoungwa mkono na madola ya Magharibi pamoja na waitifaki wao wa eneo zikiwemo Qatar, Saudi Arabia na Uturuki. Kwa mujibu wa Umoja wa Mataifa hadi sasa zaidi ya watu laki moja wameuawa na wengine milioni saba na laki nane wamelazimika kuyahama makazi yao kutokana na machafuko hayo…/
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni