Matumaini
pekee ya nchi ya kucheza fainali za michuano ya kimataifa kabla ya 2015
yaliyobaki yalianza kuyeyuka jana baada ya timu ya Taifa Stars kufungwa
1-0 na majirani Uganda kwenye Uwanja wa Taifa.
Katika mechi hiyo ya kwanza ya kuwania
kucheza fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika kwa wachezaji wa ligi za
nyumbani, CHAN, kwa mwaka 2014, bao la Uganda lilifungwa na Iguma Denis
dakika moja baada ya mapumziko.
Kabla ya kufungwa jana, timu ya taifa
ilikuwa imetoka kupoteza nafasi nzuri ya kuendelea kuwania kucheza
fainali za Kombe la Dunia za Brazili za mwakani baada ya kufungwa na
Ivory Coast 4-2 kwenye uwanja huo mwezi uliopita.
Kipigo cha mwezi uliopita kilikuja chini
ya mwaka mmoja tangu Stars inyimwe nafasi ya kucheza fainali za Kombe la
Mataifa ya Afrika, CHAN, za mwaka huu nchini Afrika Kusini na majirani
wengine -- Msumbiji.
Stars na Uganda zitarudiana jijini Kampala
wiki mbili zijazo katika mchezo ambao timu ya taifa ni lazima ishinde
kwa angalau goli 1-0 ili kufufua matumaini ya kucheza fainali za CHAN
kwa mara ya pili tangu 2009.
Kama ilivyokuwa katika mechi iliyopita ya
Taifa Stars dhidi ya Ivory Coast, timu ya nyumbani ilitawala mchezo kwa
muda mwingi wa kipindi cha kwanza lakini ikashindwa kubadili umiliki wa
mpira kuwa magoli.
Ni udhaifu ambao uliadhibiwa vilivyo muda
mfupi tangu kuanza kwa kipindi cha pili na wageni ambao walikuwa na
wachezaji wawili tu wa Uganda Cranes A kutokana na kanuni za michuano
hiyo kuibana.
Uganda ikipanga kikosi dhaifu, Tanzania
ilianza na wachezaji tisa wa kikosi cha kwanza kutokana na kufaidika na
ukosefu wa wachezaji wa ziada ya Mbwana Samatta na Thomas Ulimwengu
wanaocheza soka nje ya mipaka ya nchi.
Timu zilikuwa:
STARS: Juma Kaseja, Erasto Nyoni (David
Luhende dk.45), Shomari Kapombe, Agrey Moris, Kelvin Yondani, Frank
Damayo, Amri Kiemba, Abubakar Salum, John Bocco, Mwinyi Kazimoto (Haruna
Chanongo dk.56), Mrisho Ngassa.
UGANDA: Muwonge Hamza, Waswi Hassan,
Wadada Nico, Majegwa Brian, Kabugo Savio, Kasaga Richard, Iguma Denis,
Said Kyeyune, Mpande Joseph, Edama Patrick, Jur Tony
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni