Kwa ufupi
- Tukirudi kwenye Serikali tatu, wiki iliyopita nilitaja utata wa kwanza katika Muungano ambapo ziliundwa Serikali mbili, yaani ya Muungano na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar.
Wiki iliyopita nilieleza msimamo aliokuwa nao
Baba wa Taifa kuhusu utawala wa Serikali tatu, ambao sasa umependekezwa
katika rasimu ya Katiba.
Pamoja na kuwashukuru wasomaji kwa kutuma ujumbe wa simu, naona kuna watu hawakunielewa.
Katika makala ile nilikuwa natoa historia
ilivyokuwa hadi tukawa na Serikali mbili. Sikumaanisha kwamba kila
alichokiamini Nyerere ndiyo Watanzania wakifuate.
Kwanza ieleweke kwamba, tangu tunapata uhuru
hatukuwahi kuwa na utawala unaowashirikisha wananchi kikamilifu, hata
kama kulikuwa na chaguzi kila baada ya miaka mitano.
Tukirudi kwenye Serikali tatu, wiki iliyopita
nilitaja utata wa kwanza katika Muungano ambapo ziliundwa Serikali
mbili, yaani ya Muungano na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar.
Watu walijiuliza, iko wapi Serikali ya Tanganyika?
Jibu la swali hilo alikuwa nalo Nyerere peke yake na hakutaka watu
waendelee kuuliza. Huu nao ulikuwa utata mwingine.
Kumbuka tangu mwaka 1962 baada ya Mwalimu Nyerere
kuwa Rais wa Jamhuri ya Tanganyika, mabadiliko makubwa yalifanyika ikiwa
ni pamoja na kudhoofisha utendaji wa asasi za kiraia, vyombo vya habari
na ilipofika mwaka 1965, mfumo wa vyama vingi ukafutwa rasmi.
Hapo ndipo Chama cha TANU kikashika hatamu za uongozi. Hakukuwa na uhuru wa kutosha wa kujieleza kwa wananchi.
Nyerere aliwadhibiti hata wale walioonekana kuwa na ushawishi mkubwa wa kisiasa nje ya Serikali yake.
Mfano mzuri ni Mwenyekiti wa Chama cha Chausta,
James Mapalala ambaye aliambulia kutiwa vizuizini. Mwingine ni kada wa
UDP, Lameck Bugohe ambaye pia alishiriki kuanzisha TANU; na wengineo
wengi. Haikushangaza mwaka 1983 kwa aliyekuwa Rais wa Zanzibar, Aboud
Jumbe akapoteza urais wake kwa kuhoji tu Muungano.
Mwalimu aliendelea na msimamo wake huo hata baada ya kung’atuka mwaka 1984, na baadaye alipostaafu uenyekiti wa CCM.
Hata mwaka 1993, Nyerere alipambana na kundi la Wabunge (G55) waliotaka Serikali ya Tanganyika.
Mwalimu aliandika kitabu cha ‘Uongozi wetu na hatima ya
Tanzania’ akimlaumu aliyekuwa Waziri Mkuu, John Malecela na aliyekuwa
Katibu Mkuu wa CCM, marehemu Horace Kolimba akidai kuwa hawakumshauri
vizuri Rais Ali Hassan Mwinyi kuhusu suala hilo.
Hadi anafariki, Nyerere hakuwahi kulegeza msimamo,
na sasa umeshikiliwa na CCM. Ni wakati wa wananchi kuamua wanachokitaka
bila kufungwa na historia, itikadi za vyama wala dini.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni