Barua kwa Mke Wangu...
...A Letter to My Wife...
28th January 2019, Monday
Ni miaka miwili sasa imepita tangu tufunge ndoa na mke wangu, Asante.
Binti mrembo na mcha Mungu. Mahali tulipokutana mimi na yeye ni hadithi
ambayo nitaomba kuwasimulia siku nyingine. Ni katika zile sehemu ambazo
mtu kamwe usingetegemea/tarajia kumpata binti mwenye haiba kama zake
(We found love in a hopeless place…Rihanna Cc:
BAK).
Kama nilivyokwisha eleza hapo mwanzo, zaidi ya urembo wake,ambao
hauringii wala kuutumia vibaya kama wengine, ni binti mmoja mpole
ajabu, anajua kujali na anajituma. Ni mchango mkubwa katika maisha
yangu kwani hapa nilipofika kama sio mawazo na changamoto zake basi
sidhani kama hata robo yake ningefika. Ama hakika wahenga hawakukosea
waliposema, ‘kosea njia utaelekezwa, ila ukikosea mke…’
Naam, ni siku tena ya kumbukumbu ya kuzaliwa kwangu na pia kumbukumbu
ya miaka miwili ya ndoa. Ndoa tuliyofunga January 28, 2017 siku ya
Jumamosi..still fresh in my mind. Ni siku ambayo kwa kawaida ya watu
walio katika ndoa, tena ya ‘Kikristo’ walitakiwa kuwa pamoja
wakimshukuru Mungu kwa mbali alipowafikisha.
Haikuwa hivyo kwangu. Wiki mbili kabla ya siku hii nilikuwa
nimeshapanga na Zulekha (shombeshombe again!damn me) kukutana. Zulekha
aliwahi kuwa rafiki yangu wa kike tulipokuwa chuoni. Ni binti
aliyelelewa katika maadili ya dini sana. Very strict na kwa hiyo
mahusiano yoyote ya kimapenzi na mwanaume asiye wa Kiislamu yalikuwa
mwiko/kiwicho/taboo kwao.
Ila ukweli ni kuwa mapenzi hayafungwi na dini, hivyo tuliendelea
kuwasiliana na tupatapo nafasi kufanya yasotupasa kufanya japo kwa siri
kubwa. Baada ya kumaliza chuo, Zulekha alichumbiwa na kuolewa na
Mkurya mmoja mfanya biashara aishiye Kimanzichana. Tuliendelea
kuwasiliana na mara moja moja kucheza mechi za wizi pindi ambapo mumewe
yupo safarini. Nami miaka minane mbele nilibahatika kumpata huyu mke
wangu ambaye leo tunatimiza miaka miwili ndani ya ndoa.
Alinipigia simu kunijulisha kuwa mumewe amesafiri kwenda Geneva hivyo
kama ningeweza niende walau tukumbushie kwani ulikuwa ni muda mrefu
sana umepita tangu tukutane. Nami bila kumuwaza mke wangu nikamkubalia
na kumjulisha kuwa ningesafiri Jumapili ya tarehe 27 kwa kisingizio cha
safar ya kikazi Mtwara.
Na hivyo ndivyo nilivyomuaga mke wangu kipenzi. Alisikitika kuwa
nisingekuwepo siku ya kuadhimisha miaka miwili ndani ya ndoa yetu
changa. Ilinibidi kutumia one of those magic words, “Sorry babes, I
will make it up to you when I come back.” Alinisaidia kupaki na
kunisindikiza hadi Mbagala rangi tatu nikapande basi ili yeye arudi na
gari letu nyumbani, an Audi A3 sportback, one of my favorites.
Nilipanda basi la Hamanju kuelekea Mtwara ingawa kondakta alikuwa
akifahamu kituo changu cha ukweli. Hivyo tulikubaliana nikampa alfu
kumi anishushe kimanzichana kituoni ambapo nilimkuta Zulekha akiningoja
kwa hamu ndani ya ki-vitz alichonunuliwa na mumewe.
Tulienda hadi kwake ambapo hatukupoteza muda na kuanza kulicheza game
kwani tulikuwa na zaidi ya miezi tisa hatujawahi onana kabisa. Ulikuwa
ni mtanange wa kukata na shoka na mtoto kutotumwa dukani kwa takribani
dakika hamsini hivi ndipo kipenga cha kwanza kilipopulizwa kuashiria
muda wa mapumziko.
Uchovu wa safari, mgongano wa mawazo kwa jinsi nilivyomuacha mke wangu,
pamoja na uchovu wa mechi vilichangia kuingia katika dimbwi la
usingizi ambao kwa mara ya kwanza nahisi siku hiyo sikukoroma. Nilikuja
kustuka nasikia maumivu makali kwenye paji la uso. Kufumbua macho
nilikutana na sura ya Mkurya mwenye hasira kali akiwa kashikilia panga
mkononi. Hasira yake tu ilinitosha kuzimia kwa hofu ila nilijikaza na
kutaka kunyanyuka ambapo alinizaba na ubapa nikajikuta nimejikunyata
pembeni mwa kitanda.
Kumbe Mkurya yule alipoaga anaenda Geneva alimaanisha tu anaenda zake
Arusha ila kilichonikera mimi ni tabia yake ya ‘kutokutanguliza koti
nyumbani.’ Wakati nakua babu alituhadithia kuwa zamani walipokuwa
wakirudi kutoka safari za mbali iliwabidi wafikapo kijiji kimoja kabla
ya nyumbani kutanguliza koti lake kwa mkewe kupitia mmojawapo wa watoto
wa kijiji hicho kuashiria kuwa mwenye ynumba yu karibu. Hii ilimpa mke
nafasi ya kusafisha nyumba na kama kuna kidumu ndani kuhakikisha
kinaondoka na mke kujiandaa kumpokea mumewe. Walijua hali kama hizo
hazina budi kutokea, ila haikuwa sababu ya kumfuamia mkewe.
Babu alituambia zama zetu zimebadilika lakini kutanguliza koti ni
muhimu ila kwa kipindi chetu kutanguliza koti ni sawa na kupiga simu
siku moja kabla ya kufika, “Mke wangu, kesho natarajia kuondoka hapa
Arusha saa mbili asubuhi kurudi nyumbani.” Inatosha! Ghafla kabla
sijaweza kuzama zaidi kwenye mawazo mwanaume yule alinvamia na kuanza
kunikata vibaya mikononi na panga lile la kichwani ndilo lilinipoteza
fahamu kabisa.
Back at home, Msongola…
Mke wangu naye alipokea simu iliyomtaarifu kuwa mumewe yu mahututi
Muhimbili kutoka kwa namba asiyoifahamu na kabla hajamuuliza ni nani
simu ilikatwa. Alipata shida kufahamu kuwa nilipata ajali au ni nini
hasa kwani kwa kawaida huwa ni mvivu kuangalia taarifa ya habari mpaka
nimlazimishe. Hivyo hakufahamu kama jana yake kulitokea ajali yoyote au
la.
Aliondoka haraka na kuja hospitali ambapo alipoulizia kuhusu mgonjwa
aliyeletwa usiku wa kuamkia tarehe 28 kwa ajali hakuna aliyempatia
jibu. Kwa haraka alimpigia simu dr. Kindonga na kumuuliza kama amepata
taarifa zozote kuhusu mumewe. Dr. Kindonga naye alimjibu hana taarifa
na hawezi kufuatilia kwani alikuwa akijiandaa na mitihani yake ya
mwisho ya Masters.
Baada ya kuhangaika sana alifanikiwa kufika mapokezi ICU na kuwakuta
manesi ambao waliona aibu hata kumweleza baada ya kuwatajia jina langu.
Walimwambia tu, “Yupo ndani!” bila kutaja sababu ya mimi kuwepo huko.
Alifika ndani na kunikuta nimefungwa bandeji uso mzima…
Kuanzia hapa anasimulia mke wangu kipenzi: mwallu
Moyo ulinipasuka na kushindwa kuelewa ni nini hasa kilimpata mume wangu
Mentor. Sikuweza kumuangalia hata mara mbili kwani machozi yalinitoka
ghafla. Nilijikuta nikianguka chini na kupoteza fahamu. Nilishtuka niko
mikononi mwa nesi aliyejitambulisha kwangu kama Samira. Alinitaka
nikaze moyo nikajue jinsi ya kumtibu mume wangu kwani kwa hali
aliyonayo alinihitaji nikiwa hai kuliko mfu. Baadaye nilikuja kugundua
Samira alikuwa very sympathetic kwa kuwa hakuwa amefahamu nini hasa
kilimsibu mume wangu.
Nilijikaza na kwenda mpaka kitanda alicholazwa Mentor. Zaidi ya macho
yake na pua zilizotiwa mirija kila sehemu, huko kwingine kulikuwa
kumezibwa kabisa. Daktari alikuja na kujitambulisha;
Dokta: “Habari dada, naitwa Dokta Chrispin”
Mimi: “Shikamoo dokta, naitwa Asante. Dokta nini kimempata mume wangu?”
Dr. Chrispin (Akakohoa kwanza): “Mh! Dada (ingawa kwa vigezo vyote
angetosha kuwa babu yangu!), pole sana. Mumeo alipatwa na ajali.
Alifumaniwa na kupigwa ndo unamuona ha… ”
Dokta Chrispin hakumalizia sentensi ile nikazimia tena kwa mara ya pili
(ingawa ilikuwa ni afadhali kwani nilikuwa nipige ukunga wa kufa mtu).
Nilishtuka nipo ofisini kwa Dr. Chrspin nimelala kwenye examination
bed yake. Alikuja kunipima mapigo ya moyo na kunibembeleza huku
kanikumbatia kifuani mwake. Nililia sana na baada ya kutulia ndipo
aliponimalizia mkasa wote. Sikuamini kama mume wangu Mentor angeweza
kufanya vile. Sikuamini kama katika siku zote basi ingekuwa siku ya
kumbukumbu ya ndoa yetu. Sikuamini hadi nilipooneshwa jalada la Polisi
likielezea kila kitu kwa kinaga ubaga.
Dr. Chrispin alinitaka niende nyumbani nikaongee na ndugu na jamaa ili
kupanga mipango ya matibabu kwani gharama zake zilikuwa kubwa kiasi
kutokana na majeraha aliyoyapata hasa kichwani. Nilichukua nguo zake
nikaziweka kwenye begi ambalo nilikuwa nimemsaidia kupaki asubuhi ya
jana yake na kurudi nyumbani.
Nilianza kuwapigia simu kaka zake. Kaka yao wa kwanza Laurian alishtuka
kwanza ila baada ya kumuhadithia mkasa wote alinijibu kuwa hawezi
kutoa pesa kwa ajili ya upumbavu wa mtu mmoja na isitoshe anajenga.
Familia yake haiwezi kuishi nyumba ya kupanga. Alimalizia kwa kusema,
“Huyo mumeo nilishamuonya mara nyingi sasa basi umalaya wake usiniletee
umaskini kwenye familia yangu.”
Kaka Kabezi, ambaye baada yake ndiye Mentor alizaliwa, alikuwa mtu wa
pili kumjulisha. Yeye kwa kejeli kabisa aliniambia, “Shem, afe tu
tukurithi!”
Nililia sana usiku ule nikashindwa hata kula wala kunywa chochote. Ni bahati tu mtoto wetu Cedric alikuwa kwa bibi yake.
Nilijaribu kuwapigia wifi zangu walau wao wangeweza kunisaidia kwani
walionekana zaidi kumpenda kaka yao na walikuwa karibu naye kuliko kaka
zao wengine. Mawifi nao hawakuwa msaada wowote kwangu.
