Marekani imetaka mataifa ya Kiarabu kufanya jitihada za kuiondoa
haraka Misri katika machafuko baada ya vikosi vya usalama kuuwa
idadi kubwa ya wafuasi wa rais aliyeondolewa madarakani,
Mohamed Mursi na kufungua ukurasa mpya wa hatari kati ya jeshi
kukabiliana na wafuasi wa chama cha Udugu wa Kiislamu. Maelfu
ya wafuasi wa chama hicho wamekesha katika msikiti mmoja mjini
Cairo kuamkia leo hii kwa lengo la kutetea haki yao pamoja na
serikali kutishia kuwasambaratisha mara moja. Tukio la umwagikaji
damu la jana, lililotokana na maandamano makubwa,
limelitumbukiza taifa hilo la Kiarabu lenye idadi kubwa ya watu
katika mgogoro mkubwa baada ya kadhia ya kuondolewa
madarakani aliyekuwa rais wa taifa hilo Hosni Mubarak 2011. Katika
vurugu hizo Wizara ya Afya ya Misri inasema watu 65 wameuwawa.
Chama cha Udugu wa Kiislamu kinasema watu 61 wako mahututi
huku vyanzo vingine vikisema zaidi ya watu 70 wameuwawa. Waziri
wa Ulinzi wa Marekani Chuck Hagel amezungumza kwa njia ya simu
na Mkuu wa Majeshi wa Misri, Abdel Fattah al-Sisi, ambae aliongoza
mapinduzi ya Julai 3, ambae pia picha zake zimetapakaa katika
mitaa ya Cairo. Nae Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani Jonh
Kerry amezungumza na viongozi wawili katika jeshi la Misri na
kueleza kusikitishwa kwake na mkasa huo. Katika taarifa yake Kerry
ametoa wito kwa mataifa ya Kiarabu kuchukua hatua za haraka
kulikwamua taifa hilo.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni