Jumatatu, 23 Septemba 2013

Kenya yasema jitihada ya kuwaokoa mateka kumalizika hivi karibuni


Jeshi la Kenya limethibitisha mapema leo kuwa jitihada ya kuwaokoa watu waliotekwa nyara katika shambulizi la kigaidi lililotokea jumamosi ndani ya jengo la maduka la Westgate nchini humo inakaribia kumalizika, huku idadi ya vifo ikiongezeka na kufikia 69.
Msemaji wa jeshi la ulinzi la Kenya Kanali Cyrus Oguna amesema, jeshi hilo limefanikiwa kuwaokoa watu wengi, na kusema ni watu 10 tu bado wako ndani ya jengo hilo. Amesema askari wanne wa jeshi hilo walikimbizwa hospitali baada ya kujeruhiwa walipokuwa wakijaribu kuwaokoa watu wanaoshikiliwa ndani ya jengo hilo. Milio ya risasi imesikika mapema leo ndani ya eneo hilo ambako kundi la magaidi bado linawashikilia mateka wachache.
Kati ya watu waliouawa katika shambulizi hilo, ni raia wawili wa Ufaransa, raia wawili wa Canada, raia watatu kutoka Uingereza, mmoja kutoka China na mmoja anatokea Ghana.
Wakati huohuo, kufuatia shambulizi la kigaidi lililotokea mjini Nairobi, viongozi wa kimataifa wamejitokeza kwa wingi kuiunga mkono Kenya. Rais Barack Obama wa Marekani, na mawaziri wakuu kutoka Uingereza, Canada, Israel, na India, pamoja na viongozi wa kikanda kutoka nchi za Rwanda, Uganda, Tanzania, Burundi, Sudan Kusini, waziri mkuu wa Ethiopia, na nchi nyingine za Afrika wamelaani vikali shambulizi hilo, na wamesema wako tayari kutoa msaada wowote unaotakiwa na serikali ya Kenya.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni