Jumatano, 20 Novemba 2013


Mashambulizi ya mabomu yatikisa mji mkuu wa Iraq, Baghdad

Mashambulizi ya mabomu yanayotekelezwa nchini Iraq
REUTERS/Wissm al-Okili

Na Flora Martin Mwano
Mashambulizi ya mabomu yaliyowalenga waumini wa Kishia nchini Iraq yamesababisha vifo vya watu zaidi ya 30 na kujeruhi wengine zaidi ya 70. Kwa mujibu wa ripoti za idara ya usalama toka nchini humo milipuko nane imesikika katika maeneo mbalimbali ya mji mkuu wa nchi hiyo, Baghdad.

Mlipuko mwingine umetokea jirani na eneo ambalo Washia walikusanyika kuadhimisha kumbukumbu ya kifo cha kiongozi wao wa kiislamu, Imam Hussein.
Inahofiwa kuwa huenda idadi ya vifo itaongezeka zaidi kutokana na mashambulizi haya kufanyika siku ambayo ilitangazwa na serikali ya nchi hiyo kuwa ya mapumziko.
Hakuna kundi lililokiri kuhusika na shambulizi hilo, ingawa wanamgambo wa Kisunni wenye uhusiano na mtandao wa kigaidi duniani wa Al-Qaeda wananyooshewa kidole kutokana na kuwa na kawaida ya kufanya mashambulizi dhidi ya Washia.
Katika tukio jingine, Polisi nchini humo wameripoti kuwa mlinzi mkuu wa Rais wa nchi hiyo ameuawa katika mji wa Kaskazini wa Sulaimaniyah. Inaelezwa kuwa wavamizi walifika nyumbani kwa mlinzi huyo, Sarwat Rashid na kumpiga risasi mara tatu kichwani mbele ya mkewe.
Waziri Mkuu Nuri al-Maliki ametoa wito kwa serikali ya Washington kusaidia katika mfumo wa kijasusi na mfumo wa upatikanaji wa silaha mpya ili kukomesha mashambulizi hayo ambayo baadhi ya wanadiplomasia wanasema yanachochewa na mzozo wa nchi jirani ya Syria.
Hata hivyo wakosoaji wanasema serikali ya Iraq haijafanya jitihada za kutosha kutatua kiini cha mzozo huo baina ya waumini wa Kishia na Wasunni.
Bado hofu ya usalama ni kubwa hususani kuelekea uchaguzi mkuu wa nchi hiyo unaotarajiwa kufanyika tarehe 30 Aprili mwaka ujao.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni