Gazeti la Wall Street Journal la Marekani limefichua
kwamba mpango wa kuiondoa madarakani serikali ya aliyekuwa rais wa
Misri, Muhammad Mursi ulitayarishwa miezi kadhaa iliyopita kati ya
makamanda wa jeshi la nchi hiyo na vinara wa kambi ya upinzani.
Ripoti ya gazeti hilo imeashiria vikao vya mara kwa mara
vya jeshi la Misri na vinara wa kambi ya upinzani na kwamba jeshi
liliwahakikishia wapinzani kwamba, litaingilia kati kumuondoa madarakani
Muhammad Mursi iwapo wapinzani wa serikali watafanikiwa kukusanya idadi
kubwa ya wananchi mitaani.
Gazeti la Wall Street Journal limefichua kwamba, miongoni
mwa waliokuwa wakihudhuria vikao hivyo ni pamoja na Muhammad el Baradei,
Amru Mussa na Hamdin Sabahi.
Limesema kuwa katika vikao hivyo kambi ya upinzani ilitaka
kuhakikishiwa kwamba, jeshi litaingilia kati kumuondoa madarakani Mursi
au la.
Maelfu ya wananchi wa Misri wanaendelea kufanya maandamano
katika miji mbalimbali ya nchi hiyo wakipinga hatua ya jeshi la nchi
hiyo ya kumuondoa madarakani rais aliyekuwa amechagulwia na wananchi
Muhammad Mursi mapema mwezi huu.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni