Alhamisi, 29 Agosti 2013

Eto'o asaini mkataba na Chelsea

 
Samuel Eto'o
Chelsea imemsajili mshambuliaji wa Cameroon, Samuel Eto'o kutoka klabu ya Anzi Makhachkala ya Urussi.
Mchezaji huyo mwenye umri wa miaka thelathini na miwili amesaini mkataba wa mwaka mmoja na Chelsea.
Kocha wa Chelsea Jose Mourinho, aliamua kumsajili Eto'o baada ya maombi yake ya kumsajili nyota wa Manchester United Wayne Rooney kukataliwa.
Mapema wiki hii, ilibainika kuwa Rooney hakuwa tayari kulazimisha uhamisho wake kwa kuwasilisha ombi lake la kutaka kuondoka na hivyo kuzima matumaini ya Chelsea ya Kumsajili mchezaji huyo.
Mchezaji huyo ambaye ni mshindi mara nne wa mchezaji bora wa soka barani Afrika, alikuwa nyota wa AC Milan mwaka wa 2010 wakati Mourinho alipoiongoza kushinda kombe la klabu bingwa barani Ulaya.
Mwaka wa 2011, Eto'o alivunja rekodi ya kuwa mchezaji anayelipwa mshahara mkubwa zaidi duniani.
Klabu hiyo ya Anzi pia imemuuza kiungo wake Willian, mwenye umri wa miaka 25 kwa klabu ya Chelsea, baada ya mmiliki wa klabu hiyo mfanya biashara tajii Suleyman Kerimov kupunguza bajeti ya klabu hiyo.
Samuel Eto'o katika kikao na waandishi wa habari
Eto'o alianza kucheza soka ya kulipwa na klabu ya Real Madrid, lakini alisajiliwa na vilabu vya Leganes na Real Mollorca kwa mkopo kabla ya kupata mkataba wa kudumu Mallorca mwaka wa tisini na tisa.
Mchezaji huyo ambaye alikuwa katika kikosi cha Cameroon kilichoshinda kombe la mataifa ya Afrika mwaka wa 2002, vile vile alishinda kombe la Copa del Rey, kabla ya kujiunga na klabu ya Barcelona mwaka wa 2004.
Akiwa katika uwanja wa Nou Camp, alishinda kombe la klabu bingwa barani ulaya mara mbili mwaka wa 2006 na 2009 na alifunga bao katika fainali hizo mbili pamoja na kushinda kombe la ligi kuu ya La Liga mara tatu.
Mwaka wa 20098, Barcelona iliilipa Inter Milan pauni milioni arubaini pamoja na mchezaji huyo ili kumsajili Zlatan Ibrahimovic na mshambuliaji huyo alifanikiwa kushinda kombe la klabu bingwa barani Ulaya kwa mara nyingine chini ya Uongozi wa Mourinho katika uwanja wa San Siro.
Alijiunga na klabu ya Anzi na ripoti zinasema kuwa alikuwa akilipwa £167,825 kwa wiki mwaka wa 2011.

Mwanajeshi wa Tanzania auawa na M23 DRC

Ni lini Marekani itaishambulia Syria?


Rais Barack Obama wa 
Marekani.

MATUKIO YA KISIASA

mussashimba.blogspot.com

Rais Barack Obama wa Marekani amesema Jumatano (28.08.2013) bado hajasaini mpango wa kuishambulia Syria lakini kuna uwezekano wa kuchukuliwa hatua hiyo baada ya Marekani kuashiria haitohitaji ruhusa ya Umoja wa Mataifa.
Shutuma za kisiasa nchini Uingereza zimeweka mashaka iwapo Uingereza itaweza kujiunga na hatua ya kijeshi ya Marekani kuiadhibu serikali ya Rais Bashar al Assad wa Syria kutokana na shambulio lake la silaha za sumu iwapo hatua hiyo ya kijeshi itachukuliwa kabla ya wiki ijayo.
Timu ya wakaguzi wa Umoja wa Mataifa inaendelea na kibaruwa kigumu mjini Damascus kuchukuwa vipimo kwa wahanga wa shambulio hilo linalodaiwa kuwa la gesi ya sumu ambalo limeuwa mamia ya watu wiki iliopita na kutishia kuyaingiza mataifa ya magharibi katika vita vya wenyewe kwa wenyewe nchini Syria ambavyo hatima yake haijulikani.
Obama ambaye alikuwa ameonya kwamba matumizi ya silaha za sumu nchini Syria yatakuwa yamevuka mstari mwekundu uliowekwa na Marekani amesema serikali ya Marekani imefikia hitimisho la uhakika kwamba utawala wa Assad ndio wa kulaumiwa kwa shambulio hilo la silaha za sumu wiki iliopita.
Afisa mwandamizi wa Ikulu ya Marekani ameliambia shirika la habari la AFP kwamba serikali itawataarifu wabunge waandamizi leo hii kuhusu taarifa za kijasusi juu ya shambulio hilo la silaha za sumu.
Bado sikuamuwa
Rais Barack Obama wa Marekani.Rais Barack Obama wa Marekani.
Alipoulizwa lina anapanga kuamuru shambulio la Marekani dhidi ya Syria ambalo linatarajiwa kuanza na mashambulizi ya makombora Obama amekiambia kipindi cha televisheni cha Marekani cha PBS katika mahojiano kwamba bado hakufanya uamuzi.
Lakini ameonya kwamba Marekani inapanga kuiadhibu Syria ili kuhakikisha kwamba nchi hiyo haitorudia tena jambo hilo.
Amekiri kwamba mashambilizi hayo ya kiasi fulani yanayopangwa na Marekani hayatositisha mauaji ya raia nchini Syria na pia anaona kwamba kujihusisha katika vita vya wenyewe kwa wenyewe nchini humo ambayvo tayari vimeuwa watu 100,000 hakutosaidia hali hiyo.
Kiongozi huyo wa Marekani anayetaka kuacha haiba ya kumaliza vita vya kigeni na kutoingia katika vita vipya amesema ni muhimu kutuma ujumbe wa wazi sio tu kwa Syria bali duniani kote. Amesema inabidi wahakikishe kwamba wakati nchi zinapovunja kanuni za kimataifa juu ya silaha kama vile za sumu ambazo zinaweza kuwa kitisho kwao nchi hizo zinawajibishwa.
Diplomasia ndio suluhisho
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon.Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon.
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon ameyataka mataifa makubwa kuepusha mzozo huo wa Syria na kusema kwamba wakaguzi wa Umoja wa Mataifa inapaswa kupewa muda zaidi na kutowa ombi jipya kwa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kundokana na tafauti zao kuhusu Syria.
Amesema "Mazungumzo na usuluhishi wa kisiasa huu ni msimamo muhimu sana .Na ndio sababu kwa nini Umoja wa Mataifa umekuwa ukifanya maandalizi ya Mkutano wa Pili wa Kisiasa wa Geneva na ni matarajio yangu ya dhati mkutano huo utaitishwa kwa haraka."
Wakati huo huo Rais Vladimir Putin wa Urusi na mwenzake wa Iran Hassan Rouhani wanakubali kwamba matumizi ya silaha za sumu ni jambo lisilokubalika lakini wanapinga kuingiliwa kati kijeshi katika nchi hiyo mshirika wao.Taarifa ya Ikulu ya Urusi imesisitiza haja ya kutafuta njia za kuutatuwa mzozo huo kwa njia ya kidiplomasia tu.Marais wa nchi hizo mbili wameujadili mzozo huo wa Syria kufuatia ombi la Iran.
Mwandishi : Mohamed Dahman/AFP
Mhariri: Josephat Charo

Jumanne, 27 Agosti 2013

nyerere speech


tujikumbushe kidogo




TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI


                   TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI

Kikao cha Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) iliyomalizika leo imejadili kwa kina Masuala mbalimbali likiwemo pendekezo la Halmashauri Kuu ya CCM Mkoa wa Magharibi - Zanzibar la kumvua uanachama Ndugu Mansoor Yussuf Himid, Mjumbe wa Baraza la Wawakilishi wa Kiembesamaki.

Baadhi ya tuhuma za Ndugu Mansoor Yussuf Himid ni pamoja na:-

1.   Kushindwa kusimamia malengo ya CCM na kutekeleza masharti ya uanachama.

2.   Kushindwa kutekeleza wajibu wa mwanachama na kukiuka Maadili ya Kiongozi wa CCM.

3.   Kuikana Ilani ya CCM ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2010-2015 na kuisaliti CCM.

Baada ya kujiridhisha vya kutosha na tuhuma dhidi ya Ndugu Mansoor Yussuf Himid, Halmashauri Kuu ya CCM Taifa (NEC) imeridhia uamuzi wa Halmashauri Kuu ya CCM Mkoa wa Magharibi Zanzibar wa kumfukuza uanachama. Kwa uamuzi huo wa kumvua uanachama wa CCM Ndugu Mansoor Yussuf Himid, yeye kwa sasa sio Kiongozi tena wa CCM.

Imetolewa na:


Nape Moses Nnauye,
KATIBU WA NEC ITIKADI NA UENEZI CCM TAIFA
26/08/2013

KAMATI KUU CCM YABATILISHA UAMUZI WA HALMASHAURI KUU YA CCM BUKOBA
















 Katibu wa NEC Itikadi na Uenezi  wa CCM, Nape Nnauye akizungumza na waandishi wa habari kuhusu uamuzi wa kamati kuu wa kubatilisha kufukuzwa kwa madiwani wa Bukoba nje ya ukumbi wa NEC.

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI 
 Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya Taifa imejadili na kutolea maamuzi pamoja na mambo mengine suala la Madiwani wanane waliotangazwa kufukuzwa uanachama na Halmashauri Kuu ya CCM Mkoa wa Kagera.
 
Katika maamuzi yake, Kamati Kuu imebatilisha uamuzi uliofanywa na Halmashauri Kuu CCM ya Mkoa wa Kagera Agosti 13, 2013 wa kuwafukuza uanachama Madiwani hao. Hivyo Madiwani hao wanane ni wanachama halali wa CCM.
 
Kamati Kuu imetoa uamuzi huo, baada ya kubaini kuwa Halmashauri Kuu ya CCM Mkoa wa Kagera haikuzingatia Katiba ya CCM ya 1977 Toleo la 2012 Ibara ya 93 (15). Ibara hiyo inasomeka kuwa moja ya kazi ya Halmashauri Kuu ya CCM Mkoa ni:-
“Kumwachisha au kumfukuza uongozi kiongozi yeyote ambaye uteuzi wake wa mwisho unafanywa na Halmashauri Kuu ya CCM ya Mkoa, isipokuwa kwa suala la kumvua uanachama au uongozi Diwani lisifanyike hadi Kamati Kuu imearifiwa na kutoa maelekezo”.
 
Aidha, Kamati Kuu imewaonya Madiwani wa CCM wa Manispaa ya Bukoba, Mbunge wa Bukoba Mjini na Meya kwa kusababisha kukosekana kwa utulivu, mshikamano na amani katika Manispaa na Chama.
 
Kamati Kuu pia imeitaka Serikali kumwagiza mdhibiti na mkaguzi mkuu wa serikali(CAG) kufanya ukaguzi maalum wa haraka wa mambo yanayolalamikiwa dhidi ya Meya ili ukweli ujulikane na matokeo ya uchunguzi huo yasilishwe kwenye baraza la madiwani ili hatua stahiki zichukuliwe kwa mujibu wa sheria na taratibu zinazoongoza Serikali za Mitaa.
 
Wakati tuhuma hizo dhidi ya Meya zikichunguzwa; Kamati Kuu inawataka Madiwani wa CCM  kurejesha utulivu kwenye Manispaa na Chama kwa ujumla ili kufanikisha utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya CCM na kuwaletea maendeleo wananchi wa Bukoba.
 
Imetolewa na:-
 
Nape Moses Nnauye,
KATIBU WA HALMASHAURI KUU YA TAIFA YA CCM
ITIKADI NA UENEZI
27/08/2013
SOURCE:CCM BLOG

Slaa: Warioba asibezwe

CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kimesema Tume ya Mabadiliko ya Katiba inayoongozwa na Jaji mstaafu, Joseph Warioba, inawatakia mema Watanzania hivyo iungwe mkono.
Chama hicho kimesema Chama Cha Mapinduzi (CCM), hakitaki mabadiliko hapa nchini ndiyo maana kinabeza na kimejipanga kukwamisha baadhi ya mapendekezo yaliyomo kwenye rasimu ya Katiba mpya.
Kauli hiyo ilitolewa jana jijini Dar es Salaam na Katibu Mkuu wa CHADEMA, Dk. Willibrod Slaa, katika mikutano ya mabaraza ya wazi ya Katiba mpya.
Alisema viongozi na makada wa CCM wamekuwa wakiibeza rasimu hiyo iliyotolewa na Tume ya Mabadiliko ya Katiba inayoongozwa na Joseph Warioba kwa kuihofia kuwa inakiondoa madarakani chama chao.
Alisema katika mapendekezo ya tume hiyo imeweka wazi kuwa serikali itakayoingia madarakani italazimika kuchukua hatua kuzuia dhuluma, vitisho, ubaguzi, rushwa na upendeleo.
“Chama Cha Mapinduzi (CCM) hakitaki maneno hayo yawemo kwenye rasimu ya Katiba, wanajua wanavyotumia vitendo hivyo kuendelea kukalia madaraka,” alisema.
Dk. Slaa alisema Katiba mpya si ya Rais Jakaya Kikwete wala Chama Cha Mapinduzi (CCM) bali ni ya wananchi.
“Katiba ni ya wananchi, si ya Kikwete wala CCM, wanaobeza rasimu hiyo wanapaswa waheshimu maoni ya wananchi kwani yaliyomo humo yote ni mawazo yaliyokusanywa kutoka kwa wananchi,” alisema.
Dk. Slaa alisema CHADEMA inaunga mkono mapendekezo yaliyomo kwenye rasimu ya Katiba mpya yaliyotolewa na Tume ya Mabadiliko ya Katiba.
Dk. Slaa alisema CCM ina hofu na utawala wake kutokana na vipengele vingi vya rasimu ya Katiba kuminyaminya yaliyokuwa yakikinufaisha chama hicho tawala.
Alibainisha kuwa suala la Katiba mpya halikuwa ajenda ya CCM ndiyo maana viongozi wake walikuwa wakitoa matamko kupinga mchakato wake.
Dk. Slaa alisema katika uchumi tume imependekeza kuwa serikali ihakikishe inachukua hatua za kuwaletea wananchi maisha bora na kuondoa umaskini.
Alisema CCM hawataki wananchi waondolewe umaskini ili waendelee kuwatawala kwa urahisi, lakini CHADEMA inakubaliana na mawazo ya Tume ya Warioba.
Alibainisha kuwa Tume ya Warioba inapendekeza Katiba iseme kuwa rais atakayeahidi jambo ama utekelezaji wake akiingia madarakani asipotekeleza ashtakiwe lakini CCM wanakataa huku CHADEMA wakilikubali.
Dk. Slaa alisema chama chao kinaunga mkono hoja ya serikali tatu, kwakuwa ndiyo suluhu la matatizo ya muungano.
Alitoa mifano ya Sudan na Sudan Kusini, Eritrea na Ethiopia, kuwa muungano wa nchi hizo ulilazimishwa na matokeo yake ulisambaratika.
Alibainisha kuwa rasimu inataka wawekezaji walinde masilahi ya ndani si kuweka masharti hata kwa mambo tunayoyaweza.
“CHADEMA kinaunga mkono tume huru ya uchaguzi, kinakubaliana na nchi kuwa na tume ya maadili ya uongozi na yawe bayana lakini wenzetu wa CCM hawataki,” alisema.
Kuhusu suala la udini, alisema uhuru wa miaka 50 unaosifiwa ulipatikana kwa kuzingatia ibara ya 19 ya Katiba iliyopo inayotambua uwepo wa dini mbalimbali.
“Serikali haina dini, Watanzania ndio wenye dini. Ni wajibu wa serikali kuwalinda, wafanye ibada bila bughudha. Tumuunge mkono kupinga udini na kudumisha amani ili tuishi kama ndugu,” alisema Dk. Slaa.

SOURCE: CHADEMA  BLOG

Mbowe ashauri mambo muhimu kuwekwa wazi kwenye Rasimu

Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kimewataka wananchi kutoa maoni yao kwenye rasimu ya mchakato unaoendelea wa kuundwa kwa katiba mpya huku kikishauri mahitaji yote muhimu yawekwe wazi.
Akizungumza katika mikutano ya hadhara ya kuhamasisha wananchi kutoa maoni yao iliyofanyika wilayani Mbinga, Namtumbo na Songea, mkoani Ruvuma kuhusu mchakato huo, Mwenyekiti wa chama hicho, Freeman Mbowe, alisema maji ni moja ya mahitaji muhimu ya kila mwanadamu hivyo ni jukumu la serikali kuhakikisha kila mwananchi anapata maji safi na salama kwa ajili ya ustawi wa maisha yao ya kila siku.
Amesema kumekuwapo na kasumba miongoni mwa baadhi ya viongozi na wananchi kuwa huduma hiyo inatolewa kwa msukumo na utashi wa viongozi na inatafsiriwa kuwa ni hisani ikiwa kiongozi atajisikia kufanya hivyo lakini ikiwekwa kwenye katiba itamtaka kila kiongozi kuhakikisha wananchi wanapata maji safi na salama na kilio kisichoisha cha ukosefu wa maji katika maeneo mbalimbali nchini kitapungua kama siyo kutoweka kabisa.
Akizungumzia suala la elimu na lugha ya kufundishia kuanzia ngazi ya elimu ya msingi na kuendelea, alisema katiba inapaswa kutamka wazi kuwa lugha ya Kiingereza ndiyo lugha ya kufundishia na umuhimu wa lugha ya taifa ambayo ni Kiswahili upewe kipaumbele badala ya kuendelea na mfumo uliopo ambao umekuwa ni wa huria zaidi na kusababisha kuwapo kwa matabaka katika sekta hiyo muhimu kwa maendeleo ya taifa huku akishauri lugha za asili zisipuuzwe kwa ajili ya kulinda na kudumisha utamaduni wa Watanzania.
source chadema blog

Mchakato kura ya maoni ya Katiba waanza

Historia inatarajia kuandikwa katika Mkutano wa 12 wa Bunge la Jamhuri ya Muungano unaoanza leo, mjini Dodoma wakati litakaposafisha njia kwa Watanzania kwa mara ya kwanza, kupiga kura ya maoni ya Katiba.
Bunge litajadili Muswada wa Sheria ya Kura ya Maoni 2013, ambao ndiyo utakaotoa njia kwa Watanzania kuamua Katiba Mpya baada ya Bunge la Katiba kumaliza kazi yake.
Hii itakuwa mara ya kwanza kwa Tanzania Bara kupiga kura ya
maoni ya aina yoyote ile tangu Uhuru mwaka 1961 na ya pili kwa Zanzibar ambayo ilifanya hivyo kwa mara ya kwanza mwaka 2010 kutoa nafasi ya kuundwa kwa Serikali ya Umoja wa Kitaifa.
Kuelekea mchakato huo wa Katiba Mpya, Bunge pia litajadili Muswada wa Sheria ya Marekebisho ya Sheria ya Mabadiliko ya Katiba wa mwaka 2013.
Hatua hiyo inatokana na safari ndefu ya mchakato wa ukusanyaji wa maoni ya wananchi iliyoanza Aprili 13, mwaka jana kwa Rais Jakaya Kikwete kuzindua Tume ya Mabadiliko ya Katiba chini ya Jaji Joseph Warioba.
Juni 3, mwaka huu, Jaji Warioba alizindua Rasimu ya Katiba baada ya mchakato huo na kuruhusu uundwaji wa Mabaraza ya Katiba kwa kutegemea makundi maalumu ambayo mchakato wake unamalizika Agosti 31, mwaka huu.
Baada ya hatua hiyo, Bunge litapelekewa maboresho ya mapendekezo ya rasimu hiyo na kuyajadili ikiwamo kupitisha sheria ya mabadiliko hayo na baadaye kuweka muundo wa sheria na muundo wa kupigiwa kura hatua itakayofuata katika Bunge la Katiba baadaye Novemba, mwaka huu.
Kwa mujibu wa ratiba iliyotolewa na Ofisi ya Bunge, hoja hizo mbili zimetengewa siku tano kuanzia Septemba 9 hadi 13, mwaka huu na mjadala wa marekebisho hayo unatarajiwa kuchukua nafasi hasa kwa wabunge wa pande mbili, CCM cha Chadema juu ya kutengeneza muundo.
Chadema, kimeshatoa baadhi ya mapendekezo yake katika muswada wa Marekebisho ya Sheria ya Mabadiliko ya Katiba na Kura ya Maoni ikiwamo kupinga Rais kuteua wajumbe wa Bunge Maalumu wasiotokana na Bunge na Baraza la Wawakilishi Zanzibar.

Dk. Salim: Suala la uraia wa nchi mbili litatuliwe

Mjumbe wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Dk. Salim Ahmed Salim, amelitaka Baraza la  Katiba  Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa kuyapa uzito maoni ya Watanzania walioko nje ya nchi kuhusu suala la uraia wa nchi mbili na kuangalia jinsi ya kuyapatia ufumbuzi.

Dk. Salim  Ambaye pia ni Waziri Mkuu msataafu na Katibu Mkuu mstaafu wa uliokuwa Umoja wa Nchi Huru za Afrika (OAU),  aliyasema hayo jana jijini Dar es Salaam wakati akifungua mkutano wa Baraza hilo, ambao ulihudhuriwa na Mabalozi wastaafu, wafanyakazi wa wizara hiyo pamoja na taasisi zilizopo chini ya wizara hiyo.

Alisema kabla ya kuteuliwa kuwa mjumbe wa  Tume hiyo na hata baada ya kuteuliwa, amekuwa akisafiri mara kwa mara na kukutana na Watanzania  ambao wanaishi nje ya nchi na wengi wao wamekuwa wakizungumzia kuhusiana na suala la uraia, na wanalizungumzia zaidi suala la uraia wa nchi mbili, hivyo wizara hiyo inaweza kusaidia sana kwa kutoa mchango wake kutokana na uzoefu uliopo.

Aidha Dk Salim aliongeza kuwa wizara hiyo ina nafasi nzuri zaidi ya kuchambua na kushauri jinsi ya kutumia vizuri rasilimali za nchi kuendana na uzoefu walioupata kutokana na kufuatilia na kutembelea nchi nyingine duniani.

Akizungumzia suala la Muungano, alisema wizara hiyo ipo katika nafasi nzuri ya kuchangia katika suala la katiba gani inahitajika kwani moja ya dukuduku kubwa  la Wazanzibari ni kwamba Muungano kwa ulivyo sasa hauwapi nafasi ya kutambulika, na kupata ushirikiano katika medani ya kimataifa hasa kwa yale mambo ambayo si ya Muungano.

“Muundo wa Muungano umekuwa ni jambo ambalo limejadiliwa sana na kuonyesha tofauti kubwa kwa wachangiaji mbalimbali, kutokana na uzoefu wenu wa mambo ya nchi za nje na mchango wenu kama wizara inayotetea maslahi ya Tanzania kwa ujumla, na uzoefu uliopatikana mpaka sasa mnaweza mkachangia vizuri pia katika suala la Muungano,” alisema.

Chadema: Tunaikubali Rasimu ya Katiba, hatumkubali Jaji Warioba

Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kimesema kinakubaliana na rasimu ya Katiba kwa sababu asilimia 80 ya rasimu hiyo kwa kile inachoeleza inalinda maslahi ya wananchi.Kadhalika Chama hicho kimependekeza kuingizwa kwa kipengele cha haki ya wakulima na wafugaji katika Katiba mpya huku, kikiunga mkono kuwapo kwa serikali tatu .
Hayo yalisemwa na Katibu Mkuu wa chama hicho,Wilbroad Slaa, wakati akiwahutubia wananchi wa wilaya ya Mkuranga, mkoa wa Pwani, katika kampeni ya kukusanya maoni ya wananchi kuhusu Katiba mpya.
Slaa alisema Chadema inaunga mkono kuwapo kwa serikali tatu kama ilivyopendekezwa na Tume ya Mabadiriko ya Katiba mpya inayoongozwa na Jaji Mstaafu Joseph Warioba.
“Tunakubalina na Tume ya Warioba kwa asilimia 80, lakini tunatofautiana naye kwa asilimia 20, kitabu chake tunakipokea, na hoja zake tunazipokea, lakini yeye hatumkubali kwa kuwa ni kibaraka wa CCM,” alisema Slaa.
Kadhalika Slaa alimtaka Jaji Warioba kuhakikisha katiba mpya inasimamia haki, na kukemea vitisho, rushwa, na unyanyaswaji kwa wananchi.
Alisema Chadema inaitaka kuiona Tanzania kuwa nchi isiyo ya dhuluma huku utajiri na rasilimali zake ukihifadhiwa kwa maendeleo ya vizazi vijavyo.
Alisema Tume ya Jaji Warioba imechukua maoni ya Watanzania wengi na kuyaweka katika rasimu hiyo, lakini alitoa angalizo kwa tume hiyo kutoichakachua rasimu hiyo.
Baadhi wa wananchi wa Mkuranga walipata nafasi ya kutoa maoni yao huku wengi wakipendekeza kipengele cha Rais kushitakiwa pindi atakapoenda kinyume na utaratibu uliwekwa nchini.

Marekani yapima mikakati ya kijeshi dhidi ya Syria


epa03743404 A handout photograph made available by the White House on 13 June 2013 shows US President Barack Obama attending a meeting in the Situation Room of the White House, 02 April 2013. Seated, from left, are: National Security Advisor Tom Donilon; Lisa Monaco, Deputy National Security Advisor for Homeland Security and Counterterrorism; Tony Blinken, Deputy National Security Advisor; Ben Rhodes, Deputy National Security Advisor for Strategic Communications; and Avril Haines, Deputy Counsel to the President. Standing, from left, are: Brett Holmgren, NSS Director for Counterterrorism; Chris Fonzone, Special Assistant and Associate Counsel to the President; and Brad Smith, Deputy Legal Advisor. EPA/PETE SOUZA / THE WHITE HOUSE / HANDOUT This official White House photograph is being made available only for publication by news organizations and/or for personal use printing by the subject(s) of the photograph. The photograph may not be manipulated in any way and may not be used in commercial HANDOUT EDITORIAL USE ONLY/NO SALES +++(c) dpa - Bildfunk+++

MATUKIO YA KISIASA

Marekani yapima mikakati ya kijeshi dhidi ya Syria

Kufuatia shambulizi la silaha za sumu lililoua mamia nchini Syria, yaonekana muda wa kutafuta suluhu ya muafaka umekwisha. Marekani inaona msitari mwekundu umevukwa, na inapima uwezekano wa kuingilia kijeshi.
Baada ya kutokea shambulizi linalodhaniwa kuwa la kemikali, ambalo liliwauwa mamia ya raia na kujeruhi zaidi ya 3000 nchini Syria kwa mujibu wa shirika la misaada la madaktari wasio na mipaka, mataifa mengi ya magharibi na hasa Marekani, yanaaamini kuwa rais Bashar al-Assad ndiye anawajibika kwa shambulizi hilo. Kwa sababu kwa miezi kadhaa rais wa Marekani, Barack Obama, alionya kuwa matumizi ya silaha za kemikali yatamaanisha kuwa msitari mwekundu umevukwa, katika mazingira haya, laazima utawala wa Assad uchukuliwe hatua nzito. Kwa mujibu wa vyanzo vya Usalama vya Marekani, Ikulu ya mjini Washington inajadili njia tatu za kuchukuwa.
Eneo la kuzuiwa kuruka ndege linaweza kuwasaidia pakubwa waasi.Eneo la kuzuiwa kuruka ndege linaweza kuwasaidia pakubwa waasi.
Eneo lisiloruhusiwa ndege kuruka
Njia ya kwanza ni kuweka eneo lisiloruhusiwa ndege kuruka nchini Syria, hii ikimaanisha kuwa Wamarekani watazipiga marufuku ndege na helikopta za utawala katika baadhi ya maeneo. Hii itamaanisha kuwa vikosi vya Assad havitaweza tena kuwashambulia waasi kupitia angani. Hans-Joachim Schmidt, kutoka taasisi ya amani na utatuzi wa migogoro ya Hessian, anasema hatua hii ingekuwa ya msaada mkubwa kwa waasi kwa sababu "Assad hangeweza kuwashambulia waasi kwa kutumia helikopta na ndege zake za kivita. Hii ingewanufaisha moja kwa moja waasi."
Lakini Paul Rogers, mtaalamu wa masuala ya usalama kutoka shirika la ushauri la Oxford Reseach Group la Uingereza, anasema Marekani laazima izime mifumo ya ulinzi wa angani ya Syria, jambo ambalo anasema litakuwa ghali na la hatari sana kwa kuzingatia kuwa Urusi iliahidi kuipatia Syria mitambo ya kisasa. Juu ya wasiwasi huo, Hans-Joachim Schmidt anasema ikiwa kweli Urusi imekwisha iuzia Syria mitambo hiyo ya kisasa, basi Wamarekani watapata taabu sana. Lakini anasema haoni uwezekano mkubwa kwa Marekani kutumia mkakati huu, kwa sababu utawavuta zaidi katika mgogoro huu, kitu ambacho serikali ya Marekani haitaki. Wakati huo huo, kanda isiyoruhusiwa kuruka ndege laazima iidhinishwa na baraza la usalama la Umoja wa Mataifa, na huko Urusi na China bila shaka zitatumia kura ya turufu kuizuia.
Waziri wa mambo ya kigeni wa Marekani John Kerry ametoa matamshi yanayoashiria mashambulizi dhidi ya Assad yako njiani.Waziri wa mambo ya kigeni wa Marekani John Kerry ametoa matamshi yanayoashiria mashambulizi dhidi ya Assad yako njiani.
Mashambulizi dhidi ya maeneo ya kimkakati
Njia nyingine ni kushambulia maeneo ya kimkakati kwa makombora na maroketi kama vile viwanja na njia za kurukia ndege, na hivyo kudhoofisha uwezo wa jeshi la angani la Syria. Marekani ina meli kadhaa za kivita na nyambizi katika bahari ya Mediterannean, ambazo zinaweza kutumiwa kutekeleza mashambulizi ya namna hii na kufanya vigumu kwa ndege kuruka na kutua.
Lakini uharibifu kwa njia za ndege unaweza kukarabatiwa haraka. Schmidt anaiona njia hii kuwa ndiyo yenye uwezekano mkubwa zaidi wa kutumiwa, licha ya ukweli kuwa nayo itahitaji kuidhinishwa na baraza la usalama. "Wamarekani hawataki kujiingiza moja kwa moja katika mgogoro huu, hivyo shambulio la kijeshi lingekuwa ishara yenye ufanisi, japokuwa yenye mipaka, ya kuzuia matumizi zaidi ya silaha za kemikali," anafafanua mtafiti wa amani na utatuzi wa migoro Hans-Joachim Schmidt.
Kuwapatia waasi silahaNjia ya tatu inaweza kuwa kuwapatia silaha waasi. Hadi sasa Marekani haijawapatia msaada wa silaha waasi, ukiachilia mbali misaada ya kawaida kama vile vifaa vya tiba. Lakini Rogers anasema waasi wamekuwa wakipokea vifaa vya kijeshi kutoka Saudi Arabia na Umoja wa falme za Kiarabu kupitia Uturuki na Jordan. Lakini anasisitiza kuwa uwezekano wa waasi kupatiwa silaha moja kwa moja na Marekani ni mdogo sana, kwa sababu watahitaji kupewa mazoezi kwanza kabla hilo halijafanyika. Hofu nyingine kuhusiana na hili, ni silaha hizo kuangukia mikoni mwa kundi lenye itakadi kali la Al-Nusra Front.
Rais Bashar al-Assad akisalimiana na wanajeshi wake mjini Damascus hivi karibuni.Rais Bashar al-Assad akisalimiana na wanajeshi wake mjini Damascus hivi karibuni.
Na diplomasia je?
Lakini Uingiliaji wa tahadhari bado unabaki kuwa uingiliaji, na kwa hivyo Marekani bado inasita kufanya hivyo, kwa kuzingatia madhara yake. Tayari rais Bashar al-Assad ameonya kuwa hatua yoyote ya kuingilia kati kijeshi itasababisha moto utakaoizingira kanda nzima ya mashariki ya kati. Iran nayo inaweza kuliimarisha kundi la Hezbollah dhidi ya Israel na kundi la Taliban linaweza kuzidisha mashambulizi dhidi ya maslahi ya Marekani.
Schmidt kwa hivyo anapendekeza njia ya nne ambayo haizungumzwi katika vyombo vya habari kwa sasa: Shinikizo la diplomasia. Hata hivyo, mtaalamu huyo anahisi kuwa uamuzi wa kuishambulia Syria kijeshi umekwisha chukuliwa na kinachosubiriwa ni lini na vipi. Kinachoonekana sasa ni kwamba Marekani inatafuta washirika katika operesheni hii.
Mwandishi: Jansen Klaus
Tafsiri: Iddi Ismail Ssessanga
Mhariri: Josephat Charo

Wanajeshi wa UN wasombwa na maji-Darfur


Wanajeshi wa kutunza amani wa UN nchini Sudan.
Wanajeshi wanne wa kutunza amani wa Umoja katika eneo la Darfur nchini Sudan hawajulikani waliko baada ya kusombwa na mafuriko.
Afisa mmoja wa Umoja wa Mataifa, Rania AbdulRahman, amesema kuwa wanajshi hao walikuwa wakisindikiza msafara wa magari ya kutoa misaada, wakati waliposombwa na maji.
Afisa huyo amesema kuwa wanajeshi wengine wawili walipatikana wakiwa hai na kundi la uokoaji
Shirika la Umoja wa Mataifa wa Afya Duniani WHO, limesema kuwa zaidi ya watu laki tatu nchini Sudan, wameathiriwa na mafuriko na zaidi ya watu hamsini wamefariki mwezi huu.
Shirika hilo limesema kuwa eneo linalokaribia mji mkuu wa Khartoum ndilo limeathirika zaidi na mafuriko hayo ambayo ndiyo mabaya zaidi kuwahi kukumba eneo hilo kwa zaidi ya miaka ishirini na mitano iliyopita.

Wanajeshi wakwama kwenye mto

Kikosi cha Umoja wa Mataifa na kile cha Muungano wa Afrika katika eneo hilo la Darfur, UNAMID, ndilo kubwa zaidi duniani na lina zaidi ya wanajeshi elfu ishirini.
Mafuriko nchini Sudan
Wanajeshi hao wa kutunza amani walikuwa wakielekea eneo la Misterei, takriban kilomita hamsini, Kusini Magharibi mwa mji mkuu wa eneo hilo Geneina, na msafara wa shirika la Umoja wa Mataifa la Mpango wa Chakula Duniani WFP, wakati msafara wao uliposomba na mafuriko.
Msemaji wa WFP Amor Almagro amethibitisha kuwa wafanyakazi wa shirika hilo la WFP waliokuwa kwenye msafara huo, watano kati yao raia wa Sudan na wawili wa mataifa ya Kigeni wako salama.
Umoja wa Mataifa haujatoa majina au uraia wa wanajeshi hao ambao hawajulikani waliko.
Mwaka uliopita, katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon, alilieleza baraza la usalama la Umoja huo kuwa wanajeshi watatu kutoka Tanzania walizama majini baada ya gari lao la kijeshi, kukwama katika mto mmoja nchini Sudan.
Katibu huyo mkuu vile vile alilieleza baraza hilo kuwa kikosi chake nchini Sudan kinakabiliwa na upungufu wa vifaa vya kutosha na vya kisasa, hali ambayo inaadhiriwa juhudi zao za kutunza amani katika eneo hilo la Darfur.
Wanajeshi hao wa Umoja wa Mataifa, wako katika eneo hilo la Darfur, kujaribu kumaliza mzozo uliodumu kwa miongo kadhaa kati ya wanajeshi wa serikali na waasi.
Umoja wa Mataifa unakadiria kuwa zaidi ya watu laki tatu wameuawa kwenye mzozo huo wa Darfur.

Wanafunzi wote wafeli mtihani wa sekondari


Wanafunzi wote walifeli mtihani wa kujiunga na chuo kikuu cha Liberia
Kwa mara ya kwanza katika historia ya Liberia, wanafunzi wote wamefeli mtihani wao wa mwisho wa sekondari na hivyo kumaanisha kuwa hakuna hata mmoja ambaye atafuzu kuingia chuo kikuu.
Waziri wa elimu wa Liberia amesema ameshinda kufahamu ni kwa nini hakuna wanafunzi hao wamefeli kiasi hicho.
Zaidi ya wanafunzi elfu ishirini na watano walianguka mtihani huo ambao ungewapa fursa ya kujiunga na chuo kikuu cha Liberia ambacho ni moja ya vyuo vikuu vinavyoendesha na serikali.
Lakini wasimamizi wa chuo hicho wameiambia BBC kuwa wanafunzi hao hawakuwa makini na ufahamu mzuri wa lugha ya Kiingereza ambayo ilitumiwa kuwatahini.
Taifa la Liberia linaendelea kujinasua kutokana na athari za mapigano ya wenyewe kwa wenyewe yaliyomalizika zaidi ya miaka kumi iliyopita.
Rais wa Liberia, Ellen Johnson Sirleaf, ambaye pia ni mshindi wa tuzo ya amani ya Nobel, amekiri kuwa mfumo wa elimu nchini humo bado ungali duni na unahitaji marekebisho ya dharura.
Mwandishi wa BBC mjini Monrovia, anasema shule nyingi nchini humo havina vifaa vya kimsingi na waalimu waliohitimu.
Lakini hii ni mara ya kwanza katika historia ya taifa hilo kwa wanafunzi wote kufeli mtihani huo licha ya kulipa ada ya usajili ya dola ishirini na tano.
Chuo hicho kikuu ambacho kina idadi kubwa ya wanafunzi hakitakuwa na wanafunzi wa mwaka wa kwanza wakati muhula mpya utakapoanza mwezi ujao.
Lakini wanafunzi wengi wanasema hawajaamini matokeo ya mtihani huo na waziri wa Elimu Etmonia David-Tarpeh, ameiambia BBC kuwa anatarajia kukutana na wasimamizi wa chuo hicho ili kujadili suala hilo.

Jumatatu, 26 Agosti 2013






They Say You Can't Teach An Old Dog New Tricks. So When Did He Learn This Trick Exactly?

                   Impossible Pool Trickshot                                                                                                                                                                                                                                                                                                              
                                                Impossible Pool Trickshot                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                          

Askari wa Tanzania na A/ Kusini wajeruhiwa Kongo

Askari wa Tanzania na A/ Kusini wajeruhiwa Kongo
Msemaji wa kikosi cha kulinda amani cha Umoja wa Mataifa katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo nchini MONUSCO ametangaza kuwa, kwa akali askari watatu wa vikosi hivyo akiwemo mwanajeshi mmoja wa Afrika Kusini, wamejeruhiwa vibaya katika shambulizi la kuvizia lililofanywa na waasi huko mashariki mwa nchi hiyo. Shambulio hilo lilitokea baada ya waasi wa M23 kurusha kombora katika eneo viliko vikosi vya UN umbali wa karibu kilometa nne kaskazini mwa mji wa Goma, makao makuu ya jimbo la Kivu Kaskazini. Kwa mujibu wa msemaji wa MONUSCO, askari wengine wawili waliojeruhiwa ni Watanzania. Habari zaidi zinasema kuwa, kwa akali askari wa Afrika Kusini, wameshapambana mara mbili na waasi hao. Wakati huo huo, viongozi wa Pretoria, wamekanusha kujiri mashambulizi ya askari wa nchi hiyo dhidi ya waasi wa M23 nchini Congo DRC.

Iran yatengeneza ndege ya kisasa isiyo na rubani

Iran yatengeneza ndege ya kisasa isiyo na rubani
Wataalamu wa Iran wanaunda ndege ya kisasa kabisa ya kivita isiyo ya rubani na yenye uwezo wa kupiga picha za matukio mbali. Kiongozi anayesimamia zoezi hilo Hassan Akbari amesema kuwa, ndege hiyo ina sifa za kipekee katika kutekeleza mashambulizi ya hali ya juu katika mazingira ya kivita. Aidha katika sifa zake nyingine ni pamoja na kuwa na uwezo wa kuzalisha umeme kwa ajili ya kuhifadhi muundo wake na hivyo kuiepusha na hatari tarajiwa. Ameongeza kuwa mbawa za ndege hiyo zina urefu wa sentimita 170 na hivyo kuifanya iweze kuhimili uzito wa ndege na kuwa na uwezo mkubwa wa kuruka. Kwa upande mwingine ndege hiyo, ina uwezo wa kuchukua picha kwa umbali na kisha kuzisajili na kuainisha maeneo ya vita.
Visa vya binadamu kushiriki ngono na wanyama


Na Flora Martin Mwano>>
 sikiliza hapa>>>http://www.kiswahili.rfi.fr/aef_player_popup/rfi_player#
Karibu katika makala ya Habari Rafiki na hii leo tunajadili matukio ya binadamu kushiriki ngono au kufanya mapenzi na wanyama kuonekana vikizidi kushika kasi katika siku za hivi karibuni, nini chanzo cha mambo haya na nini suluhisho lake? Ungana na Flora Mwano mwanzo mpaka mwisho wa Makala hii.

Msafara wa wachunguzi wa Umoja wa Mataifa washambuliwa Syria

Na Victor Melkizedeck Abuso
Msafara wa wachunguzi wa Umoja wa Mataifa waliokuwa njiani kwenda karibu na mji wa Damascus nchini Syria kuanza kuchunguza ikiwa silaha za kemikali zilitumiwa kutekeleza shambulizi wiki iliyopita umeshambuliwa.

Umoja wa Mataifa hata hivyo haujasema ni nani aliyeshambulia msafara huo, ila imebainika kuwa gari la kwanza katika msafara huo lilivamiwa na kusababisha wachunguzi hao kurudi walikokuwa wametoka.
Uchunguzi huo ulitarajiwa kuanza siku ya Jumatatu siku moja baada ya serikali ya rais Bashar Al Assad kukubali kufanyika kwa uchunguzi huo baada ya waasi kuituhumu serikali  kutumia silaha za kemikali dhidi ya wafuasi wao.
Watalaam hao 20 wamekuwa Syria tangu tarehe 18 mwezi huu kuchunguza maeneo matatu yanayodhaniwa silaha za kemikali zilitumiwa dhidi ya wapinzani miezi kadhaa iliyopita.
Rais Bashar Al Assad amesema kuwa tishio la Marekani kuwa ikiwa uchunguzi utabaini kuwa silaha hizo zilitumiwa, italazimika kuingilia mzozo huo kijeshi ni jambo ambalo halikubaliki kamwe.
Akihojiwa na gazeti la kila siku la Urusi la Izvestia Assad amesisitiza kuwa Marekani haitafaulu na kamwe hawezi kuwa kibaraka cha mataifa ya Magharibi na ataendelea kupambana na makundi ya kigaidi yanayolenga kuiangusha nchi yake.
Mwaka uliopita, rais Obama alionya kuwa ikiwa serikali ya Syria itatumia silaha za kemikali dhidi ya wapinzani , nchi yake itaivamia kijeshi.
Waziri wa Mambo ya nje wa Uingereza William Hague naye amesema kuwa ikiwa silaha hizo zilitumiwa ni sharti hatua zichukuliwe lakini anahofia kuwa huenda ushahidi wa kufahamu ukweli umeshaharibiwa.
Serikali ya Assad imeendelea kusisitiza kuwa haiwezi na haijawahi kutumia silaha za kemikali dhidi ya wapinzani na itafanya hivyo ikiwa nchi yake itavamiwa na watu kutoka nje.
Machafuko nchini Syria yamesabisha zaidi ya watu Laki Moja kupoteza maisha kwa kipindi cha miaka miwli iliyopita kwa mujibu wa takwimu za Umoja wa Mataifa, na Mamilioni kusalia kuwa wakimbizi wakiwemo watoto.
Suluhu ya mzozo wa Syria inasalia kuwa kitendawili baada ya juhudi za Kidiplomasia kugonga mwamba.

Wanaume 2 wagawana mke mmoja Kenya


Mwendwa ni mmoja wa wanaume hao walioamua kugawana mke mmoja.
Wanaume wawili nchini Kenya wameibuka na mbinu isiyo ya kawaida ya kupata suluhu ya kupigania mwanamke ambaye wote wanampenda Wamesaini mkataba wakikubaliana kuishi nae kwa zamu.
Silvester Mwendwa ni mmoja wa wanaume hao. Ameeleza BBC kwanini binafsi anamuhusudu mwanamke huyo.
Mmoja ya wa wanaume hao alisema haoni ubaya wowote kwa yeye na mwenzake kumuoa mwanamke mmoja.
Amehoji sheria ya sasa inayoruhusu wanaume kuoa wanawake wengi na wakati huo huo kuharamisha mpango kama huo kwa kina mama.
Sylvester Mwendwa anasema wazazi wake wamekubali na mpango wake na wako tayari kumtolea mahari.
Wanaume hao wawili walikubali kumuoa mwanamke huyo baada ya kugundua kwamba kumbe wote wana uhusiano wa kimapenzi naye.
Na kumbe mwanamke huyo alikuwa ameahidiana na kila mmoja wao kwamba angelifunga nao ndoa bila ya wao kujuana.
Lakini walipogunduana , ilikuwa ni ugomvi wa mara kwa mara lakini mwanamke huyo alipoambiwa amchague mnmoja wao, alishindwa. Akasema anawapenda wote wawili.
Na baada ya hapo watatu hao waliafikiana kusaini mkataba ambao utaruhusu wanaume hao wawili kuishi na mwanamke huyo kama bwana na bibi ila kila mmoja wao atakuwa na wakati wake wa 'kwenda kumjulia hali.'
Vile vile mkataba huo unawashurutisha kugawana majukumu yote ya nyumbani ikiwa ni pamoja na kuwalea watoto na kutowabagua kwa kuwa wote watakuwa na haki sawa.
Hata hivyo kwa mujibu wa sheria za kenya ni haramu kwa mwanamke kuolewa na wanaume wawili na mkataba huo sasa umeibua mjadala mkali wa kisheria, huku sheria mpya ya ndoa ikitarajiwa kujadiliwa na kuidhinishwa bungeni.