
Lauden Mwambona
- Hata mwenyekiti wake ambaye ndiye alikuwa Rais, hakuwa na ubavu wa kutamka mambo hadharani kabla ya kufikishwa kwenye Kamati Kuu na hatimaye Halmashauri Kuu.
Tangu CCM ifanye mabadiliko ya viongozi ngazi ya
juu kwa kumteua Abdulrahman Kinana kuwa Katibu Mkuu imeonekana kurudi
kwenye mstari wa utendaji kazi ulioanishwa kwenye nyaraka mbalimbali za
chama.
Nyaraka za CCM ikiwamo Katiba zinatamka wazi
kwamba jukumu lake kubwa ni kushika dola kwa kuunda Serikali.
Zinasisitiza kwamba chama hicho kitaisimamia Serikali yake ili iweze
kutenda haki na kutekeleza vyema ilani ya uchaguzi.
Ni kawaida kwa chama kinachounda Serikali kinatakiwa kuwa na nguvu kuliko Serikali yenyewe.
Ni kwa msingi huo, CCM tangu enzi za Mwalimu
Julius Nyerere ilikuwa ya kwanza katika kujadili mambo muhimu ya
kitaifa na kuweka msimamo imara kabla Serikali haijaanza kufanya lolote.
Hata mwenyekiti wake ambaye ndiye alikuwa Rais,
hakuwa na ubavu wa kutamka mambo hadharani kabla ya kufikishwa kwenye
Kamati Kuu na hatimaye Halmashauri Kuu. Enzi hizo, pamoja na kwamba
walikuwapo viongozi ndani ya CCM au serikalini waliokuwa watoaji wa hoja
za msingi, lakini CCM ilikuwa imara kuwaita mara moja na kuzijadili
hoja zao kabla ya kutoa uamuzi.
Ndiyo maana kwa ngazi za mikoa na wilaya, wakuu wa
mikoa na wilaya waliwajibika kutoa taarifa za kazi kwa Halmashauri ya
CCM ngazi husika.
Viongozi wa CCM ngazi ya wilaya na mikoa walikuwa
na nguvu kuliko wakuu wa mikoa kwani enzi hizo chama kikiazimia
kukuondoa mkuu wa idara kutokana na utendaji mbaya, ilikuwa ni mara moja
unaondoka.
Hata hivyo baada ya kuingia mfumo wa vyama vingi,
CCM ilianza kuyumba kiutendaji na kusababisha watendaji Serikali kushika
hatamu. Tangu mwaka 1995 hadi mwaka jana, CCM ilishakubali Serikali
iongoze chama badala ya yenyewe kuiongoza Serikali.
Vigogo wengi wa Serikali na wabunge walituhumiwa
kwa wizi, rushwa, ufisadi wa kutisha, lakini CCM haikuchukua hatua
zozote badala yake iliafikiana na Serikali yake watuhumiwa wote
waendelee na kazi na ubunge.
Wapo walioshtakiwa mahakamani kuisababishia hasara
Tanzania, lakini badala ya CCM kukaa vikao na kuwasimamisha uanachama ,
iliogopa na kuwafanyia kampeni waendelee kuwa wabunge.
Wapo walioundiwa tume kwa ufisadi, badala ya CCM
kukaa na kuwajadili kwa kina ili kutoa ufafanuzi mbele ya Watanzania,
ilikaa kimya bila kauli yoyote. Mambo yalipozidi kipimo, ndipo mwaka
jana CCM ilipoamua kuwarudisha kwenye uongozi wakongwe wa siasa na kutoa
maelekezo kwamba CCM lazima iisimamie Serikali yake.
Maelekezo hayo yameanza kutekelezwa katika baadhi
ya wilaya ambapo baadhi ya watendaji wameanza kuitwa na kuhojiwa kwa
makosa mbalimbali.
Nao Watendaji wa CCM kitaifa wakiongozwa na Kinana wamekuwa
wakizunguka mikoa mbalimbali kufafanua utendaji wa kazi kati ya CCM na
Serikali yake.
Wanasisiti za kwamba CCM lazima iisimamie Serikali
yake kwa kuwaita kwenye vikao vya ndani watendaji wenye matatizo. Hatua
hiyo inaanza kutekelezwa wakati watendaji wengi wa Serikali
wameshajenga kiburi cha kwamba CCM haina nguvu kuliko Serikali.
Msimamo wa kutaka CCM iisimamie Serikali
hauwatishi wakurugenzi wa halmashauri, watendaji wa idara ngazi za mikoa
bali unawatisha wakuu wa mikoa na wilaya pekee.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni