Jumapili, 28 Julai 2013

Uchaguzi wa urais nchini Mali


Duru ya kwanza ya uchaguzi wa urais nchini Mali imefanyika leo tarehe 28 Julai nchini humo. Viongozi wa nchi hiyo wametabiri kuwa, karibu watu milioni saba wameshiriki kwenye uchaguzi wa leo. Katika duru hiyo, wagombea 27 wamechuana vikali kuwania nafasi hiyo. Hii ni katika hali ambayo Ibrahim Boubacar Keita, waziri mkuu wa zamani wa nchi hiyo na Soumaila Cisse waziri wa zamani wa fedha, wanatajwa kuwa na nafasi kubwa ya kuweza kushinda katika uchaguzi huo. Karibu askari 6300 wa kulinda amani wa Umoja wa Mataifa wamechukua jukumu la kulinda usalama katika uchaguzi huo. Zaidi ya hayo, askari 3200 wa Ufaransa pia bado wako nchini humo, kwa kile kinachodaiwa ni kuvisaidia vikosi vya Umoja wa Mataifa katika kazi zao za kulinda amani. Aidha chanzo kimoja cha usalama nchini Mali kimetangaza habari ya kuweko askari wa kujitolea wapatao 4500, ambao wameandaliwa na serikali ya Bamako kwa minajili ya kudhaminia usalama katika zoezi zima la uchaguzi huo. Habari kutoka Mali zimearifu kwamba, viongozi wengi wa nchi hiyo, wamepiga kura zao mjini Bamako huku wengine wakipiga kura katika vituo rasmi vilivyosimamiwa na polisi ya nchi hiyo. Hata hivyo pamoja na kuwepo askari wote hao, bado kuna wasi wasi wa kutokea machafuko ya baada ya uchaguzi nchini humo. Jana Harakati ya Umoja na Jihadi Magharibi mwa Afrika 'MUJAO', ilitoa vitisho dhidi ya serikali ya Bamako na kuwataka wananchi kutokwenda kupata kura. Aidha harakati hiyo, ilitishia kuwa, wapiganaji wake watafanya mashambulizi dhidi ya vituo vya kupigia kura, hususan katika maeneo ya kaskazini mwa nchi hiyo. Tangu wiki iliyopita, mji wa Kidal wa kaskazini mwa Mali, umekuwa ukishuhudia machafuko yanayofanywa na wapinzani ili kuvuruga hali ya usalama nchini humo. Kufichuliwa bomu la kutengenezwa kienyeji karibu na soko la mji wa Kidal, kumezitia khofu nyoyo za raia wa kawaiada kuhusiana na usalama wa eneo hilo. Aidha utekaji nyara wa watu ni suala lingine lililozua khofu kubwa katika uchaguzi wa leo. Wiki iliyopita, meya wa mji wa Kidal na mmoja wa wafanyakazi wake, walitekwa nyara. Wapiganaji wa Harakati ya Kitaifa ya Azawad waliisimamisha gari ya meya huyo, katika lango la kuingilia mji huo na kuwateka nyara watu wawili kati ya wanne waliokuwamo ndani ya gari hilo akiwemo meya huyo. Pamoja na hayo yote lakini weledi wa mambo wanaamini kwamba, kufanyika uchaguzi wa leo, ni hatua moja mbele kuelekea kwenye utawala mpya kikatiba nchini humo. Si vibaya kukumbusha hapa kwamba, uchaguzi wa leo umefanyika ikiwa ni baada ya kupita miezi sita, tangu Ufaransa ilipoingilia kijeshi mgogoro wa Mali. Aidha uchaguzi wa leo umefanyika katika hali ambayo, zaidi ya watu 500,000 wanaishi kwenye kambi za wakimbizi wa ndani na inaaminika hawakupata fursa ya kujiandikisha kama wapiga kura. Wakosoaji wanasema kuwa, jamii ya kimataifa imeishinikiza Mali kufanya uchaguzi katika hali ambayo nchi hiyo ilikuwa haijajiandaa kikamilifu kwa ajili ya zoezi hilo. Hata hivyo, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki moon amesema uchaguzi ndiyo njia pekee ya kurudisha demokrasia katika nchi hiyo ya magharibi mwa Afrika. Weledi wa mambo wanaamini kuwa, rais ajaye nchini Mali atakuwa na majukumu makubwa na hatari, hasa kwa kuzingatia mgogoro na vitisho vya wapinzani wa kaskazini mwa nchi hiyo, umasikini mkubwa na kuzorota hali ya uchumi. Wakati huo huo, wachambuzi wengine wa mambo wanaamini kuwa, uungaji mkono wa jamii ya kimataifa kwa serikali ya Bamako na ahadi kemkem za kuipatia nchi hiyo msaada wa Euro bilioni tatu, ni katika mambo yanayotia matumaini ya kutatuliwa mgogoro wa nchi hiyo.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni