Jumamosi, 21 Septemba 2013

Marekani yagonga mwamba katika kadhia ya Syria

                                                        Rais Barack Obama wa Marekani
                                                                 Rais Barack Obama wa Marekani

"Janga la kusikitisha lililotokea tarehe 21 Agosti nchini Syria ni matokeo ya moja ya mashambulio kadhaa yaliyofanywa katika kipindi cha miaka miwili na nusu iliyopita na kusababisha vifo vya makumi ya maelfu ya watu katika nchi hiyo." Hayo ni maneno ya Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki Moon aliyotoa kufuatia shambulio la kutia shaka na lililoratibiwa la silaha za kemikali, lililofanywa kwenye viunga vya mji mkuu wa Syria, Damascus. Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa aliendelea kutoa dukuduku lake kwa kusema kama ninavyomnukuu tena: "Tangu shambulio la kemikali lililofanywa na utawala wa Saddam Hussein huko Halabche mwaka 1988, hili ni shambulio muhimu zaidi lililothibitisha kutumiwa silaha za kemikali dhidi ya raia nchini Syria," mwisho wa kumnukuu.
Kutokana na ripoti ya timu ya wataalamu wa Umoja wa Mataifa kwamba silaha za kemikali zilitumiwa huko nchini Syria haibaki tena hata chembe ya shaka kwamba maafa ya kibinadamu yametokea nchini humo. Hata hivyo wanachotarajia walimwengu ni kubainishwa wahusika wa jinai hiyo chafu na ya kusikitisha. Kwa upande mmoja Marekani na waitifaki wake kwa kutegemea madai ya wapinzani wa nje ya Syria na magaidi walioko ndani ya nchi hiyo wanaituhumu serikali ya Damascus kuwa ndio iliyohusika na shambulio la silaha za kemikali la Agosti 21. Lakini kwa upande mwengine, kutokana na nyaraka za ushahidi ilizotoa, serikali ya Syria imekanusha madai hayo na kuyaelezea kuwa ni sehemu ya njama za makundi ya kigaidi yanayoungwa mkono na madola ya kigeni ya kufanikisha uingiliaji wa kijeshi dhidi ya nchi hiyo.
Wizara ya Mambo ya Nje ya Syria imetuma barua kwa Rais wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa na kwa Katibu Mkuu wa umoja huo na kueleza kwamba uungaji mkono wa Marekani na waitifaki wake kwa makundi ya kigaidi nchini Syria ni ukiukaji wa wazi wa sheria za kimataifa na maazimio ya Baraza la Usalama kuhusiana na mapambano dhidi ya ugaidi.
Wizara ya Mambo ya Nje ya Syria imeashiria vitendo vinavyofanywa waziwazi na Magharibi vya kutoa mafunzo, hifadhi na utumaji silaha kwa magaidi nchini Syria na kufafanua kwamba wapinzani wenyewe wanakiri kwamba makundi ya kigaidi yanapokea shehena kubwa kubwa za silaha kupitia mipaka ya Uturuki, Jordan na Lebanon. Wakati huohuo japokuwa mpango uliobuniwa na Russia umezima moto wa vita uliotaka kuwashwa na Marekani nchini Syria, na hadi sasa licha ya Washington kuhaha huku na kule imeshindwa kuushawishi ulimwengu uiunge mkono katika mpango wake wa kuishambulia kijeshi Syria lakini viongozi wa nchi hiyo wangali wameshikilia uzi uleuele wa kuzidisha mbinyo dhidi ya serikali ya Damascus. Kwa mujibu wa makubaliano yaliyofikiwa kati ya Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani John Kerry na mwenzake wa Russia Sergei Lavrov, Syria inapaswa kusaini mkataba unaopiga marufuku silaha za kemikali na kukabidhi silaha zake kwa jamii ya kimataifa ili ziangamizwe. Kulingana na mpango huo wenye vipengele sita ulioafikiwa na Washington na Moscow, serikali ya Syria inatakiwa ndani ya kipindi cha wiki moja kinachomalizika leo Jumamosi iwe imekabidhi orodha ya maghala ya silaha zake za kemikali na kuyaweka chini ya udhibiti wa kimataifa. Hii ni katika hali ambayo viongozi wa Syria sio tu wametangaza kuwa wako tayari kutoa ushirikiano juu ya suala hilo lakini kwa upande wa ndani pia imeelezea uwezekano wa kutangaza usitishaji vita katika medani za mapambano. Hapo kabla pia serikali ya Damascus ilikuwa imeshatangaza kuwa iko tayari kuhudhuria kikao cha Geneva 2, lakini upande wa wapinzani umekwamisha kufanyika kikao hicho kwa kutoa masharti na shuruti kadhaa. Hakuna shaka kuwa uungaji mkono wa Marekani na waitifaki wake kwa ugaidi ulioratibiwa dhidi ya Syria ndio uliokwamisha kupatikana ufumbuzi wa kisiasa kwa mgogoro wa nchi hiyo. Ni muda mrefu sasa Washington imegonga mwamba na kushindwa kufikia malengo yake nchini Syria, na msimamo ulioonyeshwa na jamii ya kimataifa na walimwengu kwa ujumla wa kutokuwa tayari kuiunga mkono serikali ya Barack Obama katika kuanzisha vita dhidi ya Syria umedhihirisha hofu na wasiwasi wa jamii ya kimataifa juu ya sera za upigaji upatu wa vita za White House wanazozitekeleza viongozi wa nchi hiyo kwa kufuata amri na maelekezo ya Wazayuni.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni