Jumamosi, 24 Agosti 2013

Katiba kuirejesha Misri kwenye zama za Mubarak?!

Katiba kuirejesha Misri kwenye zama za Mubarak?!
Marekebisho ya Katiba ya Misri yaliyopendekezwa na tume iliyoundwa na watawala wa nchi hiyo waliowekwa madarakani na jeshi yanaweza kuwapa nguvu za kurudi madarakani wanasiasa wa zama za utawala wa dikteta wa nchi hiyo Hosni Mubarak. Ripoti iliyotolewa na tume hiyo ya watu 10 ambayo ilivuja siku ya Jumatano iliyopita imependekeza kufutwa vifungu 32 vya katiba ya Misri yenye jumla ya vifungu 236 na kufanyiwa marekebisho vifungu vingine 109 vya katiba hiyo. Shakhsia mbalimbali nchini Misri wakiwemo wanaharakati wa kutetea haki za kiraia na wa makundi ya Kiislamu wamelalamikia marekebisho hayo ambayo yatajadiliwa na baraza la wajumbe 50 watakaoteuliwa na serikali ya mpito. Miongoni mwa mapendekezo yaliyotolewa ni ya ibara mpya isemayo bunge pekee ndilo litakalokuwa na mamlaka ya kumwondoa madarakani Rais. Marekebisho mengine makubwa yaliyopendekezwa na tume hiyo ni ya kurejesha mfumo wa upigaji kura wa zama za utawala wa Mubarak wa kuwapigia kura wagombea binafsi tu badala ya kutengwa baadhi ya viti vya bunge kwa ajili ya orodha za vyama vya siasa. Kwa mujibu wa katiba ya sasa ya Misri iliyotungwa baada kung'olewa madarakani utawala wa dikteta Hosni Mubarak, thuluthi mbili za viti vya bunge zinapatikana kupitia orodha za wagombea wa vyama vya siasa, mfumo ambao uliiwezesha harakati ya Ikhwanul Muslimin na vyama vingine vya Kiislamu kupata ushindi wa asilimia 80 za viti katika uchaguzi wa bunge uliofanyika nchini humo…/


Hakuna maoni:

Chapisha Maoni