Wifi mkubwa, Suraya, aliniambia hatoweza kunisaidia kwani anajiandaa
kwenda nje ya nchi asubuhi kesho. Wifi anayefuatia, Dora, sista du
kweli alinijibu hatoweza kutoa chochote ila ataleta chakula hospitali
na kuanzia siku hiyo akawa hapokei tena simu yangu. Wifi mdogo, tena
afisa wa Jeshi la Magereza, aliniambia yuko radhi kwenda kumlipia
mfungwa atoke gerezani kuliko kutibu Malaya. Na Malaya huyu ni kaka
yao, mume wangu. Moyo uliniuma sana nikakosa cha kufanya.
Marafiki zake; Willian, Alfred, Livingstone, Salvatory, Shabani, Peter,
Aneth, Arnold, Dotto, Mary, Christine na wengine wengi wote
walijifanya kuwa bize au hawana uwezo wa kumsaidia ilhali hao hao
walikuwa marafiki wake wakubwa akiwa mzima.
Wengine kama kina Alfred na Willian walidiriki kunitongoza kabisa kwa
ahadi za kunisaidia. Nilimlilia Mungu na kumuomba aniepushe na jaribu
hili. Nilimuomba anioneshe mlango mwingine wa kutokea kwani niliamini
upo. Ukweli nilishindwa kuomba muda mrefu kwani niliishia kulia na
kulala hapo hapo nilipo.
Huku hospitali Dr. Chrispin akaanza kunisumbua nifanye haraka kwani
nikichelewa sana mume wangu hatapona hata akifanyiwa hiyo operation.
Ikanibidi kwenda kumlilia Dr. Chrispin.
1st February 2019, Friday
Niliwahi hospitali kwenda kumhudumia mume wangu ambaye hadi wakati huo
alikuwa amelazwa tu ICU bila matibabu yoyote ya ziada. Nilienda
kumwangukia Dr. Chrispin kumuomba anisaidie. Nilikuwa nimekuja na ile
Audi ya mume wangu nikamwambia dokta ikiwezekana achukue hiyo amtibu
mume wangu na akipona tutamlipa fedha la asipopona basi aichukue gari
hiyo. Dr. Chrispin alinijibu tu, “Dada, hizo gari zipo chache sana hapa
nchini nitakuwa chambo cha kuibiwa na kuuwawa mimi.” Akakataa katukatu
akaniambia; “Ila dada…ukinifikiria vyema nitakusaidia ” Hukuhitaji PhD
kumuelewa mzee yule asiye na haya. Ila kwa muonekano pia wa sura yake
alikuwa serious.
Nilirudi nyumbani kwa majonzi makubwa kwani dokta Chris ndo alikuwa
tegemeo la mwisho katika matumaini yangu ya kumuokoa mume wangu
kipenzi. Nilianza kutafuta ATM cards za mume wangu walau nikaangalie
ana kiasi gani kimebaki benki na kama kinaweza kutosha kusaidia kulipia
matibabu yake. Kumbe ndugu zake walipokuja kunisalimia waliondoka na
kadi zote za benki. Ilikuwa ni kama wameshaamua ndugu yao afariki.
Sikukuta chochote kwenye wallets zake ila wakati narudishia kadi
nyingine kwenye wallet ndipo kikadondoka kikaratasi kilichokunjwa
vizuri. Ilikuwa ni barua;
“
Mke wangu kipenzi,
Kama unaisoma barua hii ni dhahiri kuna jambo baya limenikuta. Na
zaidi sana najua litakuwa linahusika na umalaya wangu. Najua kuomba
msamaha sitakuwa nimekusaidia kwa lolote. Ila ni ombi langu unisamehe,
zaidi sana kwa mzigo ambao nitakuwa nimekutwisha.
Umalaya wangu umeniponza mke wangu na kamwe nisingependa kosa langu
hilo liwe mzigo kwako mke wangu. Jitahidi kuwataarifu ndugu zangu
watakusaidia. Kaka zangu na dada zangu pamoja na marafiki zangu. Kwa
bahati nzuri unafahamiana nao vyema mke wangu.
Pia unaweza kuuza hiyo audi yangu itasaidia kwa gharama zozote hata
ikitokea nimefariki. Tafadhali mke wangu, nyumba hiyo niliiandikisha
kwa ownership ya mwanetu ili kwa vyovyote vile ndugu wasijaribu
kukuibia. Usiiuze.
Mke wangu kipenzi (hata sidhani kama bado nastahili kukuita
hivyo!), kama yote yakishindikana tafadhali usifanye jambo lolote zaidi
ya hilo litakalokufanya ujutie maisha mbeleni. Ni heri uniache nife
kwa dhambi zangu kuliko kutenda dhambi nyingine kuniokoa mimi. Najua
ulivyo mzuri mke wangu, Asante. Watakutongoza wengi wakati huu wakijua
una shida, tafadhali sana mke wangu usiwakubalie. Narudia tena, ‘Ni
heri nife kwa dhambi zangu walau nitakuwa mfano wa kutoigwa kwa wengine
wenye tabia kama yangu.’
Jambo la mwisho mke wangu. Yote hayo yakishindikana rudi kwa Mungu
wako unayemuamini na uniombee mke wangu. Hiyo ilikuwa moja ya sababu
iliyonivuta kwako. Mlilie yeye akusaidie kwani hawa wa duniani wote
wakishindwa kusaidia basi ama kwa hakika Mungu yule niliyekufahamu
ukimuamini atakusaidia.
Nisamehe tena mke wangu na niombee msamaha kwa mwanetu Cedric ikitokea nimefariki.
Wako,
Mentor.”
Ilimaliza barua hiyo na kunifanya nijisikie mnyonge kuliko alivyotarajia mume wangu.
Ila jambo moja katika ile barua lilinitia moyo, alipoongelea imani
yangu. Nikajiuliza I wapi imani yangu? Nikajilaumu kwa kwenda kutafuta
msaada kwa binadamu. Nakumbuka nilipiga magoti pale pale na kumlilia
Mungu kuwa mimi mja wake sikustahili adhabu na aibu kama ile. Ni kweli
mume wangu nampenda kama ahadi yetu ya ndoa ilivyosema, ‘kwenye shida
na raha’ . Nikamwambia Mungu kama kweli yu pamoja nami basi katika
jaribu lile anipe mlango wa kutokea.
Kwa mara ya kwanza siku ile tangu ajali ya mume wangu niliweza kuomba
muda mrefu bila kulia. Nilijihisi kama naongea naye uso kwa uso. Naam,
Mungu hakupi jaribu lililo juu ya imani yako wapendwa kwani katika
ndugu na marafiki zake wote nilioongea nao nilimsahau Felix. Huyu
aliwahi kufanya kazi na mume wangu wizara moja wakati wameanza kazi
baada ya kumaliza chuo. Yeye alisikia kwa watu kuwa rafiki yake amepata
ajali akaja moja kwa moja nyumbani na kuniuliza kama nina shida yoyote
nikamueleza kila kitu ila ukweli ni kuwa moyoni nilikuwa na wasiwasi
asijekuwa kama wenzake akaanza kunitongoza pia.
Felix aliniambia yeye kama yeye asingeweza kunisaidia ila kuna Msambaa
mmoja, Iggy, anamfahamu anaweka bond magari kama niko tayari tukaweke
bond Audi ya mume wangu nipewe pesa ya kumtibu. Nilikubali na siku
hiyohiyo jioni mume wangu alifanyiwa operation na Dr. Chrispin.
Ilimchukua miezi minne kupona kabisa na kurudi nyumbani. Gharama ambazo
kwa hakika hatukuweza kulipa hivyo ilibidi walichukue gari lake pamoja
na cellica niliyokuwa nimenunua mwaka 2013 kwa mkaka mmoja hivi.
Ingawa ni kama alinihonga kwa bei aliyoniuzia.
Ama hakika mke wa mtu sumu wapendwa ila pia Mungu ni mweza wa yote.

Sikujua kama mume wangu katika hali ile aliyokuwa nayo angeweza kupona na kama ningeweza kupata msaada wowote.
Wasalaam wapendwa,
@Mentor & mwallu.
SOURCE: JAMII FORUM
NINI MAWAZO YAKO KATIKA BARUA HII TUANDIKIE HAPO CHINI