Waziri wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki wa Tanzania amesema kuwa, ugomvi wa wanasiasa katika jumuia hiyo hauwezi kuathiri shughuli za kibiashara na uchumi wa Tanzania kwa kuwa wafanyabiashara wanaangalia faida zaidi katika shughuli zao. Samuel Sitta amesema hayo wakati akijibu maswali ya waandishi wa habari waliotaka kujua athari za kiuchumi zitakazopatikana baada ya kuwapo taarifa ya wafanyabiashara wa Rwanda kutaka kupitisha mizigo yao katika bandari ya Mombasa badala ya ile ya Dar es Salaam. Sitta ameongeza kuwa, taarifa ya wafanyabiashara wa Rwanda kuazimia kutumia bandari ya Mombasa si za ukweli na kwamba wanaofanya hivyo ni wale waliokosa zabuni mbalimbali. Hivi karibuni msemaji wa Chama cha mizigo nchini Tanzania (Tatoa) Elias Lukumay, aliiambia kamati ya Bunge ya Bajeti kuwa nchi za Rwanda na Uganda zimekubaliana kutumia bandari ya Mombasa, Kenya kutokana na urasimu unaodaiwa kuwepo katika bandari ya Dar es Salaam. Uamuzi huo wa Rwanda na Uganda unatafsiriwa kuwa unatokana na msigano wa kisiasa ulioibuka hivi karibuni baina ya Rais Jakaya Kikwete na Rais Paul Kagame wa Rwanda baada ya ushauri wake wa kumtaka Kagame akutane na waasi wa FDLR kwa ajili ya kujadili amani ya taifa lao.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni