
Mashabiki wa Simba na Yanga wakitambiana wakati wa maandamano maalumu
yaliyofanywa kutangaza Nani Mtani Jembe inayoendeshwa na Kilimanjaro
Premium Lager kwa mashabiki wa timu hizo jana, Dar es Salaam.
Dar es Salaam. Saa chache kabla ya pambano,
rekodi za miaka 48 iliyopita zinaonyesha Yanga imewafunga wapizani wake
wa jadi, Simba magoli 112 dhidi ya 98 katika mapambano 97 waliyokutana
tangu 1965 hadi sasa.
Simba na Yanga zitashuka kwenye Uwanja wa Taifa,
Dar es Salaam kesho kukabiliana katika pambano la Ligi Kuu Tanzania Bara
litakalopigwa kuanzia saa 10 jioni.
Gazeti hili lilifanya uchunguzi wake na kubaini
kuwa kuanzia mwaka 1965 hadi mwaka huu,Yanga ina rekodi nzuri zaidi ya
kucheka na nyavu tofauti na Simba.
Rekodi hizo zinaonyesha,katika kipindi hicho,
Simba na Yanga zilikutana katika mashindano tofauti mara 97, ambapo
Yanga ilipachika wavuni magoli 112 wakati Simba ilizamisha magoli 98.
Hata hivyo, katika kipindi hicho, Simba ndiyo
inashikilia rekodi ya kushinda mabao mengi zaidi kupitia mechi moja
baada ya kuitwanga Yanga mabao 6-0 katika pambano lililofanyika Julai
16,1977.
Katika pambano hilo mabao ya Simba yalikwamishwa
wavuni na Abdalah Kibaden aliyefunga matatu dakika za 10, 42 na 89,
Jumanne Hassan ‘Masimenti’ aliyefunga mawili dakika za 60 na 73 na lile
la kujifunga la beki wa Yanga, Selemani Sanga dakika 20.
Pia, Kibaden ambaye sasa ni kocha wa Simba
anajivunia rekodi binafsi ya kupachika mabao matatu kwenye mchezo mmoja
ambayo hakuna aliyeivunja mpaka sasa.
Rekodi ya juu zaidi ya ushindi wa Yanga katika
pambano dhidi ya Simba ni mabao 5-0 iliyoyapata katika pambano
lililopigwa Juni mosi 1965 wakati huo Simba ikiitwa Sunderland.
Katika mchezo huo, Yanga ilijipatia mabao yake
kupitia kwa Maulid Dilunga aliyefunga mawili dakika za 18 na 43, Salehe
Zimbwe dakika 54 na 89 na Kitwana Manara dakika ya 86.
Lakini, mwaka jana Simba iliichabanga Yanga mabao
5-0 katika mechi ya mwisho ya Ligi Kuu Bara na mechi ya mwisho msimu
uliopita ya ligi hiyo, Yanga ilishinda 2-0.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni