Kwa akali watu 42 wameripotiwa kuuawa na wengine wasiopungu 500 kujeruhiwa, katika milipuko miwili mikubwa ya kigaidi, iliyotokea mjini Tripoli, kaskazini mwa Lebanon. Habari zinasema kuwa, miripuko hiyo, imetokea leo baada ya sala ya Ijumaa katika mji huo ambapo wa kwanza umetokea karibu na msikiti wa Al-Taqwa, huku wa pili ukitokea karibu na msikiti wa As-Salam katika eneo la Mina. Habari zaidi zinasema kuwa, kuna uwezekano idadi ya vifo ikaongezeka kutokana na ukubwa wa miripuko hiyo. Habari za awali zinasema kuwa, moja ya miripuko hiyo umetokea umbali wa mita chache kutoka nyumba ya Najib Mikati Waziri Mkuu wa Lebanon aliyejiuzulu. Hata hivyo ofisi ya Waziri Mkuu huyo, imetangaza kuwa, Mikati hakuwepo mjini Tripoli. Shirika la Habari la Lebanon limetangaza kuwa, mripuko wa pili umepelekea kuchimbua shimo lenye urefu wa mita tano na upana wa mita mbili na nusu, huku ukiharibu vibaya nyumba za jirani na tukio na kuharibu pia zaidi ya magari 60. Tarehe 15 Agosti, kulitokea shambulio la kigaidi katika mji wa Al-Ruwaysi kusini mwa mji mkuu Bairut, Lebanon na kupelekea watu 25 kuuawa na wengine zaidi ya 300 kujeruhiwa.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni