Jumapili, 28 Julai 2013

Wanajeshi wa Misri wauwa wanamgambo kumi Sinai


Vikosi vya usalama vya Misri vimewauwa kwa risasi wanamgambo kumi waliokuwa na silaha na kufanikiwa kuwatia nguvuni wanamgambo wengine 20 katika oparesheni yao ya masaa 48 huko katika jangwa la Sinai. Afisa mmoja wa jeshi la Misri ameeleza kuwa, operesheni zilizofanywa na vikosi vya nchi hiyo huko kaskazini mwa Sinai kwa ajili ya kuwasaka wanamgambo imepelekea kuuawa wanamgambo kumi waliokuwa na silaha. Jangwa la Sinai ambalo liko kwenye mpaka wa Misri na ardhi za Palestina zinazokaliwa kwa mabavu na Wazayuni, limekuwa na likishuhudia mapigano kati ya watu wenye silaha wasiojulikana na vikosi vya Misri tangu apinduliwe Rais Muhammad Morsi wa nchi hiyo mwezi Julai mwaka huu.
Wanajeshi wawili wa Misri waliuawa Alhamisi iliyopita katika shambulio la lililofanywa na watu wenye silaha kwenye kituo cha upekuzi cha kijeshi karibu na mji wa Sheikh Zuweid huko katika jangwa la Sinai.
Wakati huo huo watu wawili wameuawa leo katika matukio mawili tofauti nchini Misri wakati wafuasi wa Muhammad Morsi rais wa nchi hiyo aliyeng'olewa madarakani na jeshi walipopambana na wapinzani wa rais huyo wa zamani wa Misri. Watu hao wawili wameuawa leo katika mji wa bandari wa Suez na katika mji wa Kafr el Zayat, kaskazini mwa nchi hiyo.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni