
Na Hamida Shariff, Mwananch
Theophil alisema mkutano huo uliyapigia kura
majina matatu yakiwamo ya wabunge wengine wawili vijana; John Mnyika na
Zitto Kabwe na kwamba Makamba alipitishwa kuwa chaguo lao baada ya
kupata kura 70 kati ya 105 zilizopigwa.
Waazimia kuunda timu ambayo itamshawishi January Makamba kuwania urais katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015.
Morogoro. Viongozi wa Vyuo Vikuu
21 nchini wameazimia kwa kauli moja kuunda timu ndogo itakayokwenda
kumshawishi Mbunge wa Bumbuli na Naibu Waziri wa Mawasiliano, Sayansi na
Teknolojia, Januari Makamba kuwania urais katika Uchaguzi Mkuu wa 2015.
Rais wa Serikali ya Wanafunzi wa Chuo Kikuu
Mzumbe tawi la Mbeya, Theonest Theophil alisema hilo ni moja ya
maazimio yaliyofikiwa katika mkutano wa siku mbili na kuwashirikisha
marais, makamu wa rais, mawaziri wakuu na maspika wa vyuo 21 nchini.
Theophil alisema mkutano huo uliyapigia kura
majina matatu yakiwamo ya wabunge wengine wawili vijana; John Mnyika na
Zitto Kabwe na kwamba Makamba alipitishwa kuwa chaguo lao baada ya
kupata kura 70 kati ya 105 zilizopigwa. Alisema Zitto alipata kura 20 na
Mnyika kura tisa, huku kura tisa zikiharibika.
Alisema viongozi hao wamepanga kutembea nchi nzima
na kuwashawishi Watanzania kumuunga mkono Makamba endapo ataafiki
kuwania nafasi hiyo ya urais, huku wakidai kwamba wamechoshwa na
viongozi wenye visasi na uadui ambao wamekuwa wakitumia muda mwingi
kulumbana na kupambana badala ya kuwatumikia wananchi.
Theophil alisema mkutano huo ulilenga kujadili
mustakabali wa nchi katika masuala ya ubora wa elimu na vihatarishi vya
amani ambavyo vinatokana na chuki za kidini, siasa na visasi. Pia
walijadili tatizo la ajira kwa vijana, ukuaji wa uchumi na mchakato wa
Katiba Mpya ambao alisema hivi sasa ni kama umetekwa na ushabiki wa
kisiasa.
Theophili alisema walibaini kwamba ili kukabiliana
na changamoto zilizopo lazima nchi iwe na uongozi thabiti, hivyo
walimchagua Makamba kama mmoja wa viongozi wenye sifa za kushika wadhifa
wa urais kwa kuzingatia sifa alizonazo.
Alizitaja baadhi kuwa ni kuonyesha uwezo na
ujasiri katika nafasi za uongozi alizowahi kushika na uadilifu, kwani
hajawahi kuhusishwa na vitendo vya rushwa na ufisadi katika uongozi
wake.
Kwa upande wake, Said Ngolola kutoka Chuo Kikuu
cha Dar es Salaam alisema tatizo la mikopo kwa wanafunzi wa vyuo vikuu
limekuwa likiathiri mfumo wa elimu ya juu nchini, kutokana na kushindwa
kwa waliopewa dhamana ya kusimamia suala hilo hali ambayo imekuwa
ikileta migogoro isiyoisha..
Mkutano wa viongozi hao uliandaliwa na kufadhiliwa
na asasi isiyokuwa ya kiserikali ya FPID inayojihusisha na mapambano
dhidi ya maradhi, ujinga na umaskini yenye makao yake makuu Dar es
Salaam.
Katibu wa asasi hiyo, Frances Ndunguru alisema
asasi hiyo haina uhusiano wowote na wanasiasa, bali lengo ni kuwezesha
makundi mbalimbali ya kijamii kukutana na kujadili masuala yenye
masilahi kwa nchi.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni