Habari kutoka Dar es Salaam zinasema kuwa, Katibu wa Jumuiya na
Taasisi za Kiislamu Tanzania, Sheikh Ponda Issa Ponda yupo chini ya
ulinzi huku akitibiwa majeraha katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili.
Sheikh Ponda alisafirishwa usiku wa manane kutoka Morogoro baada ya
kupigwa risasi juzi alipokuwa akisindikizwa na wafuasi wake kwenda
katika Msikiti wa Mungu Mmoja Dini Moja mara baada ya kumaliza kutoa
mhadhara katika kongamano mjini hapo. Mwenyekiti wa Kongamano hilo,
Sheikh Idd Mussa Msema, alidai kuwa Sheikh Ponda alipigwa risasi tatu
begani na maafisa wa polisi waliokuwa wakijaribu kumkamata. Taarifa
kutoka ndani ya familia ya Ponda zinasema kwamba baada ya kupata taarifa
za kupigwa risasi, baadhi ya masheikh walifunga safari kwenda Morogoro
na kumrejesha Dar es Salaam usiku huohuo. Kabla ya kurudishwa Dar es
Salaam, imeelezwa kuwa Sheikh Ponda alipelekwa katika Zahanati ya
Islamic Foundation kabla ya kusafirishwa hadi Hospitali ya Taifa ya
Muhimbili kwa ajili ya kupatiwa matibabu. Polisi wanaendelea kushika
doria Muhimbili huku ikitangazwa kuwa kiongozi huyo wa Waislamu ametiwa
mbaroni na yuko chini ya ulinzi wa polisi.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni