Jumapili, 1 Septemba 2013

Obama abadilisha msimamo kuhusiana na shambulio la kijeshi dhidi ya Syria

Obama abadilisha msimamo kuhusiana na shambulio la kijeshi dhidi ya Syria
Rais Barack Obama wa Marekani ambaye kwa muda wa wiki sasa amekuwa akipiga ngoma ya vita dhidi ya Syria, anaonekana kulegeza msimamo kuhusiana na kadhia hiyo. Licha ya Obama kusema kwamba, shambulio la silaha za kemikali nchini Syria ni tishio kwa Marekani na washirika wake, lakini pamoja na hayo amesema kwamba, uingiliaji wa kijeshi wa Washington nchini Syria unapaswa kupata idhini na ridhaa ya Kongresi ya nchi hiyo. Obama amesema kama ninavyomnukuu, "licha ya kuwa mimi ni Rais wa Marekani na nina uwezo wa kutoa idhini ya kufanywa shambulio la kijeshi, lakini naitaka Kongresi ichukue uamuzi kuhusiana na hili" mwisho wa kunukuu. Rais wa Marekani ametangaza kwamba, nchi yake ni lazima iingilie kijeshi suala la Syria. Obama ameashiria kwamba, shambulio la kijeshi dhidi ya Syria linaweza kufanywa kesho, wiki ijayo au mwezi ujao na kuongeza kwamba, nchi yake ni Marekani na kwamba, haiko tayari kufumbia macho kile kinachojiri nchini Syria. Obama amebainisha kwamba, amefanya mazungumzo na viongozi wa Demokrat na Repulican na kwamba, viongozi hao wametangaza kukubaliana na shambulio la kijeshi la Washington dhidi ya Syria.
Inaonekana kuwa, hatua ya Rais Obama ya kulegeza msimamo ina mfungamano na matukio ya hivi karibuni kieneo na kimataifa. Ukweli wa mambo ni kwamba, Obama amejikuta yuko peke yake baada ya kushindwa kupata idhini ya jamii ya kimataifa kupitia Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kwa ajili ya kuishambulia kijeshi Syria. Hadi sasa rasimu tatu za maazimio yaliyopendekezwa na Wamagharibi na waitifaki wao kwa ajili ya kuishinikiza Syria zimegonga mwamba katika Baraza la Usalama baada ya kupigiwa kura ya veto. Pigo la hivi karibuni kabisa la Wamagharibi katika uwanja huo ni kukwama pendekezo la Uingereza lililowasilishwa katika Baraza la Usalama la kutaka idhini ya kuishambulia kijeshi Syria. Baada ya Uingereza kujiweka pembeni, Marekani imebakia na mshirika mmoja tu yaani Ufaransa katika propanga za kupigia upatu shambulio la kijeshi dhidi ya Syria. Hata hivyo Ufaransa nayo mambo yake hayako shwari sana hasa kutokana na kuwa, kuna wimbi kubwa la upinzani nchini humo ambalo halitaki kuiona Paris ikishirikiana na Washington katika shambulio la kijeshi dhidi ya Syria. Vyombo vya habari nchini Ufaransa vinamtaja Rais Francois Hollande wa nchi hiyo kwamba, ndiye swahiba na mshirika pekee wa Marekani  barani Ulaya katika kupiga ngoma ya vita dhidi ya Syria. Weledi wa mambo wanaamini kwamba, matukio haya ndio yaliyomfanya Rais Obama afikirie mara mbili mbili hasa baada ya kujiona  kwamba, kwa namna fulani amebakia peke yake katika kadhia ya kutaka kuishambulia kijeshi Syria. Pamoja na hayo, Obama hataki kuubeba peke yake mzigo mzito wa kuishambulia kijeshi Syria. Mbali na kuachwa mkono na washirika wake katika kuishambulia kijeshi Syria, Obama anakabiliwa pia  na upinzani mkali wa fikra za waliowengi ndani ya Marekani. Kwani kwa mujibu wa uchunguzi wa maoni zaidi ya asilimia 60 ya Wamarekani wanapinga nchi yao kuishambulia kijeshi Syria. Wachambuzi wa mambo wanaamini kwamba, hatua ya Obama ya kuacha kutumia mamlaka aliyonayo kikatiba ya kutoa idhini ya kushambuliwa kijeshi Syria na badala yake kutaka Kongresi ya nchi hiyo ichukue uamuzi wa hilo, ni hila na ujanja wa kisiasa ambao lengo lake ni kutaka kupata himaya ya Kongresi kuhusiana na hilo hasa kwa kutilia maanani kwamba, Kongresi ya Marekani itaunga mkono kushambuliwa kijeshi Syria.
 

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni