Jumanne, 16 Julai 2013

Marekani yaendelea kutenda jinai nchini Pakistan


Ndege zisizo na rubani za Marekani maarufu kama 'Drone' zimeendelea kufanya mashambulizi katika maeneo ya kikabila ya Waziristan, kaskazini magharibi mwa Pakistan licha ya upinzani mkali kutoka kwa serikali na wananchi wa nchi hiyo. Ripoti zinaonyesha kuwa, siku ya Jumapili Julai 14 takriban watu 9 waliuawa katika mji wa Mir Ali huko Waziristan baada ya Marekani kudondosha mabomu ikitumia ndege zake zisiso na rubani. Tokea mwaka 2004, Marekani kwa kutumia kisingizio cha kupambana na ugaidi, imekuwa ikishambulia eneo hilo la kikabila la Waziristan kwa mabomu na takwimu zinaonyesha kwamba, hadi sasa Washington imefanya mashambulizi zaidi ya 350 na kusababisha vifo vya zaidi ya watu 3000 katika eneo hilo. Duru mbalimbali zinaripoti kuwa, wahanga wengi wa mashambulizi hayo ni raia wa kawaida hususan akina mama na watoto.
Serikali, wananchi, vyama vya kisiasa na mashirika ya kijamii nchini Pakistan yamekuwa yakipinga jinai hizo za Marekani na kusisitiza kwamba mashambulizi ya Washington huko Waziristan ni kinyume na sheria za kimataifa.
Wachambuzi wa masuala ya kisiasa wanaitakidi kwamba, mashambulizi ya ndege zisizo na rubani za Marekani katika eneo la kikabila la Waziristan huko Pakistan yamemuweka katika hali ngumu Waziri Mkuu wa nchi hiyo, Nawaz Sharif ambaye siku baada ya siku anakabiliwa na maswali mengi kutoka kwa wananchi kuhusu jinai hizo za Washington. Itakumbukwa kwamba, moja kati ya ahadi alizotoa Nawaz Sharif wakati wa kampeni za kabla ya uchaguzi wa mwezi Mei ni kukabiliana na mashambulizi ya ndege za Marekani zisizo na rubani na kuhakikisha mashambulizi hayo yanakomeshwa. Ni kutokana na ahadi hiyo ndio maana kiongozi huyo akawatumia barua viongozi wa vyama vya siasa, wale wa kidini na wale wa mashirika ya kijamii kwa ajili ya kuwaalika kwenye kikao kitakachojadili masuala ya usalama na kuandaa ramani ya njia itakayoainisha jinsi ya kukabiliana na mashambulizi hayo ya Marekani.
Kwa sasa Pakistan inakabiliwa na changamoto mbili kubwa za kiusalama. Changamoto ya kwanza ni mashambulizi ya kigaidi ya mara kwa mara yanayotekelezwa na makundi ya kigaidi, na ya pili ni hujuma za angani za Marekani huko Waziristan. Mawili hayo yanatarajiwa kupewa kipaumbele kwenye mkutano huo wa kujadili usalama wa taifa utakaofanyika baadaye mwezi ujao.
Serikali ya Islamabad inasisitiza kwamba, mashambulizi hayo ya angani ni ujumbe wa wazi kwamba Marekani haiheshimu uhuru wa kujitawala wa Pakistan wala haina heshima yoyote kwa wananchi wa nchi hiyo. Marekani imekuwa ikidai kwamba, mashambulizi yake yanawalenga wanamgambo wa Taliban na imekuwa ikitumia vyombo vyake vya habari kuonyesha kwamba, wanaouawa kwenye hujuma hizo ni magaidi ingawa ukweli wa mambo ni kuwa, wahanga wakubwa ni raia wa kawaida wasio na hatia.
Alaa kullihal, weledi wa mambo wanaamini kwamba, Waziri Mkuu Nawaz Sharif anaweza kufanya mazungumzo na Marekani ili mashambulizi hayo ya anga yasitishwe lakini kwa upande mwingine atalazimika kuikinaisha Washington kwamba kwa kutumia jeshi la Pakistan, anaweza kukabiliana na makundi ya kigaidi katika eneo la Waziristan lenye milima mingi.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni