HISTORIA YAKE
John Pombe Joseph
Magufuli alizaliwa tarehe 29 Oktoba 1959 huko wilayani Chato Mkoani Kagera
(hivi sasa Chato ni wilaya ya mkoa mpya wa Geita) na atatimiza miaka 56 Oktoba
mwaka huu.
Magufuli alianza
elimu ya msingi katika Shule ya Msingi Chato wilayani Chato mwaka 1967 na
alihitimu mwaka 1974. Alifaulu na kujiunga na Shule ya Seminari Katoke,
Biharamulo ambako alisoma kidato cha Kwanza na cha Pili mwaka 1975 - 1977,
akahamishiwa Shule ya Sekondari Lake, Mwanza ambako alisoma kidato cha Tatu na
Nne mwaka 1977 - 1978.
Masomo ya kidato cha
Tano na Sita aliyapata mkoani Iringa katika Shule ya Sekondari Mkwawa kati ya
mwaka 1979 na 1981. Halafu alirudi Chuo cha Ualimu Mkwawa kusomea Stashahada ya
Elimu ya Sayansi akibobea kwenye masomo ya Kemia, Hisabati na Elimu; hii
ilikuwa mwaka 1981 – 1982.
Alipopata stashahada
yake, moja kwa moja alikwenda kuanza kazi ya ualimu katika Shule ya Sekondari
Sengerema, akifundisha masomo ya Kemia na Hisabati. Ajira hii aliifanya kati ya
mwaka 1982 na 1983.
Kisha alijiunga na
Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) kwa mujibu wa sheria akianzia Makutupora, Dodoma
(Julai - Desemba 1983), kisha akaenda kambi ya Makuyuni, Arusha (Januari hadi
Machi 1984) na akamalizia katika kambi ya Mpwapwa mkoani Dodoma (Machi – Juni
1984).
Mwaka 1985 alijiunga
Chuo Kikuu cha Dar es Salaam akisomea Shahada ya Sayansi ya Elimu akibobea
kwenye masomo ya Kemia na Hisabati na alihitimu mwaka 1988.
Mwaka 1989 - 1995
alifanya kazi katika kiwanda cha Nyanza Cooperative Union (Ltd.) akiwa mkemia
na wakati huohuo alianza masomo ya shahada ya uzamili ya Sayansi katika Chuo
Kikuu cha Salford nchini Uingereza, kikishirikiana na Chuo Kikuu cha Dar es
Salaam ambako alisoma kati ya mwaka 1991 na 1994.
Magufuli aliendelea
na elimu ya juu zaidi kwa maana ya Shahada ya Uzamivu ya Kemia kuanzia mwaka
2000 hadi 2009 ambayo aliihitimu katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam na kuwa
mhitimu wa shahada ya udaktari. Dk Magufuli ana mke, watoto na familia imara.
MBIO ZA UBUNGE
Dk Magufuli alianza
mbio za ubunge mwaka 1995, alipojitosa katika jimbo la Chato kwa tiketi ya
Chama Cha Mapinduzi (CCM) na kushinda wakati akiwa na miaka 36. Rais Benjamin
Mkapa akamteua kuwa Naibu Waziri katika Wizara ya Miundombinu. Kazi ya Ubunge
na unaibu waziri ilimpeleka salama hadi mwaka 2000.
Uchaguzi wa mwaka
2000 ulipoitishwa, Dk Magufuli aligombea na kushinda kwa mara ya pili. Rais
Mkapa akamteua kuwa Waziri wa Wizara ya Miundombinu na akakaa hapo hadi kipindi
cha uongozi wa Mkapa kilipokamilika.
Mwaka 2005 aliendelea
kutupa karata jimboni kwake kuwania ubunge kwa kipindi cha tatu. Akaingia
kwenye orodha ya wabunge waliopita bila kupingwa. Lakini safari hii, Rais
Jakaya Kikwete alimteua kuongoza Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi
hadi mwaka 2008 alipohamishiwa Wizara ya Mifugo na Uvuvi, ambayo aliiongoza
hadi mwaka 2010.
Mwaka 2010 wana CCM
wa Chato hawakuchoka kumpa ridhaa Dk Magufuli, hii ikiwa mara ya nne. Mara hii
hakupita bila kupingwa, alipambana na mgombea kutoka Chadema, Rukumbuza
Vedastus Albogast ambaye alifanikiwa kumtoa jasho Magufuli.
Katika uchaguzi ule
alipata ushindi wa asilimia 66.39 dhidi ya asilimia 26.55 za mgombea wa
Chadema. Na baada ya kuchaguliwa kuwa mbunge kwa mara ya nne, Rais Kikwete
alimrudisha katika Wizara ya Ujenzi ambako yuko hadi hivi sasa.
MBIO ZA URAIS
Dk Magufuli ni mmoja
wa wana CCM ambao wamekuwa wakitajwa sana kuwa anaweza kuwa mgombea sahihi wa
CCM baada ya kipindi cha Rais Kikwete kumalizika. Lakini yeye mwenyewe amekuwa
akikana na kutotaka kuhusishwa na kinyang’anyiro hicho. Hata hivyo, watu wa
karibu na Dk Magufuli wanasema kuwa ameshafuatwa na vigogo wakubwa ndani ya CCM
wakimwomba, wakati ukifika, achukue fomu. Yeye amekuwa na msimamo kuwa anapaswa
kupima hali ya mambo kabla hajaamua kujihusisha na urais au la.
NGUVU ZAKE
Nguvu ya kwanza ya
Magufuli iko katika uwezo wake wa kielimu. Inawezekana kuwa elimu si kila kitu
katika siasa, lakini ukweli unabakia kuwa mwanasiasa mwenye elimu ya kutosha
akiwa na sifa nyingine za kushika wadhifa fulani, ana nafasi kubwa sana ya
kufikiriwa kuliko yule ambaye hana elimu. Katika hili Magufuli amejizatiti na
amebobea sana. Elimu ukiichanganya na ujana vinamfanya awe mgombea wa umri
ambao ni karata muhimu ndani ya CCM.
Lakini jambo lingine
linalompa nguvu, ni kukaa kwa muda mrefu katika wizara zake. Amekuwa Naibu
Waziri wa Miundombinu kwa miaka mitano na pia Waziri wa Miundombinu wakati wa
Mkapa; akaongoza wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kwa miaka
mitatu kabla ya kuongoza ile ya Uvuvi na Mifugo kwa miaka miwili. Lakini pia
tangu mwaka 2010 hadi hivi leo ameiongoza Wizara ya Miundombinu bila
kuhamishwa. Jambo hili hulikuti kwa mawaziri wengi sana, hasa katika serikali
ya Kikwete.
Jambo la tatu
linalompa nguvu ni umakini na na uwezo wa kusoma na kuchambua nyaraka. Watu
wanaofanya kazi na Dk Magufuli, kote alikopita wanasema kuwa, tofauti na
mawaziri wengi waliowazoea ambao huhitaji kuchambuliwa taarifa hadi
zirahisishwe, kwake ni tofauti. Yeye husoma kila jambo na kwamba anatumia muda
mwingi sana kusoma kila taarifa na hadi anaweka mistari na michoro kwenye
taarifa.
Mhandisi mmoja ambaye
amewahi kufungiwa leseni na Magufuli anasema kuwa kosa moja kubwa alilofanya ni
kumwandikia Magufuli taarifa ndefu lakini yenye uongo kwenye aya moja. Anasema
kuwa aya hiyo ilikuwa iko ukurasa wa 20 lakini ndani ya muda mfupi “Magufuli
aliibaini na kibarua chake kiliota nyasi”. Utendaji huu wa kufuatilia hadi
vilivyomo kwenye maandishi ndani kabisa, umewashinda wanasiasa na viongozi
wengi, Magufuli anabebwa na jambo hilo.
UDHAIFU WAKE
Moja ya udhaifu
mkubwa wa Dk Magufuli ni tabia ya “kufanya maamuzi haraka”. Baadhi ya watendaji
wa wizara yake wanasema kuwa anafanya maamuzi haraka mno na kuna wakati
inaonekana maamuzi yake hayana tija, au ni ya kung’ang’ania tu kwa sababu za
kimsimamo. Kuna mambo kadhaa ambayo yamekuwa na madhara makubwa katika wizara
alizoziongoza:
Kwa mfano, uamuzi
alioufanya wa kukamata meli iliyotuhumiwa kufanya uvuvi haramu na kukiuka
sharia, haukuwa na tija kwa taifa kwani baada ya kesi ile kwisha, serikali
iliamriwa kulipa kiasi cha shilingi za Kitanzania bilioni 2.8 pamoja na
kurudisha meli husika kwani mahakama ilijiridhisha kuwa ilikuwa inafanya
shughuli zake kihalali.
Lakini pia amewahi
kufanya mazoezi ya “bomoa bomoa” kwa haraka mno tena kuna wakati bila
kuzingatia haki za binadamu za wanaovunjiwa nyumba na makazi yao. Hii, ndiyo
sababu Waziri Mkuu Mizengo Pinda, tena akiwa katika ziara ya Wilaya ya Chato
alimtaka kutumia nguvu hizo kutumikia wananchi. Baadaye Rais Kikwete alifafanua
watu wanaostahili kubomolewa nyumba kuwa ni wale waliofuata barabara na siyo
wale wa asili na ambao barabara imewafuata. Kwa hiyo, wale ambao wamefuatwa na
barabara wanastahili kulipwa fidia.
Kosa jingine kubwa
linalompa Magufuli udhaifu usiomithilika, ni uamuzi na ushiriki wake katika
mpango haramu wa uuzaji wa nyumba za serikali ambao ulilalamikiwa sana wakati
akiwa Waziri wa Nyumba. Katika nchi ambayo wafanyakazi hawana nyumba na
serikali inahitaji sana viwanja katika maeneo maalum, haikutarajiwa uamuzi wa
namna ile ungekuwa na tija. Uamuzi ule uliisababishia serikali hasara kubwa na
uliacha manung’uniko mengi maana hata wasio wafanyakazi wa serikali, nao
walinufaika na nyumba zile.
NINI KINAWEZA
KUMFANYA APITISHWE?
Suala la kwanza
linaloweza kumvusha Dk Magufuli kwenye chekecheo la wagombea ndani ya CCM ni
uchapakazi na nidhamu kazini. Magufuli ni mchapakazi na mimi binafsi namwona
kama waziri mchapakazi kuliko mawaziri wote ambao wamebahatika kufanya kazi
kwenye serikali ya Kikwete. Ikiwa CCM inahitaji Rais ambaye atakuwa na uwezo
mkubwa wa kutenda na kusimamia kazi, basi Magufuli ndiye anaweza kabisa
kuchukua nafasi.
Jambo jingine
linaloweza kumvusha Magufuli ni msimamo. Yeye ni kiongozi mwenye misimamo
isiyotia shaka. Hajui kuuma maneno lakini anajua nini anachokisimamia.
Watendaji wa Wizara ya Miundombinu wanasema ni vigumu kumyumbisha Magufuli
katika jambo ambalo anaona hilo ndiyo njia, lazima mlitekeleze kwanza. Tabia ya
namna hiyo alikuwa nayo Mwalimu Julius Nyerere, kwamba akishaamua jambo fulani
na kama anajua njia yake, humtoi relini.
Alipokuwa Waziri wa
Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi alithubutu hata kumtaja Naibu wake kwamba
anahodhi viwanja. Mwaka 2013, aliwashangaza watu wakati alipopishana hadharani
na Waziri Mkuu Pinda, kuhusu suala la magari ya mizigo kupita katika barabara
yakiwa yamezidisha uzito.
Baada ya Pinda
kuruhusu, Magufuli aliweka msimamo kuwa jambo hilo halikubaliki na
halitekelezeki na akalipiga marufuku. Baadhi ya watu walichukulia msimamo wa
Magufuli kama dharau kwa Waziri Mkuu wake lakini wanaomfahamu wanasema angekuwa
tayari kufa na msimamo wake. Ikiwa CCM wanahitaji mgombea urais mwenye sifa ya
msimamo thabiti, namwona Magufuli akiwa mbele kabisa.
Jambo la tatu ni
kutokuwa na makundi. Kati ya mambo ambayo yanaiumiza CCM hivi sasa ni ikiwa
itajikuta imepitisha mgombea mwenye makundi na anayeweza kuleta migawanyiko.
Chama hicho kinahofia kuwa mtu wa namna hiyo atakosa uungwaji mkono wa makundi
yanayosigana na hivyo anaweza kuangushwa kwenye uchaguzi kutokana na vita ya
ndani ya chama.
Pamoja na Magufuli
kuwa waziri muhimu sana kwenye serikali ya Kikwete, angeweza kuwa mtu wa maana
kwenye makundi ya kusaka urais lakini amejiweka pembeni sana. Kwa sababu ya
kusimama katikati, anaweza kabisa kuwa mmoja wa watu watakaoonekana wanastahili
kupewa nafasi ili kutuliza nguvu ya makundi. Kuna wakati Samuel Sitta alidai
kwamba wakati ukifika atashirikiana na marafiki zake Bernard Membe, Harrison
Mwakyembe pamoja na Magufuli kumchagua anayefaa kuwania urais, lakini Magufuli
alikana na kujiweka kando na kundi hilo.
Kingine kinachoweza
kumpitisha ni kufahamika na kuuzika. Bila shaka CCM inahitaji mgombea
anayeuzika na kufahamika ili kupunguza mishale ambayo itakuwa inapigwa na UKAWA
dhidi ya taswira ‘mbaya” ya chama hicho. Ili kujitoa katika hatari hiyo nadhani
Magufuli anaweza kuvushwa.
Na mwisho, Magufuli
anaweza kuvuka mchujo kwa sababu ya taswira yake kwa Rais Kikwete. Kama
tunavyofahamu, rais anayeondoka anakuwa na mchango mkubwa katika kusababisha
uteuzi wa rais ajaye na tayari kuna viashiria vingi mno vinavyoonesha kuwa
Kikwete huenda anamchukulia Magufuli kati ya wana CCM wachache anaowaamini.
Kikwete amewahi
kuhutubia mkutano mmoja Kanda ya Ziwa na wananchi wakawa hawamsikilizi, bali
alipopanda jukwaani Magufuli, wananchi wakanyamaza na Kikwete akarudishiwa
kipaza sauti akaendelea na hotuba yake huku akisisitiza kuwa Magufuli ni
kiongozi imara.
Lakini kama hiyo
haitoshi, Rais Kikwete alipotoka kwenye matibabu nchini Marekani aliwahi
kunukuliwa akisema “…nilitaka kutangaza mapema kuhusu ugonjwa wa kansa uliokuwa
ukinisumbua, lakini Magufuli ndiye alinikataza kufanya hivyo wakati wa kikao
cha Baraza la Mawaziri”. Kauli hii ya Kikwete inachukuliwa kama dalili ya
kuonesha ni jinsi gani anamwamini Magufuli. Na hata katika hotuba zake Dk
Magufuli hakosi kumsifu Dk Kikwete.
NINI KINAWEZA
KUMWANGUSHA?
Jambo la kwanza
linaloweza kumwangusha Magufuli ni dhana ya “ugeni” ndani ya CCM. Magufuli
hakuwahi kuwa kiongozi wa CCM na hakuwahi kuitumikia CCM. Yeye amefanya kazi
serikalini kisha akawa mbunge, na kwa miaka 20 sasa amekuwa waziri na si
kiongozi wa CCM. Wahafidhina na watu wasiokubali mabadiliko ndani ya CCM
wanamchukulia kama “mtu wa kuja” kwenye chama chao na ikiwa sauti zao zitakuwa
nyingi anaweza kuangushwa.
Kitu cha pili ni
misimamo yake. Misimamo inaweza kumvusha Magufuli kwenye mchujo wa wagombea wa
CCM, pia inaweza kabisa kumwangusha. Ikiwa upitishaji wagombea utafanywa kwa
lengo la kupata mtu ambaye ikiwa atakuwa rais atakuja kuendeleza mitandao,
kujuana na kubebana, nadhani Magufuli ataogopwa. Misimamo yake katika baadhi ya
mambo imekuwa ikiwakwaza makada wa chama hicho ambao wangependa ulaji uendelee
kuwepo, kwa hiyo, sifa hii inaweza kutumika kumpunguza.
Jambo la mwisho
linaloweza kumwengua kwenye safari hii ni kukosa kundi kubwa ndani ya chama
linalomuunga mkono. Ndani ya CCM, kwa wanachama wa kawaida, naambiwa hata
katika vikao vya chama hicho, Magufui hana uungwaji mkono mkubwa. Hali hii
inaweza kuwa kikwazo kwake, hasa itakapotokea kuwa makundi makubwa ya wasaka
urais yakapenya na kufanikiwa kuteka mwelekeo wa maamuzi ya chama hicho.
ASIPOPITISHWA (MPANGO
B)
Magufuli anaweza kuwa
na mipango miwili muhimu kwa sasa. Kwanza, kuendelea na ubunge katika jimbo la
Chato. Pamoja na kuwa hali yake ya kisiasa ndani ya jimbo si salama sana kwa
maana ya nguvu ya UKAWA kuzidi kuwa kubwa, bado anaweza kurejea na akafanikiwa
na huenda, kama chama chake bado kitachaguliwa kuongoza dola baada ya uchaguzi,
anaweza kupenya na kuchukua nafasi ya juu zaidi ya uwaziri.
Pili, aaweza kurudi
chuo kikuu ili kufundisha vijana. Kama tunavyofahamu nchi yetu iko kwenye
kampeni kali ya kuhamasisha vijana wasome sayansi na Magufuli ni mwanasayansi
aliyebobea katika masomo ya Kemia na Hisabati. Atakuwa na fursa nzuri sana ya
kulisaidia taifa kukuza uwezo wa taaluma ya vijana katika maeneo aliyobobea.
HITIMISHO
Wahenga walisema,
“mwenda pole ndiye hula vinono”. Mipango ya kimya kimya ya Magufuli katika
safari ya ikulu kupitia CCM inaweza kuwa na maana kubwa sana. Tayari
tumekwishaona makada wote wa chama hicho ambao walianza safari hiyo kwa fujo na
mbwembwe wakionywa na kuwekwa kwenye uangalizi maalum. Inawezekana Magufuli
alisoma “mchezo” huu mapema na akawa hataki “kudandia treni kwa mbele”.
Nachokiona mimi ni kuwa Magufuli ni mmoja wa wana CCM tishio
sana dhidi ya makundi makubwa ya vigogo ambayo yamejipanga kuingia ikulu muongo
mmoja uliopita. Namtakia ndugu John Pombe Joseph Magufuli, safari salama na ya
heri katika mbio hizi.
Source jf