
- Kocha wa Yanga, Ernest Brandts, aliiambia Mwanaspoti jana Ijumaa kuwa ushindani baina ya mastraika ni mzuri kwani utachochea wachezaji wake kujituma zaidi na kugombea namba.
KAMA kuna nafasi ngumu kwenye kikosi cha mabingwa wa Tanzania Bara, Yanga msimu ujao, basi ni nafasi ya ushambuliaji.
Yanga mpaka sasa ina washambuliaji sita na uongozi wa klabu hiyo umepanga kuongeza mmoja wa kigeni.
Washambuliaji waliopo ni Jerryson Tegete, Didier
Kavumbagu, Shaban Kondo, Said Bahanuzi, Mrisho Ngassa na Hussein Javu.
Kama haitoshi klabu hiyo bado inaendelea na mazungumzo na Hamis Kiiza
huku pia straika wa Uganda anayedai dau kubwa, Moses Oloya, naye
akitarajiwa kutua klabuni hapo. Lakini Oloya ana uwezekano wa kwenda
Simba pia.
Yanga itaachana na mshambuliaji raia wa Nigeria,
Brendan Ogbu, kwa vilen amekuwa majeruhi hivyo kushindwa kulishawishi
benchi la ufundi.
Kocha wa Yanga, Ernest Brandts, aliiambia
Mwanaspoti jana Ijumaa kuwa ushindani baina ya mastraika ni mzuri kwani
utachochea wachezaji wake kujituma zaidi na kugombea namba.
“Wapo wengi lakini ni faida pia kwani watajituma
kwa kuhofiana wao kwa wao, kila mmoja atataka kucheza, hivyo itasaidia
timu kuwa na washambuliaji wenye uchu wa mabao kwani hakuna hata mmoja
ambaye atataka kuanzia benchi,”alisema Brandts.
Aliongeza: “Kila mara nimekuwa nikilalamikia
washambuliaji, lakini sasa naona mwanga mzuri mbele kwani wako wengi na
naamini watafanya kazi.”
Jerry Tegete
Amekuwa na misimu miwili mibaya na ametupia lawama matatizo ya goti kuwa ndiyo yalishusha kiwango chake.
Sasa amepanga kuibuka upya msimu ujao huku akikiri
kuwa kazi itakuwepo kwenye nafasi hiyo, lakini hahofii kwani anasema
kazi yake itakuwa kupiga mabao tu.
Didier Kavumbagu.
Alianza vizuri mzunguko wa kwanza msimu uliopita
alipopachika mabao manane, lakini mzungukko wa pili alifunga mabao
mawili tu na kumaliza katika nafasi ya pili kwa ufungaji akiwa amefunga
mabao 10.
Amerudi kwenye fomu sasa kwani amekuwa akifunga mazoezini na kwenye mechi za kirafiki.
Mrisho Ngassa
Wimbi la majeruhi ndiyo kitu pekee kinachoweza kumnyima namba kwenye kikosi cha kwanza, lakini vinginevyo ana namba ya uhakika.
Ameonyesha kiwango cha kuvutia kuanzia mazoezini na ni chaguo la kwanza la benchi la ufundi.
Shaban Kondo
Alisajiliwa hivi karibuni kutoka Msumbiji
alikokuwa akicheza soka la kulipwa. Ana umbo kubwa na urefu mzuri
unaostahili kwa mshambuliaji, amefunga mabao mazoezini na kwenye mechi
za kirafiki. Kocha ameonekana kumkubali na kumpa mbinu zaidi kila mara.
Said Bahanuzi
Anajulikana kwa jina la Straika wa Kagame baada ya
kutisha sana kwenye michuano hiyo iliyofanyika mwaka jana na kuibuka
mfungaji bora.
Lakini alipotea baadaye. Alifunga bao moja tu
kwenye Ligi Kuu msimu uliopita tena kwa penalti katika mechi ya watani
wa jadi Yanga na Simba. Kwenye mazoezi ya hivikaribuni ameonyesha
kiwango kizuri.
Hussein Javu
Ni mshambuliaji mpya kutoka Mtibwa Sugar, amepata
nafasi ya kusajiliwa na klabu hiyo baada ya kuonyesha uwezo mkubwa
katika mechi mbili dhidi ya Yanga na Simba ambazo zote alitupia magoli
nyavuni kwenye ligi iliyopita.
Makipa wa Ligi Kuu Bara wamiminika na kurundikana katika kikosi
cha Yanga kwa ajili ya mazoezi chini ya kocha Mkenya Razack Siwa.
Walinda mlando hao ni pamoja na Msafiri Davo
aliyekuwa Kagera Sugar, Nelson Kimath aliyeidakia Yanga miaka ya nyuma
wameungana na Deogratius Munishi ‘Dida’, Yusuph Abdul na Juma Kazembe.
Siwa aliliambia Mwanaspoti akisema: “Wapo wengi
ambao wanahitaji kuja kufanya mazoezi hapa tunawaangalia, mambo ya
usajili wao sijui lolote.”
Siwa ameongeza kuwa, hata kipa wa zamani wa klabu
hiyo na Taifa Stars, Ivo Mapunda ambaye kwa sasa anaichezea Gor Mahia
atajifua hapo.
Naye, Kimath amesema: “Nimeamua kuja kujifua hapa
kwa sababu Siwa ni kocha mzuri nimekuwa namjua kwa kipindi kirefu
alinifundisha miaka ya nyuma nilipokuwa nacheza hapa.”
Kutokana na hali hiyo, kocha Brandts anaamini kuwa
timu yake inazidi kuimarika na haoni kama atakuwa na tatizo lolote la
kutetea ubingwa wa Bara msimu mpya na hata kufanya vizuri katika
mashindano ya kimataifa.
“Mwenendo wa timu katika maandalizi yetu uantia
moyo, tunaendelea na kazi ya kuiimarisha timu ili kazi ikianza basi tuwe
na msimu bora, tunataka msimu bora pengine kuliko yote iliyotangulia,”
alisema kocha huyo akiwa na matumaini makubwa.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni