Jumatano, 20 Novemba 2013


Rage ‘stop’, Kibadeni ‘out’


Ismail Aden RAGE
Sasa hii ni ukiukwaji wa katiba, hatuna imani naye na hata kama angekuwepo tungemweleza wazi kitendo chake hatukiafiki, tumemsimamisha mpaka Desemba mosi
Dar es Salaam. Wakati Kamati ya utendaji ya Simba ikimsimamisha Mwenyekiti wake, Ismail Aden Rage, imewafungashia virago makocha wake, Abdallah Kibadeni ‘King’ na msaidizi wake, Jamhuri Kiwehlo ‘Julio’ kuinoa timu hiyo yenye maskani yake mtaa wa Msimbazi.
Akizungumza Makao Makuu ya klabu hiyo jana, Kaimu Mwenyekiti wa Simba, Joseph Itang’are ‘Kinesi’ alisema kikao cha Kamati ya Utendaji iliyokaa juzi usiku imefikia uamuzi wa kumsimamisha Mwenyekiti wao kwa kile walichoeleza kutokuwa na imani naye baada ya kushindwa kuitisha mkutano mkuu wa mabadiliko ya katiba.
Hii itakuwa mara ya pili kwa Rage, kusimamishwa ndani ya klabu hiyo, awali alisimamishwa Machi mwaka huu baada ya wanachama kufanya mapinduzi ya kumwondoa akiwa kwenye matibabu nchini India, hata hivyo aliporudi alisema hatambui mapinduzi hayo na kuitisha mkutano alioufanya kwenye Ukumbi wa Bwalo la Polisi Oyestbay huku akiahidi kuitisha mkutano mkuu wa dharura wa mabadiliko Agosti. Hata hivyo, aliahirisha kwa kile alichoeleza ni kupisha mwezi mtukufu wa Ramadhani.
Hata hivyo, jana Kinesi alisema: “Mkutano mkuu wa mwaka ulikuwa ufanyike mwezi huu wa Novemba na ajenda kubwa ni mabadiliko ya katiba, lakini cha kushangaza Rage amewaambia wanachama hakuna mkutano mpaka mwakani na ameondoka yupo nje ya nchi.
“Sasa hii ni ukiukwaji wa katiba, hatuna imani naye na hata kama angekuwepo tungemweleza wazi kitendo chake hatukiafiki, tumemsimamisha mpaka Desemba mosi.
Kinesi alisema Desemba mosi ndiyo utafanyika mkutano mkuu wa wanachama na hatma ya Rage itajulikana kwenye mkutano huo iwapo wanachama wataridhia kumwondoa au wataamua adhabu yake ya kumsimamisha iendelee au arejeshwe kundini kumaliza muda wake ambao unafikia ukingoni Aprili mwakani.
Rage ambaye yuko Juba, Sudan Kusini na anayetarajiwa kurudi nchini Ijumaa, simu yake ilikuwa haipatikani na alitumiwa ujumbe juu ya maono yake kwa hatua hiyo, hakujibu.
Mbali na Rage, pia rungu hilo la Kamati ya utendaji limeangukia benchi ya ufundi la klabu hiyo baada ya kuwafungashia virago  ‘King’ na ‘Julio’ kutokana na mwenendo mbovu wa timu yao iliyomaliza mzunguko wa kwanza wa ligi ikiwa inashika nafasi ya nne ikiwa na pointi 24.
Kinesi alisema nafasi ya Kibadeni itachukuliwa na  aliyekuwa Kocha wa timu ya Gor Mahia, Zdravko Logarusic raia wa Crotia akisaidiwa na Seleman Matola.
Alisema kocha huyo atatua nchini Desemba mosi na timu itaanza rasmi mazoezi Desemba 2 kujiandaa na mzunguko wa pili wa Ligi Kuu Bara.
Akizungumza kwa njia ya simu baada ya uamuzi huo, Kibadeni alisema “Nashukuru kwa hatua hiyo, ni kazi nzito ya kuinoa Simba na kwa vile wamenifukuza timu iko juu wala sijali ingekuwa chini ningesikitika
.Alisema kwa sasa ataishughulikia familia yake na kuangalia afanye nini baadaye, lakini akasema ana mkataba wa miaka miwili Simba.
Julio alipotafutwa kwa njia ya simu alisema hawezi kuzungumza kwa njia hiyo atazungumza ana kwa ana.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni