
Mwakilishi Maalum wa masuala ya elimu
katika Umoja wa Mataifa, Gordon Brown, amewashukuru familia ya Malala na
madaktari ambao wamemwezesha Malala kuishi na kutekeleza yale ambayo
wataliban walitaka asitekeleze. Bwana Brown amesema siku ya leo sio tu
ya kusherehekea kuzaliwa kwa Malala na kunusurika kwake, bali ni siku ya
kusherehekea mtazamo na ndoto yake:
(SAUTI YA BROWN)
"Ndoto yake kwamba hakuna chochote, uwe
upuuzi wa kisiasa, viwe vitisho au risasi za mwuaji, kinachopaswa
kuwazuia haki ya kila mtoto, hususan wasichana na wavulana milioni 57
ambao wamenyimwa elimu, kuweza kwenda tena shuleni. Naamini kwamba leo
tunaona uwezo mpya mkubwa duniani. Ni uwezo wa vijana kubadilisha
ulimwengu na kuwezesha upatikanaji wa elmu kwa wote."
Katika hotuba yake, rais wa Baraza Kuu la
Umoja wa Mataifa, Vuk Jeremic, ameelezea kujivunia kwake kuwa kwenye
jukwaa moja na Malala, na kusifu jinsi ambavyo amekuwa mfano kwa wengi
wanaotetea haki zao za binadamu za kimsingi.
(SAUTI YA VUK)
"Leo tunasherehekea miaka kumi na sita
ya kuzaliwa kwa msichana maalum na jasiri sana: Malala Yousafzai.
Kuvumilia kwake ni ushahidi wa ujasiri wake, na ushahidi ulio hai kuwa
vitendo vya mtu mmoja vinaweza kuleta matumaini kwa mamilioni ya
waathiriwa wa ubaguzi na kutengwa. Elimu hulenga kuwawezesha watoto
kunawiri wakiwa watu wazima, kama wazazi, wachuma riziki, viongozi wa
kijamii na raia wanaowajibika, na kuwapa stadi, tabia na ufahamu
watakaohitaji ili kuchangia jamii zao"
Naye Katibu Mkuu, Ban Ki-Moon, amemshukuru mtoto Malala kwa kuamua kusherehekea siku ya kuzaliwa kwake kwenye Umoja wa Mataifa…
(SAUTI YA BAN)
"Malala alichagua kusherekea siku yake ya kuzaliwa na
ulimwengu. Anatutolea wito tutimize ahadi zetu- tuwekeze katika vijana
na kutanguliza elimu. Kwa kusherehekea siku hii maalum kwenye Umoja wa
Mataifa, Malala anawaambia wengine kama yeye kote duniani kwamba hawapo
peke yao. Serikali na wadau wamepiga hatua muhimu katika elimu. Lakini
bado kuna kazi nyingi ya kufanya. Watoto milioni 57 hawaendi shuleni.
Wengi wao ni wasichana. Nusu yao wanaishi katika nchi zenye mizozo.
Hatuwezi kuacha hali hii iendelee. Hakuna mtoto anayepaswa kufa kwa
sababu ya kwenda shule."
Bwana Ban amesisitiza kwamba hakuna mahali popote ambapo
walimu na watoto wanapaswa kuogopa kwenda shule, akirejelea lengo la
mkakati wake wa kimataifa wa Elimu Kwanza.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni