Ijumaa, 20 Septemba 2013

Maandamano ya katiba mpya, yazuiwa Tanzania


Jeshi la Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam Tanzania, limeviruhusu vyama vya Chadema, CUF na NCCR Mageuzi kufanya mkutano wao wa hadhara kwenye viwanja vya Jangwani hapo kesho Jumamosi, Septemba 21, lakini limewazuia wafuasi wa vyama hivyo kufanya maandamano. Awali vyama hivyo vilikuwa vimeitisha maandamano hayo ambayo yangewashirikisha viongozi, wanachama na wafuasi wa vyama hivyo kwa kuanzia eneo la Tazara hadi viwanja vya Jangwani jijini Dar es Salaam, lakini Kamanda wa Polisi Kanda ya Dar es salaam, Kamishna Suleiman Kova amekataa suala la kufanyika maandamano hayo kwa madai kuwa, yanaweza kuzusha machafuko. Lengo la kuitishwa maandamano na mkutano huo ni kupinga mchakato mzima wa Katiba mpya na kumshinikiza Rais Jakaya Mrisho Kikwete asiusaini Muswada wa Marekebisho ya Sheria ya Mabadiliko ya Katiba kwa kuwa umehodhiwa na Chama Cha Mapindizi CCM. Kwa upande mwingine Kova amesema kuwa, Jeshi la Polisi limepata taarifa za kijasusi kuwa, vyama hivyo vimeandaa uhamasishaji mkubwa kwa watakaotumia pikipiki na watembea kwa miguu.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni